Friday

NADHARIA YA TENDO UNENI (Do things with words) ya Austin 1962 pdf

0 comments
NADHARIA YA TENDO UNENI
Nadharia hii ilianzishwa na mwanafalsafa John L. Austin (1962) katika kitabu chake cha ‘how to do things with words’. Huyu alidai kwamba mara kuna mambo mengi tunatenda kwa kunena, yaani kwa maneno tu tusemayo tunatenda. Kwa ujumla nadharia hii ni majibu/pingamizi dhidi ya madai/mtazamo wa wanafalsafa mantiki na Masharti Ukweli wanaodai kwamba kazi kuu ya lugha ni kueleza, kufafanua au kualifu mambo mbalimbali.
Katika nadharia hii Austin anafafanuna kwamba si sentensi zote hufanya kazi ya kuarifu jambo katika lugha na pia si sentensi zote tunazoweza kupima ukweli au usikweli wake.
Pia anasema kuwa kuna sehemu kubwa ya mawasiliano ya binadamu huhusisha maswali, mishangao, amri, na namna mbalimbali za kuelezea hisia au matakwa ya watu. Hapa alikuwa na maana kuwa lugha hufanya kazi nyingine kama vile kushangaa au kuuliza swali. Kwa mfano:-
  • Niwie radhi
  • Wewe ni mhudumu hapa?
  • Chipsi mayai mishikak tafadhali
Semi zote hizi haziarifu jambo na hivyo haziwezi kusema kuwa kweli au si kweli. Anaendelea kwa kusema kuwa hata sentensi ambazo kimuundo ni maelezo si zote zote zinatumika kueleza au kuarifu jambo na hivyo si zote zinaweza kupimwa ukweli au usikweli wake.
  • Kwa hayo machache nafunga rasmi mkutano
  • Nakuonya sheria zitafuata mkondo wake
  • Nakukaribisha sana katika harusi yangu
  • Naweka dau kwamba Brazil itanyakua kombe la dunia mwaka huu
Sentensi hizi zote hufanya kazi zaidi ya kutoa taarifa au kuelezea jambo. Sentensi hizi ni vitendo au sehemu ya vitendo ambavyo msemaji anavisema kwa kutenda kwa njia ya kusema. Hii ina maana kuwa kusema kwa sentensi hizo ndio kutenda kwake.
Semo Tendeshi na Vitenzi Tendeshi
Austin anasema kuwa semo tendeshi ni zile ambazo kusemwa kwake huwa ndiko kutendwa kwa vitendo vinavyodokezwa na vitenzi vinavyotumika.
Vitenzi Tendeshi
Vitenzi tendeshi ni vitenzi ambavyo kusemwa kwake ndio kutendwa kwake. Baadhi ya vitenzi hivyo ni kama vile: ahidi, onya, karibisha, alike, kemea, shauri, omba radhi, nk Austin anasema kuwa si kila semo ni semo tendeshi wala si kila kitenzi ni kitenzi tendeshi. Kwa mfano vitenzi kama vile –pika, washa gari, heshimu, oa hivi si vitenzi tendeshi.
Madai ya Tendo Uneni
Nadharia ya tendo uneni hudai kuwa viambo vya lugha vina uwezo wa kutenda aina fulani fulani ya matendo ya kimawasiliano kuelekeza, kuahidi, kuomba radhi nk. Unenaji wa viambo hivyo ndio utendaji wa matendo yanayodokezwa na vitenzi husika kaika viambo hivyo. Kila kinachotendwa kwa kunena tu au kutoa tu semo fulani ndicho huitwa tendo uneni.
Masharti ya Tendo Uneni Austin anasema kuwa matendo uneni hayakamiliki kwa sababu tu vitenzi tendeshi vimetumika. Kuna masharti ya uneni ambayo lazima yatimizwe ndipo tendo uneno husika ikamilike. Yeye anabainisha masharti sita na kuyagawa katika makundi matatu (A, B na C)
Kundi A.
  • Lazima kuwe na utaratibu kaida (ambao ni universal-unaojulikana ulimwengu mzima) juu ya utendaji wa tendo hilo na kwamba athari ya tendo hilo ijulikane mahali pote.
  • Mazingira na watu wanaohusika katika uneni wa tendo husika lazima yawe muafaka
Kundi B.
  • Utaratibu wa kutenda/kutekeleza tendo husika lazima ufuatwe kwa usahihi
  • Utaratibu huo lazima pia ufuatwe kikamilifu.
Kundi C.
  • Aghalabu wahusika wawe na mawazo huria na dhamira ya kweli ya kufanikisha tendo husika
  • Iwapo shughuli/wajibu ambao anatakiwa kutimiza baada ya tendo uneno unafahamika basi ni lazima wahusike watekeleze.
Hali Malidhawa katika Matendo Uneni
Austin anafafanua kuwa ili tendo uneni likamilike na kukubalika ni lazima kuwe na kile alichokiita hali malidhawa kinachohalalisha tendo husika. Hali malidhawa ni jumla ya vitendo na sifa ambazo tendo uneni husika huhitaji ili kukidhi/ili liwe halali au litimie. Kwa kiasi kikubwa hali malidhawa imetokezwa katika sifa ya matendo uneni.
Hali malidhawa inahusu mambo yafuatayo:-
i) Nani anayeongea/nena/uliza/anayetenda tendo uneni.
ii) Ananena nini
iii)Anasema kwa nani/anamnenea nani?
iv) Ananena wapi
v) Ananena kwa sababu/lengo gani
Kwa mfano; wewe ni nani unayenihukumu miaka 20 jela? Wewe ni nani unayenibatiza?
Miundo ya Matendo Uneni
