Benard Odoyo Okal
IKISIRI
Kamusi kadhaa wahidiya (za lugha moja) za Kiswahili kama vile Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la kwanza, pili na tatu, zimewahi kutungwa kutokana na juhudi za Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) inayojulikana sasa kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ili kusaidia mafunzo ya Kiswahili na taaluma ya leksikografia katika taasisi kadhaa za elimu. Kamusi nyingi wahidiya za Kiswahili zimetungwa kwa kutumia mitindo anuwai ya utoaji maelezo ya taarifa muhimu za vidahizo husika licha ya kwamba kuna lugha kienzo maalum ya kuzingatiwa katika kuwasilisha taarifa hizo za vidahizo. Hivyo basi, makala haya yanahakiki kiulinganifu wa taarifa muhimu kuhusu vidahizo katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la tatu (TUKI, 2013) na Kamusi ya Karne ya 21 (Mdee, Njogu na Shafi, 2011). Uhakikiki linganishi katika makala haya umehusisha masuala anuwai hasa maelezo ya idadi ya vidahizo, mpangilio wa vidahizo, taarifa za kisarufi (tahajia na matamshi, kategoria ya kidahizo, ngeli, uelekezi wa vitenzi, mofolojia hasa minyambuliko ya vidahizo, maana na matumizi ya vidahizo katika miktadha anuwai) pamoja na vipengee vingine vya lugha kienzo ya msimbo kwa mujibu wa taaluma ya leksikografia.
1.0 UTANGULIZI
Utungaji wa kamusi ni sanaa ya kipekee ambayo ilianza kuonekana katika karne ya 5 Kabla ya Kristo na kushamiri kule Uchina, Uyunani na Roma na hatimaye kusambaa kote ulimwenguni (Crystal, 1987). Hadi sasa, utungaji wa kamusi za aina tofauti ungali unaendelezwa na watu binafsi na taasisi anuwai. Shughuli za utungaji wa kamusi wahidiya ya Kiswahili zilianzishwa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kutokea kubuniwa kwake mwaka wa 1930 hadi mwaka wa 1964 wakati Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ilipoundwa (Mbaabu, 1996). Hata hivyo, kabla ya taasisi hii kuanza shughuli zake, watu wengine binafsi waliweza pia kutunga kamusi wahidiya na thaniya mbalimbali za Kiswahili kama vile: Dr. L. Krapf, A Dictionary of the Swahili Language - 1882, Rev. Canon Binns, Swahili-English Dictionary - 1925, Fredrick Johnson, Kamusi ya Kiswahili - 1935, R. A. Snoxall, Concise English-Swahili Dictionary - 1958, C. Sacleux, Dictionnaire Swahili- Francais - 1939-41 na pia Alfonse Lenselaer, Dictionaire Swahili-Francais – 1975 miongoni mwa wengine (Polome,1967; Bakhressa, 1992).
TUKI imetunga Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la kwanza (TUKI, 1981) na Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la pili (TUKI, 2004). Taasisi hii imetunga pia kamusi za nyanja anuwai. Mbali na TUKI, kuna pia taasisi nyinginezo kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lililotunga Kamusi ya Agronomia na Ufugaji (BAKITA, 1987) miongoni mwa nyingine. Kuna kamusi wahidiya nyinginezo za Kiswahili kama vile Kamusi ya Karne ya 21 (Mdee na wenzie, 2011) na Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la tatu (TUKI, 2013). Licha ya kuwa kuna kamusi za aina mbalimbali na taasisi kadha za utungaji wa kamusi, kuna mitindo anuwai inayotumiwa na wanaleksikografia katika utungaji. Utungaji unaweza kuwa na mitindo mbalimbali; hata hivyo kitu muhimu katika kamusi ni utoaji wa taarifa za vidahizo au leksimu zinazoingizwa katika kamusi ya lugha ili kurahisisha maana yake. Kidahizo ni ‘neno linaloorodheshwa katika kamusi ili litolewe maana zake pamoja na taarifa nyinginezo’ (TUKI, 2004: x).
Kuna aina mbili za vidahizo kama vile kidahizo kikuu chenye umbo la msingi na maana, na kidahizo mfuto ambacho ni kinyambuo kinachoingizwa ndani ya maelezo ya kidahizo kikuu (TUKI, 2001). Kama vile twaa ni kidahizo kikuu ilhali twalia ni kidahizo mfuto ambacho kimeumbwa kutokana na mnyambuliko wa kidahizo twaa na hatimaye kuorodheshwa kama kidahizo kamili katika kamusi. Aghalabu vidahizo katika kamusi yoyote ile huangaziwa kwa kutumia chapa nene au chapa iliyokoza. Hata hivyo, maneno haya (vidahizo) yanapotolewa taarifa nyinginezo kwa mujibu wa kunga za taaluma ya leksikografia, huitwa kitomeo (kidahizo pamoja na taarifa zake zote).
Licha ya kwamba kuna mtindo bia wa kuorodhesha na kupanga vidahizo vya kamusi kama vile kuviandika upande wa kushoto wa makala, kuviandika kwa chapa iliyokoza na maelezo yake kufuatia, wataalamu mbalimbali huelekea kuwa na mitindo mingine ya kuongeza taarifa nyingine muhimu ili kurahisisha matumizi ya kamusi husika. Taarifa hizo ni kama vile za matamshi, mofolojia, sintaksia, semantiki, matumizi kimuktadha na kietimolojia. Makala haya yanatalii taarifa hizi mbalimbali za vidahizo na kuonyesha namna zinavyoshughulikiwa katika kamusi za lugha ya Kiswahili. Maelezo yametolewa ya uchanganuzi wa taarifa muhimu kuhusu vidahizo katika kamusi kwa ujumla na pia uhakiki kiulinganishi wa taarifa hizo muhimu za vidahizo katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la tatu (TUI, 2013) na Kamusi ya Karne ya 21 (Mdee na wenzie, 2011).
