Wednesday

DHANA YA FASIHI LINGANISHI, Historia na kuibuka kwake

0 comments
Katika kazi hii ya tulioyojikita kujadili mambo yaliyopelekea kuibuka kwa fasihi linganishi, tumeigawa kazi yetu katika  sehemu  tatu ambazo ni utangulizi, kiini na hitimisho. Katika utangulizi tumeelezea dhana ya ulinganishi, dhana ya fasihi linganishi kwa kutumia wataalamu mbalimbali na historia ya fasihi linganishi.  Katika kiini  cha swali tumeonesha sababu zilizosababisha kuibuka kwa fasihi linganishi na mwisho  tumehitimisha kwa kuuangalia umhimu wa fasihi linganishi.

Dhana ya fasihi linagnishi.
Kabla ya kuangalia dhana ya fasihi linganishi ni vema kuanza na dhana ya kulinganisha. Kulinganisha ni dhana ya kufanya tathmini ya vitu viwili au zaidi ili kujua ubora, kufanana, na kutofautiana kwa vitu hivyo. Mtu anayehitaji kufanya ulinganisho ni lazima atahitaji kwanza kuwa na mahitaji maalumu kwa ajili ya kazi hiyo. Mahitaji hayo ni kama vile; maarifa ya ujuzi juu ya vilinganishwavyo, kuwepo kwa vitu viwili au zaidi vinavyolinganishwa na kuwepo kwa kigezo au vigezo  maalumu vya kulinganisha. Wataalamu mbalimbali wamefasili dhana ya fasihi linganishi kama ifuatavyo;
Henry Remak (1971), anafasili fasihi linganishi kama uwanja wa kifasihi unaohusika na uchunguzi na mahusiano ya kifasihi nje ya mipaka ya nchi moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo. Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Remak fasihi linganishi haiishii kuangalia mahusiano ya kifasihi peke yake bali huangalia mahusiano  kati ya fasihi na fani nyinginezo zisizo za kifasihi.
Kwa mujibu wa Boldor (2003), akimrejelea Compbell (1926), anaeleza kuwa, fasihi linganishi ni taaluma inayochunguza uhusiano uliopo baina ya fasihi mbili au zaidi nje ya mipaka ya kitaifa kwa njia ya kulinganisha mfanano na msigano.
Kwa mujibu wa Totosy de Zepetnek (1996), anafafanua dhana ya fasihi linganishi kuwa ni stadi ya sayansi ya jamii ijihusishayo na ulinganishaji wa fasihi na matokeo mengine ya shughuli
Wamitila (2003), anaizungumzia dhana hii kuwa ni mbinu ya kuchunguza, kuchambua, na kueleza sifa za mfanano zilizopo katika matini ya fasihi.
Kwa ujumla tunaifasili dhana ya fasihi linganishi kama taaluma inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa uhusiano na usigano uliopo baina ya fasihi mbili au zaidi zinazohusisha vipengele tofauti vya kiutamaduni , itikadi na historia.
Historia ya fasihi linganishi
Fasihi linganishi imetokana na maneno ya kifaransa “ la literature compere” yenye maana ya comperative literature kwa lugha ya kiingereza ikiwa na maana ya fasihi linganishi kwa lugha ya Kiswahili. Fikra za kulinganisha fasihi za jamii au mataifa mbalimbali ni za kale zaidi ikilinganishwa na sura ya ulinganishaji  ilivyo hivi sasa kama nyanja ya kitaaluma. Fasihi linganishi misingi yake ilianza kuonekana katika jamii za kale za kiyunani zilizokuwa na nguvu za kihadhi mathalani zama za mwanafalsafa wa kizamani wa kiyunani Aristotle. Pia jamii za baada ya kristo zilihusisha na ulinganishaji na ulinganuzi wa matini za kidini (Biblia). Kadhilika wasanii wa kiarabu wa enzi za kati walihusisha na ulinganishaji na ulinganuzi wa kazi za sanaa. Hata na hivo pamoja na kufanya ulinganishaji wa kazi za kisanaa katika zama hizo ni wazi kuwa suala lenyewe la ulinganishaji lilikuwa linafanywa kwa misingi ya kipwekepweke na isiyo na taaratibu zinazojulikana na walinganishaji wengine hususani wa maeneo mengine ya ulimwengu. (Basnell 1993).
Sababu za utokeaji wa fasihi linganishi