Ili kujua vizuri miundo ya matendo uneni ni muhimu kukumbuka uainishaji wa sentensi uliofanywa na wanafalsafa mantiki ambapo wanafalsafa hao walizigawa katika makundi matatu;
Maelezo, Maelekezo na Swali.
Miundo ya matendo uneni hupatikana kwa kuangalia kiwima au kiukinzani kati ya sentensi na dhima ambayo sentensi hiyo inakumbatiwa/kuibeba. Miundo hii iko kama ifuatavyo:-
  1. Matendo Uneni Dhahiri
Haya ni matendo uneni ambayo huonesha kiwima kati ya aina ya sentensi na dhima ambayo inabeba. Mfano wa maelezo: Kaka yangu ni dereva wa daladala, Watanzania tumejifunza mengi kutokana na ushindi wa Uhuru Kenyata.
Mfano wa maelekezo: Weka dawa mahali pasipofikiwa na watoto, Marufuku kutupa takataka katika eneo hili—kimuundo si maelezo ila ni maelekezo yenye amri na ombi.
Mfano wa maswali; Familia yenu ina watu wangapi? Mbali na Wamasai ni watu gani wengine wanaojihusisha na ufugaji?
  1. Matendo uneni yasiyo dhahiri
Haya ni matendo ambayo aina ya sentensi haiwiani bali inakinzana. Kwa mfano:- Unaweza kumkopesha shilinga elfu kumi—sentensi hii kimuundo ni swali lakini dhima ni ombi. Kwa hiyo inafanya tendo uneni lisilo dhahiri. Mfano mwingine Njaa inaniuma sana—kimuundo sentensi hii inatoa inatoa taarifa lakini dhima ni kuomba chakula.
Kwa hiyo katika muundo huu ni kuwepo kwa muundo tofauti na dhima.
Aina za Matendo Uneni Austin (1962) ametaja aina tatu:-
  1. Kile kisemwacho
Aina hii inahusu usemi wa sentensi yoyote yenye maana inayoeleweka pia iwe na kitu kinachorejelewa.
  1. Lengo la kusema/kunena
Hii inahusu lengo la kile msemaji anachokisema au anachokiongea. Lengo la kile msemaji anakiongea kinatengeneza tendo uneni. Kwa mfano mwanafunzi anawaambia wenzake ‗mwalimu anakuja‘—badala ya kuwaambia waache kelele, wanafunzi wanaosikia mwitiko huu wanaweza kuitika tofauti tofauti. Wengine kwa kunyamaza, wengine kuzomea au wengine kuendelea kupiga kelele tu.
  1. Matokeo ya kisemwacho
Inahusu athari/matokeo ya kile kisemwacho kwa msikilizaji. Matokeo ya kisemwacho kwa msikilizaji inaweza kuwa iliyokusudiwa au haikukusudiwa. Kwa ufupi aina hii inahusu majibu ya msikilizaji kimwili,kimaneno, kisaikolojia, kiakili nk.
Aina za Matendo Uneni Zilizoboreshwa John Searle (1975) aliboresha aina za matendo uneni. Katika uboreshaji wake alisema kwamba kuna aina nyingi sana za matendo uneni na labda hazina ukomo. Hii ni kwa sababu aina hizo hutegemea lengo, muktadha na lugha husika. Hivyo akapendekeza aina za ziada za matendo uneni. Baadhi ya aina alizopendekeza ni hizi zifuatazo:-
  1. Ahadi
Haya ni matendo uneni ambayo humfunga mnenaji katika utekelezaji wa kile alichokinena kwa siku za baadaye. Mfano wa vitenzi kwa tendo uneni hii ni; tuza, ahidi, zawadi, nk lazima utekeleze.
  1. Maelekezo/ Directives
Haya ni matendo uneni ambayo hulenga kuchochea jambo fulani lifanyike na msikilizaji kama atakavyo msemaji. Vitenzi vinavyoweza kutumika ni pamoja na; amrisha, omba, onya, shauri, pendekeza, sihi nk. Kwa mfano;
Tunapendekeza jaribio la Pragmatiki lifanyike Alhamisi badala ya Jumatano
Nakusihi uachane na kile kivulana chako cha chuo
  1. Hisia (Expressive)
Haya ni matendo uneni ambayo hudhihirisha hisia, imani, mitazamo au mawazo ya msemaji juu ya jambo fulani. vitenzi kama vile; shukuru, pongeza, sifu, fariji, samehe nk hudhihirisha. Kwa mfano
  • Nimeamua kukusamehe rafiki yangu
  • Nashukuru kwa wema wako
  1. Matamko
Ni matendo uneni ambayo hunenwa kwake hubadili ukweli fulani wa mambo katika dunia. Vitenzi vinavyoweza kutumika ni kama vile; jiudhuru, achisha kazi, fungua (mkutano), funga (mkutano), hukumu, oza(mke au mume), tangaza, kupa jina nk. Kwa mfano;
  • Kuanzia leo nimekuachisha kazi
  • Kuanzia sasa natangaza kwamba Wiliam na Helena ni mume na mke
  • Naufungua mkutano rasmi, mjisikie huru kuchangia hoja
  1. Uwakilisho
Haya ni matendo uneni ambayo hueleza kile ambacho mnenaji haamini kuwa ni kweli au si kweli. Matendo uneni ya aina hii hujumuisha maelezo, shadidia au mahitimisho kwa mfano:-
  • Lulu hakumuua Kanumba
  • Wanaume si waaminifu katika mahusiano
  • Wasichana wa mjini hawana mapenzi ya kweli
  • Wanaume siyo waaminifu katika mahusiano
  • Kada yule hatapitishwa na chama chake kugombea urais na chama chake mwaka huu
  • Yule mwanao wa pili wa kiume ni shoga

No comments:

Post a Comment