Makala yamejengwa kwa msingi wa nadharia ya metaleksikografia (metalexicography). Nadharia ya metaleksikografia ni nadharia pana na ya kijumla inayohusisha masuala yote yanayohusu utungaji na uhakiki wa kamusi (Wiegand, 1983). Nadharia hii ya metaleksikografia hujumuisha nadharia nyingine mahususi: kwanza, nadharia ya historia ya leksikografia inayotoa chimbuko na maendeleo ya taaluma ya leksikografia. Pili, nadharia ya kijumla ya leksikografia inayohusisha uteuzi na matumizi ya kamusi, utoaji fasili za vidahizo na kanuni za utungaji wa kamusi, mpangilio wa vidahizo vya kamusi, na utafiti wa kileksikografia. Tatu, nadharia ya utafiti kuhusu matumizi ya kamusi ambayo aghalabu huangazia sehemu ya utangulizi na tamati ya kamusi. Nne, nadharia ya uhakiki wa kamusi ambayo hurejelea vipengee anuwai vya lugha kienzo (metalanguage) kama vile vya msimbo vinavyohusisha: matumizi ya chapa nene ya kidahizo, kuandika othografia ya kidahizo, fonolojia/matamshi ya kidahizo, kategoria ya kidahizo, semantiki ya kidahizo, matumizi ya kidahizo na kadhalika.
Makala yamejikita katika mtazamo wa utoaji fasili ya vidahizo na uhakiki wa kamusi kwa kuzingatia baadhi ya matumizi ya lugha kienzo ya msimbo. Kamusi hizi mbili zinaelekea kuzingatia mitazamo hii ya metaleksikografia; hivyo basi makala yanalenga kudhihirisha mlingano na tofauti zinazobainika baina ya KKS3 na KK21 kwakuzingatia masuala mbalimbali mahususi ya kileksikografia.
2.0 TAARIFA MUHIMU KUHUSU VIDAHIZO KATIKA KAMUSI
Kamusi wahidiya ya kisinkronia ya lugha iliyotungwa kikamilifu huweza kuwa na sifa ya ujumuishi na ukamilifu kimaelezo (Bright, 1992). Ujumuishi humaanisha kuwa kamusi husika sharti ihusishe masuala mengi kutoka nyanja na taaluma anuwai ili kuimarisha mawasiliano miongoni mwa watumiaji wa lugha husika. Kwa jumla, wataalamu mbalimbali wa masuala ya leksikografia wanasisitiza kuwa taarifa muhimu kuhusu vidahizo katika kamusi huweza kuwekwa katika kategoria kuu kiothografia na kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia kisemantiki/kimaana, kiensaiklopidia na hata kiuhusiano (Bright, 1992; Bussmann, 1996; Frawley, 2003).
Yanayozingatiwa katika masuala ya othografia na fonolojia kuhusu kidahizo ni kama vile tahajia au mwendelezo, silabi na matamshi yake. Matamshi humaanisha jinsi kidahizo kinavyoandikwa kwa kuzingatia alama za unukuzi makinifu za kimataifa kama unavyoonekana katika kamusi kadhaa za Kiingereza.
Masuala ya kimofolojia huangazia kategoria ya kidahizo, umoja na wingi wa kidahizo, ngeli ya kila kidahizo, nomino na vilevile mnyambuliko wa vitenzi katika hali mbalimbali kama vile kutenda, kutendana, kutendeana na kadhalika. Mnyambuliko husaidia uundaji wa vidahizo husika hivyo basi huchangia ongezeko la idadi ya vidahizo katika lugha. Maelezo ya kidahizo kimatumizi aghalabu huangazia matumizi ya kidahizo kimuktadha au kisajili kama vile matumizi yake kidini, kishairi na kibaharia. Vilevile huangazia lahaja chanzi ya kidahizo na matumizi yake kimaeneo.
Kisemantiki, kidahizo huangaziwa kwa kutoa fasili yake kwa mujibu wa kanuni na mbinu mbalimbali za utoaji wa fasili za kidahizo. Kwa kuwarejelea kina Landau (1984), Jackson (1988) na Mdee (1992) kama walivyorejelewa katika Bwenge (1995), utoaji wa fasili hufaa kuzingatia kanuni kama vile kuepuka mzunguko, kuakisi kategoria ya maneno, kuwa fupi, fasaha na rahisi kueleweka huku ikiepuka utata kimaana.
Bwenge (1995) anapomrejelea Gold (1983), anaeleza kuwa mbinu mbalimbali hutumiwa katika utoaji maana au semantiki ya kidahizo katika kamusi kama vile: fasili fafanuzi, fasili elekezi ya kutegemea maoni au hisi ya mtungaji na fasili hiponimi ya kulinganisha na kulinganua leksimu moja ya jumla na nyingine mahususi. Pia kuna fasili antonimu inayoonesha uelekeo tofauti au kinyume wa kidahizo husika, fasili chambuzi inayoonesha sifa za jumla za jamii ya kidahizo na baadaye kutoa ufafanuzi wa sifa mahususi za kidahizo husika. Wakati mwingine, wanaleksikografia huweza kutumia fasili ainishi ya kuonesha sifa asilia ya kinachorejelewa, fasili unde inayotolewa bila kufafanua sifa za kiashiriwa, fasili kanuni inayoonesha jinsi kidahizo kinavyotumiwa na fasili sinonimu ya kuelezea vidahizo visawe au vyenye maana sawa.
Maelezo ya kidahizo kisintaksia huonesha upatanisho wa kisarufi huku sentensi sahihi zikioneshwa. Uelekezi wa vidahizo vitenzi pia huangaziwa moja kwa moja katika maelezo haya ili kumsaidia msomaji kurahisisha matumizi ya kamusi husika. Uelekezi huchangia kuwapo kwa vidahizo vitenzi elekezi ambavyo huweza kuongezewa yambwa na vidahizo vitenzi visoelekezi ambavyo haviwezi kuongezewa yambwa vinapotumiwa katika sentensi. Taarifa kuhusu etimolojia ya kidahizo huonesha asili ya kidahizo husika kama vile Kiingereza, Kiarabu, Kijerumani, Kihindi, Kireno na hata Kifaransa. Maelezo ya kidahizo kiuhusiano au kifahiwa huonyeshwa katika kamusi ili kudhihirisha iwapo vidahizo vinahusiana kisinonimia, kihomonimia na kipolisemia.