Ponera (2014) anataja Sababu za utokeaji wa fasihi linganishi zinajikita katika historia na maendeleo ya kisansi na teknolojia. Sababu za kihistoria  kama vile safari zilizofanywa na wataalamu mbalimbali duniani, watu binafsi waliokuwa wanafanya kazi kiupweke pweke, misukosuko ya kifikra, mwingiliano na upanuzi wa hadhira. Sababu ya  maendeleo ya sayansi na teknolojia ni  Udigitishaji.
Safari zilizofanywa na wataalamu mbalimbali duniani. Inakadiriwa  kuwa katika karne ya 19 wataalamu mbalimbali kutoka Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla walifanya safari katika mataifa mbalambali duniani. Wakiwa katika safari zao walikuta kulikuwa na tofauti za kifasihi ambazo waliweza kuzibaini katika utendaji wa fasihi katika jamii hizo, hususani katika fasihi simulizi. Tofauti hizo walizoweza kuzibaini ndizo kwa namna moja au nyingine ziliamsha urazini wao  wa kuzilinganisha na kuzilinganua fasihi na sanaa hizo. Kwa mfano mtaalamu aitwae Veselovsky alitumia muda mrefu kwenda Italia kujifunza jinsi wenyeji wa huko walivotenda shughuli mbalimbali za sanaa. Shughuli hii aliifanya karne ya kumi na tisa. Kimsingi yeye mtaalamu huyu ndiye aliyefungua njia katika kufanya shughuli mbalimbali za fasihi linganishi Urusi (Ponera 2014, uk 92)
Watu binafsi waliokuwa wakifanya kazi kiupweke pweke. Hawa  walitoa mchango mkubwa sana katika kuibuka, kuitangaza na kuieneza fasihi linganishi. Maarifa ya awali ya taaluma hii yalijikita katika kulinganisha maudhui ya sanaa na kaida za maisha ya kila siku ya binadamu na   mambo yanayomzunguka, hivyo kutokana upweke waliokuwa wanaupata watu hao binafsi katika ufanyaji wao wa kazi ulipelekea kuibua fasihi linganishi. Mfano wa mambo hayo ni kama vile; dini , siasa, na matabaka. Baadhi ya watu waliofanya kazi kiupweke pweke ni pamoja na Paul van Tieghem ambaye aliendesha makongamano huko Sorbonne kati ya mwaka 1827 na 1840. Pia aliandika na makala na vipeperushi kuhusu dhana ya fasihi linganishi na kuzisambaza katika sehemu mbalimbali huko ulaya na kwingineko duniani.
Misukosuko ya kifikra; msukumo mkubwa unaojitokeza katika fasihi linganishi ni ule unaojielekeza katika utoshelevu wa taaluma yenyewe. Hii inatokana na ukweli kuwa taaluma hii inaruhusu mwingiliano wa taaluma mbalimbali nyingine kama vile; tafsiri, nadharia ya uhakiki, anthropolojia, masomo ya dini, historia na Jiografia. U-mseto huo ndio uliosababisha kuibuka kwa fasihi linagnishi kwani wataalamu mbalimbali walianza kulinganisha taaluma moja na nyingine, vipengele tofauti ndani ya taaluma moja, na vipengele vinginevyo. Hivyo basi taaluma ya fasihi linganishi inaonwa kuwa ni somo la utafiti wa fasihi bila mipaka. Muono huu hutokana na misingi ya  fasihi linganishi ambayo ni ujuzi na uwezo wa kusoma, kuandika na kuchunguza na kuhakiki hadhi za kazi ya jamii mbalimbali.
Jambo lingine lililopelekea kuibuka kwafasihi linganishi ni Muuingilian. Kuwako  kwa fasihi linganishi hutokana na sababu kadhaa, sababu mojawapo ni ile inayohusisha na muingiliano wa jamii mbalimbali za hapa duniani. Muingiliano huo kwa namna moja au nyingine, huzilazimisha jamii mbalimbali kutagusana katika masuala kadhaa likiwamo suala la fasihi. Hatima ya mtagusano huo ni kusana kazi za fasihi kwa kutumia muelekeo wa tamaduni wa jamii nyingine. Mfano mzuri hapa ni muingiliano wa jamii za Afrika mashariki na wale wa mashariki ya kati. Baada ya jamii hizi mbili kushirikiana kwa muda mrefu sana, ulifika wakati wa kuwa sehemu ya jamii hiyo, mfano; watu wa mashariki ya kati walilazimika kusana kazi ya fasihi yao kwa kutumia utamaduni wa watu wa upwa wa bahari ya hindi, kwa hakika kazi hizi hazikuzungumzia kabisa masuaka ya watu wa upwa huo, badala yake zilijikita kusawiri masuala ya huko mashariki ya kati kwa kutumia lugha ya watu wa upwa huo. Muingiliano huo uliwalazimu wataalamu wa fasihi kuona kuwa kuna sababu za kuzilinganisha kazi za fasihi zenye mielekeo tafauti ya kiutamaduni na zilizoibuka kama zama tofauti ili kusitiri matakwa ya jamii husika kifasihi. Kwa kufanya hivyo ndipo kulijitokeza dhana ya fasihi linganishi.