Uhakiki linganifu wa taarifa muhimu kuhusu vidahizo umefafanuliwa katika makala haya kwa kurejelea Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la tatu, itakayorejelewa kama KKS3 na Kamusi ya Karne ya 21 itakayorejelewa kama KK21.
2.1Taarifa za vidahizo vya KKS3 na KK21
Taarifa muhimu za vidahizo katika kamusi hizi zimegawanywa katika vipengele vitatu ambavyo ni idadi na mpangilio wa vidahizo polisemi na homonimu, taarifa za kisarufi, na vipengele vingine vya lugha kienzo ya msimbo ili kurahisisha maelezo. Vipengele hivi vitatu vinafafanuliwa kama vifuatavyo:
2.1.1 Idadi na Mpangilio wa Vidahizo
Inadhihirika kuwa KKS3 na KK21 zinatofautiana katika idadi ya maneno na vidahizo kama tunavyoelezwa katika jalada la kila kamusi: KKS3 (TUKI, 2013) na KK21 (Mdee na wenzie, 2011). Idadi hii imepangwa katika jedwali 1lifuatalo:
Jedwali 1: Idadi ya vidahizo katika KKS3 na KK21
Kamusi
Maneno jumla
Vidahizo
Vidahizo vipya vilivyoteuliwa
KKS3
Zaidi ya 285,000
Zaidi ya 25,000
Takriban 2,000
KK21
Zaidi ya 280,000
Vipatavyo 43,000
Vipatavyo 1,000
Vidahizo vyote katika kamusi hizi mbili vimeorodheshwa kialfabeti kutoka A hadi Z. Vidahizo vyenyewe vimeandikwa kwa kuorodheshwa na baadaye kutolewa maelezo yafaayo ya kuvifasili. Vidahizo vyote vimeandikwa kwa chapa iliyokoza. Vidahizo vya KKS3 vimeandikwa kwa rangi ya nili au buluu iliyokoza na vya KK21 vina rangi ya pinki iliyokoza. Kimsingi vidahizo vya lugha huwa na mahusiano kama vile ya kisinonimia, kiantonimia, kihomonimia na kipolisemia. Mathalani, vidahizo vya kamusi vinavyohusiana kisinonimia hurejelewa kama vidahizo sinonimu. Vidahizo sinonimu au visawe humaanisha vile vidahizo ambavyo huwa na maumbo tofauti lakini vyenye maana sawa (Lyons, 1981; Prinsloo, Chuwa na Taljard, 2000; TUKI, 2004; Mdee na wenzie, 2011).
Usinonimia huweza kusababishwa na tofauti za lugha kilahaja, matumizi ya neno kisajili, hisia za watu, kuwapo kwa maneno ya utohozi, matumizi ya misimbo, matumizi ya tasfida, tabia ya kitu na umbali kimazingira baina ya watumiaji lugha husika (Gibbe, 1977). Kuna sinonimu kamilifu na sinonimu karibia inayofanana kimaana na kimatumizi katika baadhi tu ya miktadha (Lyons, 1981). Udhihirishaji wa vidahizo sinonimu katika kamusi za KKS3 na KK21 umeoneshwa kwa kutumia alama ya mkato (,) kama tunavyoona kuhusu kidahizo aibu katika jedwali 2 lifuatalo:
Jedwali 2: Udhihirishaji wa vidahizo sinonimu katika kamusi
KKS3
uk.6
aibu/ajibu/ nm(-) [i-/zi-]jambo livunjialo mtu heshima; fedheha, kinamasi, hizaya, tua, haya, soni, janaa, izara; (mt) ~ya maiti aijuaye mwosha.(>Kar)
KK21
uk.5
aibu nm [i-/zi-] jambo la kumtia mtu fedheha, jambo la kumvunjia mtu heshima; tahayuri, soni (nah) ona aibu jitia aibu tia mtu aibu: Alivua nguo mbele ya watu bila kuona aibu.
Ingawa kuonyesha vidahizo sinonimu au visawe katika kamusi huwa rahisi kutokana na matumizi ya mkato (,), kwa upande mwingine changamoto hutokea katika uingizaji wa vidahizo homonimu na polisemi. Homonimu ni leksimu zilizo na miundo inayofanana lakini zenye maana tofauti ambazo pia hazina uhusiano wa kiasili (Lyons, 1981; Crystal, 1987; Hatch na Brown, 1995; Prinsloo na wenzie, 2000; Fromkin, Rodman na Hyams, 2007). Homonimu huwa na matamshi yanayofanana, tahajia inayofanana hata hivyo huwa na chanzo tofauti (Mojela, 2006). Homonimu huweza kurejelewa vilevile kiothografia kama homografu kwa kuandikwa kwa namna inayofanana na huwa na sifa ya kuleta utata kimaana na kimawasiliano (Bussmann, 1996).
Kwa mujibu wa Allan katika Bussmann (1996), chanzo cha homonimia ni matumizi ya tasfida katika lugha, matumizi ya lahaja na urari au mlingano katika matamshi. Utata kimaana katika homonimia huonekana kwa sababu homonimu moja huweza kuwa katika kategoria ya nomino na kitenzi kwa wakati mmoja. Kwa mfano kuna ‘pe.a’ (kitenzi) na ‘pea’ (nomino) katika KKS3 (TUKI, 2013: 454). KK21 pia inadhihirisha kategoria hizi mbili kama vile pea (kitenzi) na pea (nomino) (Mdee na wenzie, 2011: 415). Hata hivyo, KK21haioneshi mpaka wa mzizi wa kitenzi katika vidahizo vitenzi vyake kama tunavyoona katika KKS3. Kutokana na utata kimaana unaodhihirika kwa sababu ya matumizi ya homonimu, wanaleksikografia hutumia ujuzi mwingi katika utungaji wa kamusi hasa kwa kuziorodhesha homonimu zote katika kamusi na kuziwekea namba za kipeo. Kama vile, chungu 1, chungu2… (TUKI, 2013:73-74). Matumizi ya namba za kipeo hudhihirika pia katika KK21 kama vile, chungu 1, chungu2… (Mdee na wenzie, 2011:70-71). Mifano mahususi ya homonimu katika kamusi hizi mbili za KKS3 na KK21 inaangaziwa katika jedwali 3:
Jedwali 3: Mifano ya homonimu katika KKS3 na KK21
KKS3
chungu, fulusi, fuma, gololi, goma, guni, harija, hela, jaa, jabali, kaa,kaidi, kaifa, kaimu, kamba, kinga, kipeo, kunda, mbuzi, mwari, nyanje, nyanya, paa, pea, panda, rajua, ripoti, somo, shuka, teka, tema, tembe, tusi, uga, ujaji, vua, walia, winda, yakini, zana, zinga.
KK21
chungu, fuma, goma, guni, harija, hema, jaa, kaa, kama, kamba, katika, kigae, kinga, kipepeo, kuba, kuna, mbuzi, meza, mwanamgambo, mwari, nyanya, nyoka, paa, pea, paka, panda, rai, shuka, sijida, sita, somo, tai, tema, tembo, uhuni, varanga, vua, wamba, yamini, ziada, ziara.
Kamusi za KKS3 na KK21 zinalingana katika udhihirishaji wa vidahizo homonimu kwa kuviorodhesha na kuviwekea namba ya kipeo. Hata hivyo, idadi ya maana zinazotolewa kuhusu homonimu moja husika huelekea kutofautiana kutoka kamusi moja hadi nyingine. Kwa mfano, kidahizo pea kimetolewa maana nne katika KKS3 huku KK21 ikitoa maana tatu kama inavyodhihirishwa katika jedwali 4 lifuatalo:
Jedwali 4: Udhihirishaji wa vidahizo homonimu katika kamusi
KKS3
uk.454
pe.a1/pɛja/kt [sie] fikia hali ya ukubwa au ya kuiva. ~lea, ~leka, ~lesha.
pe.a2/pɛja/kt [ele] fagia. ~esha, ~lea, ~leana, ~leka, ~lewa.
pea3/pɛja/nm(-) [i-/-zi-]jozi.
pea4/pɛja/nm(-) [i-/zi-]parachichi.
KK21
uk.415
pea1kt<sie> kuwa na umri mkubwa; komaa, pevuka
pea2kt<ele> ondoa uchafu au kitu kisichotakiwa; fagia, pogoa
pea3nm [i-/zi-] vitu viwili vinavyofanya seti moja; jozi /Kng/
Kutokana na jedwali hili la 4, KKS3 inaangazia maana nne tofauti za kidahizo pea hata hivyo KK21 huangazia maana tatu. Tofauti ni kuwa, KKS3 imeongeza maana nyingine ya kiutohozi kuhusu tunda linaloitwa pea.
Istilahi polisemia ilibuniwa na Breal katika miaka ya 1897 (Bussmann, 1996). Polisemia ni uhusiano ambapo kidahizo kimoja kinadhihirisha maana zaidi ya moja ambazo zinahusiana na zenye asili moja (Crystal, 1987; Hatch na Brown, 1995; Fromkin na wenzie, 2007). Polisemia hurejelewa pia kama uhusiano wa kuongezea kidahizo fulani maana zaidi ili kuashiria jina jipya au kiashiria kigeni (Prinsloo na wenzie, 2000). Kidahizo kinachohusiana kipolisemia hurejelewa kiisimu kama polisemi yaani ‘neno lenye maana mbili au zaidi zinazokaribiana sana…’ (TUKI, 2013: 465).
Mara nyingi polisemi huingizwa katika kamusi mara moja kama kidahizo kimoja kisha tarakimu ya kawaida hutumiwa katika utoaji wa maelezo ya maana zake zinazohusiana (Yule, 1996). Ni wajibu wa mwanaleksikografia kutambua vidahizo polisemi kwa kuangalia uhusiano kimaana unaotokana na etimolojia kwa sababu si vidahizo vyote vinavyofasiliwa kwa kutumia tarakimu hizi ni polisemi. Tarakimu za 1, 2, 3 za kawaida zimetumika katika kamusi hizi zote mbili kwa namna inayofanana. Tazama matumizi katika jedwali 5:
Jedwali 5: Matumizi ya tarakimu katika midhihiriko ya vidahizo polisemi
KKS3
uk.546
tawi/tawi/ nm (ma-)[li-/ya-]1 sehemu ya mti inayoota kutoka shinani, agh. hutoa majani na matunda; tamviri, tagaa. 2 sehemu ya ofisi ndogo ya chama, shirika, n.k.: ~la Chama cha Ushirika.(>Kar)
KK21
uk.492
tawi nm ma- [li-/ya-] 1 sehemu ya mti inayoota majani, maua na matunda; tagaa, tanzu 2 ofisi ambayo ni sehemu ya ofisi kubwa ya chama, shirika au kampuni.
Ingawa ni vigumu kuweka mpaka maalum kimaana baina ya homonimu na polisemi, tofauti mbalimbali baina yake zimewahi kuabainishwa (Lyons, 1981; Bussmann, 1996; Mojela, 2006):
Kwanza, polisemi huandikwa mara moja kama kidahizo na maana zake zinazohusiana huwekwa katika fungu moja kwa kutumia nambari za kawaida za [1, 2, 3…] ilhali homonimu hurudiwa kuandikwa kwa kuorodheshwa moja baada ya nyingine huku nambari za kipeo kama vile [1, 2, 3…] zikitumiwa na mzizi wa kila kidahizo huandikwa ukijisimamia. Pili, polisemi ina mzizi mmoja na homonimu ina mizizi tofauti. Mifano ya polisemi yenye mzizi mmoja ni kama vile nyayo (nm) [alama za miguu na falsafa] na kifaru (nm) [mnyama na chombo cha kivita]. Polisemi hizi za nyayo na kifaru zinaashiria kategoria moja ya leksimu nomino.