Jambo lingine lililopelekea kuibuka kwa fasihi linganishi ni upanuzi wa hadhira. Dhana  hii ya upanuzi wa hadhira huenda pamoja na ukuaji wa masoko ya kazi ya fasihi. Baadhi ya watunzi wa kazi za fasihi walipata wazo la kuongeza idadi ya wasomaji au wasikilizaji wa kazi zao. Hivyo walilazimika kuzitafsiri kazi zao katika lugha za kule walikolenga kuwafikia wasomaji. Kwa kufanya hivyo walijikuta wameingia katika dhana hii ya fasihi linganishi. Mfano wa kazi za fasihi linganishi ni alfulela ulela, mabepari wa venissi, safari za Guliva, hekaya za abunuwasi na safari za saba Sindbad Baharia.
Udigitalishaji. Kabla ya majilio ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika dunia ya kwanza, mwamko wa  dhana ya fasihi linganishi hapa ulimwenguni ulikuwa ni wa kiwango cha chini  ukilinganishwa na mwamko baada ya teknolojia. Baada  ya jamii kuishi katika kipindi cha uduni wa kiteknolojia kwa muda mrefu hatimaye ilianza kuhama na kuelekea katika matumizi ya nyenzo kadhaa za kiteknolojia. Kipindi hiki kilitambulishwa sana na ugunduzi, matumizi na usambaaji wa kompyuta hapa ulimwenguni, hapo ndipo jamii ilipoingia katika hatua mpya ya kutumia mifumo mipya ya kama vile mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA). Dhana ya TEHAMA kwa ujumla wake hujumuisha vipengele, hatua, na mifumo itumikayo katika kuchakata, kutengeza, kusambaza, kuwasilisha, kutumia, na kuhifadhi viambata mbalimbali  ya habari. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia jamii imeweza kujifunza, kusoma, na kufuatilia kazi za fasihi kutoka katika mataifa mbalimbali kupitia mitandao kama vile televisheni, radio, tovuti na mitandao ya kijamii kuwasiliana na kubadilishana nyaraka mbalimbali, hivyo ilipelekea wataalamu wa fasihi kuanza kuzilinganisha na kuzilinganua ili kubaini dhima na mapungufu ya kazi hizo kifani na kimaudhui. (Ponera 2014 uk 143 na uk 145).
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na historia mbalimbali ndiyo yaliyochangia kuibuka kwa fasihi linganishi ambayo imepelekea jamii kuweza kulinganisha fasihi kutoka katika mataifa mbalimbali na kutambua ufanano na uhusiano na usigano wa fasihi. pia fasihi linganishi imesaidia kufahamu masuala mabalimbali ya ulimwengu, kihistoria, itikadi, imani, mabadiliko ya jamii na maendeleo ya fasihi ya ulimwengu.

















                                                             MAREJEO
Wamitila, K .W. (2003), Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Group Books: Nairobi.
Remark ,H.H.(1971), Comparative Literature: its definition  and Function. Southern illios :      
                                   Carbondale.
Basnell, S,(1993), Comparative literature.  A critical Introduction: Oxford University.  
                              Blackwell.
TUKI , (2004). Kamusi ya  Kiswahili Sanifu. Oxford  University Press. Nairobi.
Ponera, A.S.(2014). Utangulizi wa Nadharia ya Fasihi Linganishi. Karljamer Print Technology:  
                          Dar es Salaam.
Totosy de, Z. (1996). Essays in Reader Oriented Theory, Criticizes  and Pedagogy. Michigan
                                  Technological University: Michigan

No comments:

Post a Comment