Nyayo huweza kurejelewa kivyake kama kidahizo kamusini. Aidha, inabainika kuwa neno wayo halifai kuzingatiwa kama umoja wa nyayo. Hii ni kwa sababu, neno nyayo lipo katika ngeli ya {I-} na pia ngeli ya {ZI-} (TUKI, 2013:434). Aidha, katika kamusi hizi zote, wayo ni wingi wa uwayo na hupatikana katika ngeli ya {U-ZI} na pia katika ngeli ya {A-WA} hasa tunaporejelea aina ya samaki (TUKI, 2013: 633 na Mdee na wenzie, 2011: 570). Maneno yote mawili yanaangaziwa kamusini kama vidahizo mbalimbali.
Homonimu ina mifano kama vile ka.a (kitenzi), kaa (nomino), pe.a (kitenzi) na pea (nomino). Hivyo basi, homonimu hujitokeza katika kategoria anuwai kama vile nomino na hata kitenzi. Tatu, polisemi hutokea kimatumizi katika miktadha inayohusiana huku homonimu ikielekea kutokea kisadfa, kifonetiki na kisemantiki. Nne, homonimu huunda umbo moja linalogawika katika maneno mengine hata hivyo husalia na othografia na fonolojia asilia ilhali polisemi haijigawi katika maneno mengine. Tano, polisemi inahusiana kimaana na kietimolojia, na homonimu huelekea kutohusiana kimaana na pia kietimolojia.
2.1.2 Taarifa za Kisarufi
Istilahi sarufi hujumuisha uchunguzi wa masuala ya fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki (Makoti, 2007). Hivyo basi, suala la sarufi linahusisha umbo sauti (fonolojia), maumbo (mofolojia), miundo (sintaksia) na maana (semantiki) (Kihore, Massamba na Msanjila, 2009). Kimsingi, vipengele vya taarifa za kisarufi katika kamusi kwa jumla vinahusisha masuala kama vile mofolojia, matamshi, kategoria na matumizi ya kidahizo kimuktadha, ngeli za nomino na hata uelekezi wa vitenzi (Chomi, 1995).
a) Tahajia na Matamshi
Kiswahili huainishika kimuundo kama lugha ambishi bainishi kwa sababu maneno yake huweza kuwekewa viambishi maalum ama awali au tamati (Mgullu, 1999). Muundo huu hutusaidia katika udhihirishaji wa tahajia za maneno yake. Tahajia ni ‘uwakilishaji wa sauti kwa herufi katika maandishi kufuatana na muendelezo wa maneno uliokubaliwa’ (TUKI, 2004: 390). Kamusi zote za KKS3 na KK21 zimetumia herufi za Kilatini katika kuandika vidahizo kutoka mwanzo hadi mwisho. Mfumo wa kuandika sauti za lugha kimaandishi ndio hurejelewa kitaaluma kama othografia. Katika othografia ya Kiswahili kuna sauti zinazowakilishwa na herufi moja hata hivyo kuna nyingine zinazowakilishwa na herufi zaidi ya moja kama vile [ch, sh, th, dh, ny, ng’ na gh] (Kihore na wenzie, 2009).
Kiulinganifu, KK21 haijashughulikia matamshi ya vidahizo kama tunavyoona katika KKS3. KK21 haijazingatia suala la matamshi labda kwa sababu ya madai kuwa maneno ya Kiswahili hutamkwa jinsi yanavyoandikwa (Chomi, 1995). Kwa upande mwingine, matamshi ya kila kidahizo yameonyeshwa katika KKS3 kama vile kidahizo kandia kinatamkwa kama /kandija/ na hudhihirishwa katika kitomeo kama ifuatayo:
kandi.a/kandija/ kt [ele] tilia guu; kalia vibaya; chongea. (TUKI, 2013: 191)
b) Kategoria za Vidahizo
Kimsingi vidahizo vya kamusi aghalabu huainishwa katika kategoria nane muhimu kama vile nomino, kitenzi, kivumishi, kielezi, kiunganishi, kihusishi, kihisishi au kiingizi na kiwakilishi (TUKI, 2004; Mdee na wenzie, 2011). Katika kamusi hizi zote za KKS3 na KK21, kategoria zote nane za vidahizo zimeoneshwa baada ya kuandika tahajia za vidahizo, matamshi yake na vifupisho vyake vinavyooneshwa kwa kutumia chapa ya italiki. Hata hivyo, inabainika kuwa KKS3 huonesha namna kila kidahizo kinavyotamkwa tofauti na KK21 inayoangazia tu vidahizo bila kuonesha matamshi yake. Vifupisho vya kategoria hizi vinalandana katika kamusi zote kama vile: nomino (nm), kitenzi (kt), kivumishi (kv), kielezi (kl), kiunganishi (ku), kihusishi (kh), kihisishi (ki) na kiwakilishi (kw). Tazama mifano ya kategoria ya kidahizo kielezi (kl) kifuatacho:
abadi kl neno linaloonyesha kutokoma kwa muda; daima, milele: Anaishi hapa abadi. /Kar/ (Mdee na wenzie, 2011: 1).
abadi /abadi/ kl daima, milele. (>Kar) (TUKI, 2013: 1)
c) Umoja na Wingi wa Vidahizo
Kimsingi vidahizo vya kategoria ya nomino huandikwa katika umoja na wingi. Vidahizo nomino vina viambishi awali vya kuashiria umoja na wingi. Hata hivyo, kuna vidahizo vingine ambavyo havibadilishi maumbo moja kwa moja hasa nomino za kawaida katika ngeli kama vile [i-/zi-] ama katika umoja au wingi. Kamusi hizi zote zimeonyesha umoja na wingi wa kidahizo baada ya kutaja kategoria yake kuu. Katika KKS3 kuna viambishi vya kuonyesha wingi wa vidahizo katika parandesi mduara ( ). Hata hivyo katika KK21 hakuna matumizi ya alama yoyote katika udhihirishaji wa wingi wa kidahizo vyote. Tazama mfano wa kidahizo afa katika jedwali lifuatalo:
Jedwali 6: Midhihiriko ya umoja na wingi wa vidahizo
KKS3
uk. 4
afa /afa/nm (ma-) [a-/wa-] mtu anayewatendea wengine mabaya.(>Kar)
KK21
uk. 3
afa nm ma- [a-/wa-] mtu anayefanya matendo mabaya kwa wengine.
Kinachodhihirika hapa ni kuwa neno afa katika ngeli ya {A-WA} lenye wingi maafa hurejelea mtu au watu wanaowatendea wenzao mabaya. Matumizi yake ni tofauti na kidahizo maafa ambacho hupatikana katika ngeli ya {YA-} na kinachomaanisha ‘tukio la kudhuru linaloleta hasara; kisirani’ (TUKI, 2013:292). Ngeli hii ya {YA-} hujumuisha pia vidahizo kama vile madhila na maasi. Hata hivyo, kuna neno asi ambalo ni kitenzi wala si nomino katika kamusi. Hivyo basi, asi hutumiwa tunaporejelea kitenzi na maasi tunaporejelea nomino. Isichukuliwe kuwa neno asi huweza kutumiwa kama umoja wa maasi na afa kama umoja wa maafa hali inayopotosha ukweli uliopo.
d) Ngeli (Kategoria ndogo za Nomino)
Istilahi ngeli hutumiwa kumaanisha ‘kundi la nomino katika baadhi ya lugha lenye sifa zinazofanana kisarufi’ (TUKI, 2004: 307). Ngeli za nomino za Kiswahili huangaziwa kimofolojia kwa kutazama viambishi vya mianzo ya nomino, kisemantiki kwa kuzingatia maana za nomino na kisintaksia kwa kuzingatia uhusiano wa nominohusika yaani kiupatanisho wa kisarufi (Mgullu, 1999). Kimofolojia nomino za Kiswahili huwa na ngeli kama vile: {MU-WA, M-MI, JI-MA, KI-VI, U-N, U-MA, U-Ø kama vile ukuta/kuta, Ø-MA kama vile dede/madebe, Ø-Ø kama vile taa/taa]. Kisintaksia kuna ngeli kama vile: (YU-A-WA, U-I, LI-YA, KI-VI, I-ZI, U, U-YA, U-ZI, YA, I, KU, PA-MU-KU). Kisemantiki, nomino huzingatiwa kimaana kama vile ngeli za 1&2 hurejelea viumbe hai (Habwe na Karanja, 2004). Ngeli zimeonyeshwa kisintaksia katika kamusi zote za KK21 na KKS3 ambapo ngeli huangaziwa baada ya kutaja wingi wa nomino na huonyeshwa katika parandesi ya mraba [ ]. Tazama jedwali 7 lifuatalo:
Jedwali 7: Midhihiriko ya ngeli za vidahizo
KKS3
uk.5
agizo /agizɔ/ nm (ma-) [li-/ya-] 1amri: ~ la Rais. 2 maelekezo
KK21
uk. 4
agizo nm ma- [li-/ya-] amri anayopewa mtu ili atekeleze jambo fulani.
e) Uelekezi wa Vitenzi
Kwa mujibu wa KK21, kitenzi ni ‘neno linalotoa taarifa kuhusu jambo linalofanyika, lililofanyika au litakalofanyika’ (Longhorn, 2011: 229). Wataalamu mbalimbali hueleza kuwa vitenzi vya Kiswahili huweza kuainishwa katika kitenzi halisi (kikuu na kisaidizi) na vilevile kitenzi kishirikishi (vikamilifu na vipungufu) (Habwe & Karanja, 2004). Hata hivyo, Kihore na wenzie (2009) wanaeleza kuwa kuna vitenzi vikuu, visaidizi na vishirikishi.
Licha ya kwamba kuna aina mbalimbali za vitenzi katika lugha, katika utungaji wa kamusi vitenzi huangaziwa kiuelekezi. Hii inamaanisha kuwa kitenzi huainishwa kwa kutazama iwapo kinaweza kufuatwa na nomino moja kwa moja au la katika sentensi husika. Iwapo kitenzi huweza kufuatwa kimatumizi na nomino katika sentensi basi ni kitenzi elekezi na iwapo hakifuatwi au hakihitaji kufuatwa moja kwa moja na nomino basi hurejelewa kama kitenzi sielekezi (TUKI, 2004; Longhorn, 2011). Aghalabu nomino hizi zinazofuata vitenzi hurejelewa kiuamilifu kama yambwa.
Katika kamusi hizi mbili, uelekezi wa vitenzi umeonyeshwa kwa kutumia alama [ ] katika KKS3 au <> katika KK21 baada ya kutaja kategoria ya kitenzi husika. Kitenzi elekezi hufupishwa kama [ele] au <ele> na kitenzi sielekezi hufupishwa kama [sie] au <sie> kwa mujibu wa kamusi husika. Tazama mifano katika jedwali 8 lifuatalo:
Jedwali 8: Mifano ya uelekezi wa vidahizo vitenzi
KKS3
uk. 283
lainish.a/lajiniʃa/ kt[ele] fanya iwe laini au –ororo. ~ana, ~ia, ~iana, ~ika, ~iwa, ~wa.
landan.akt [sie] kuwa na sura zinazofanana; fanana, shabihiana, lingana: Baba ana~ na mwanawe. ~ia, ~ika, ~isha.
KK21
uk. 262-263
lainishakt<ele> sababisha kitu kiwe laini au –ororo. lainisha, lainishia, lainishika, lainishwa. /Kar/
landanakt<sie> fanana; shabihiana. Adijah analandana na baba yake.
Aidha mizizi ya vidahizo vitenzi vyote imeonyeshwa katika KKS3 na haionyeshwi katika KK21. Kuna mizizi ya vitenzi vinavyoonyeshwa kwa kutumia alama ya nukta katika KKS3 kama vile ach.a. Hata hivyo, hakuna mizizi ya vidahizo vitenzi katika KK21 kama tunavyoona katika mifano ifuatayo:
ach.a /aʧa/ kt... (TUKI, 2013:2)
acha kt<ele>... (Longhorn, 2011:2)
f) Minyambuliko ya Vidahizo
Mnyambuliko ‘ni tendo lifanyikalo la kuzalisha neno au maneno mapya kwa msingi wa neno jingine’ (TUKI, 2004: 263). Aghalabu mnyambuliko huonekana katika vitenzi vya lugha ya Kiswahili na huwa katika hali au kauli ya kutenda, kutendea, kutendewa, kutendeka, kutendesha, kutendana, kutendama, kutendata na hata kutendua (Habwe na Karanja, 2004). Vitenzi elekezi huweza kunyambuka katika kauli zote kama vile tendana, tendea, tendeana, tendeka, tendesha na tendewa lakini vitenzi sielekezi huweza kunyambuka hadi hali tatu tu za (~ea/~ia), (~eka/~ika au ~leka/~lika au ~ka), na pia (~esha/~isha au ~lesha/~lisha/~sha)] (TUKI, 2004). Kauli hizi huweza kuwakilishwa kwa kutumia viambishi mbalimbali kama vile: [-w-, -ik-/-ek-, -ish-/-esh-/-iz-/-ez-, -il-/-li-/-el-/-le-/-ili-/-ele-/-i/-e-, -o-/-u-, -am-, -at-, -an-] (Kihore na wenzie, 2009).
Kuna mitazamo ya shule anuwai za uainishaji wa minyambuliko ya vidahizo vitenzi kama vile shule ya kwanza ya mawazo na shule ya pili ya mawazo (Kiango, 2008). Shule ya kwanza huangazia kanuni tano za uzalishaji vinyambuo vitenzi kama vile:
Jedwali 9: Mnyambuliko kwa mujibu wa mawazo ya shule ya kwanza
Hali za mnyambuliko
Mifano
[-i-/-e-], [-li-/-le-]
pita-pitia, peta-petea, zaa-zalia, kwea-kwelea
[-na]
piga-pigana
[-ik-/-ek-], [-lik-/-lek-]
pita-pitika, samehe-sameheka, twaa-twalika, tembea-tembeleka
[-ish-/-esh-]
[-lish-/- lesh-], [-z-]
imba-imbisha, weza-wezesha
tambua-tambulisha, ongea-ongelesha, potea-poteza
[-w-], [-iw-/-ew-], [-liw-/-lew-]
piga-pigwa, fa-fiwa, pa-pewa,
twaa-twaliwa, pokea-pokelewa
Mtazamo mwingine ni wa shule ya pili ya mawazo kama vile:
Jedwali 10: Mnyambuliko kwa mujibu wa mawazo ya shule ya pili
[-i-/-e-]
[–li-/-le-]
piga- pigia, meza-mezea
kimbia- kimbilia, pokea-pokelea, sahau-sahaulia
[-na] kutendana
piga-pigana, pigia-pigiana
[-k-] hali au uwezo
umia-umika, somea-someka
[-sh-]/
[-z-] /
[-y-] utendeshi
ondoa-ondosha, piga-pigisha, pita-pisha au paa-paza
lia-liza au kojoa-kojoza
pona-ponya, ogopa-ogofya, juwa-juvya, lewa-levya Matumizi ya -y- huonekana katika vitenzi vyenye mizizi inavyoishia na konsonanti n, p na w zinazobadilika kuwa kama vile n kuwa y, p kuwa f, na w kuwa v.
[-w-]
piga-pigwa, tia-tiwa, safisha-safishwa na pigia-pigiwa.
Kwa kuwa nia ya makala haya ni kuhakiki namna minyambuliko inavyoonekana katika kamusi hizi mbili, ningependa moja kwa moja nirejelee midhihiriko yake katika kamusi hizi bila kuangazia shule gani muhimu. Katika kamusi hizi zote mnyambuliko wa vitenzi huwekwa kama taarifa za mwisho za kila kidahizo. KKS3 inaoneshaa tu viambishi vya kurejelea hali ya mnyambuliko wa vitenzi inayoleta utata kimatumizi miongoni mwa wasomaji wa lugha ya Kiswahili ilihali KK21 inaonyesha mnyambuliko kikamilifu wa kila kidahizo kitenzi ambapo mabadiliko kimaumbo huonyeshwa. Tazama tofauti katika kidahizo lainisha katika jedwali 11lifuatalo:
Jedwali 11: Midhihiriko ya mnyambuliko wa vidahizo vitenzi
KKS3
uk. 282
lainish.a/lajiniʃa/ kt[ele] fanya iwe laini au –ororo. ~ana, ~ia, ~iana, ~ika, ~iwa, ~wa.
KK21
uk. 262
lainishakt<ele> sababisha kitu kiwe laini au –ororo. lainisha, lainishia, lainishika, lainishwa. /Kar/
Lainisha limefafanuliwa katika KKS3 katika hali sita za (~ana, ~ia, ~iana, ~ika, ~iwa, ~wa) ilhali KK21 ina hali nne za (-a, -ia, -ika, -wa). Aidha, tunaweza kujiuliza kwa nini vidahizo vingine katika KKS3 hunyambuka hivyo na hakuna mnyambuliko katika KK21kama tunavyoona kitenzi landana katika jedwali 12 lifuatalo:
Jedwali 12: Kutolandana katika utokeaji wa minyambuliko ya vidahizo vingine
KKS3
uk.283
landan.a /landana/ kt[sie] kuwa na sura zinazofanana; fanana, shabihiana, lingana: Baba ana~ na mwanawe. ~ia, ~ika, ~isha.
KK21
uk.263
landana kt<sie> fanana; shabihiana. Adijah analandana na baba yake.
Kwa mujibu wa KKS3, kidahizo landan.a kinanyambuka katika hali tatu za (~ia, ~ika, ~isha) ilhali KK21 haitoi viambishi vya kuonyesha mnyambuliko badala yake mfano wa matumizi yake huonyeshwa.
g) Uingizaji wa Vinyambuo katika Kamusi
Makala haya yamerejelea vinyambuo kama vinavyoelezwa katika KK21 (Mdee na wenzie, 2011) kama maneno au vidahizo vilivyoundwa kutokana na myambuliko wake katika hali mbalimbali na hatimaye kuingizwa katika kamusi kama kidahizo kamili chenye taarifa zake mbalimbali. KK21inaangazia hali tatu ya vinyambuo: i) vinyambuo vitenzi ambavyo havikuzalishwa kutokana na vitenzi pamoja na vinyambuo nomino, vinyambuo vielezi na vinyambuo vivumishi. ii) Vinyambuo vitenzi vilivyoundwa kutokana na mizizi ya vitenzi kama vile soma huwa somea, someana, someka, someka, somesha na somwa na maana zake huweza kutabirika. iii) Vinyambuo vitenzi ambavyo maana yake haiwezi kutabirika kwa kujua maana ya kitenzi cha msingi.
Kamusi hizi zote zinadhihirisha kuwa vidahizo vinyambuo vyote huingizwa katika kamusi kama kidahizo kamili na kutolewa taarifa zifaazo; hata hivyo kamusi zote zinatumia alama tofauti za kuonyesha mnyambuliko. Kama vile kidahizo kitenzi twaa limenyambuliwa na kinyambuo chake twali.a (TUKI, 2013) au twalia (Mdee na wenzie, 2011) huingizwa katika kamusi hizi kama kidahizo kamili kama tunavyoona katika jedwali 13:
Jedwali 13: Uingizaji wa vidahizo vinyambuo katika KKS3 na KK21
KKS3
uk. 570-571
twa.a /twa:/ kt [ele] ondoa kitu mahali kilipo au kilipowekwa na kukishika mkononi; chukua. ~lia, ~liana, ~lika, ~lisha, ~liwa.
twali.a kt [ele] chukulia mtu kitu. ~lia, ~liana, ~lika, ~lisha, ~liwa.
KK21
uk. 509
twaa kt<ele> chukua kitu na kukitia mkononi; shika, ondoa. twalia, twaliana, twalika, twaliwa.
twalia kt<ele> bebea mtu kitu.twaliana, twalika, twalisha, twaliwa.
h) Maana na Matumizi ya Vidahizo Kimuktadha
Maana za vidahizo katika kamusi hizi mbili za KKS3 na KK21 zinaelekea kuchukua na kuafikiana na kanuni na mbinu za utoaji fasili za vidahizo. Bwenge (1995) anazitaja kanuni hizo za utoaji fasili za vidahizo kama ifuatavyo: fasili iepuke mzunguko na badala yake itoe maana moja kwa moja, kila neno linalotumika katika fasili fulani halina budi pia kufasiliwa katika kamusi hiyo hiyo; fasili ifafanue maana halisi ya kidahizo na wala si kitu kingine tofauti; na fasili iakisi kategoria ya kidahizo. Fasili iwe rahisi kueleweka, iwe fupi lakini wakati huo huo iwe fasaha, iepuke utata katika maelezo yake na fasili za leksimu zilizomo kwenye kikoa kimoja cha maana ni muhimu ziwe sare au ziwe na muundo sawa. Hii inamaanisha kuwa maneno kama vile homonimu hufaa kuwa na muundo sawa.
Kwa upande mwingine kuna mbinu za fasili kama vile: fasili fafanuzi, fasili elekezi, fasili hiponimu, fasili antonimu, fasili chambuzi, fasili ainishi, fasili unde, fasili kanuni na fasihi sinonimu. Kwa mfano, kidahizo laini huelezwa kwa kutumia fasili antonimu ambapo maana hutolewa kwa kuangazia uelekeo kinyume. Tazama jedwali 14 lifuatalo:
Jedwali 14: Matumizi ya mbinu ya fasili antonimu
KKS3
uk.282
laini /laini/ kv1 -siyokwaruza, -siyo ngumu; teketeke, -ororo, dabwadabwa.
KK21
uk.262
lainikv1 -siyo ngumu; dabwadabwa 2 -siyokwaruza; -ororo 3 (muziki) usiokuwa na kelele wala mikwaruza; taratibu /Kar/
Aidha, matumizi ya vidahizo kimuktadha yameoneshwa kwa kutumia vifupisho vya nyanja husika kama vile kishairi (ksh/ush), kibaharia (bh/bah), kidini (kd/din), kinahau (nh/nah), kimisemo (ms/mse), kimethali (mt/met) na kadhalika. Tazama mfano katika jedwali 15 lifuatalo linaloonyesha muktadha wa kishairi (ksh/ush) wa kidahizo abu:
Jedwali 15: Mfano wa matumizi ya vidahizo kimuktadha
KKS3uk. 1
abu/abu/ nm(-) [a-/wa-](ksh) baba (>Kar).
KK21uk.1
abunm [a-/wa-] (ush) mzazi wa kiume; baba /Kar/
i) Etimolojia ya Vidahizo
Katika kamusi ya lugha ya Kiswahili, kuna maneno ambayo yamechukuliwa moja kwa moja kutoka lahaja zake, lugha nyingine za Kibantu au yale yaliyotoholewa kutokana na lugha za kigeni kama vile Kiajemi (Kaj), Kiarabu (Kar), Kiebrania (Kbr), Kichina (Kch), Kifaransa (Kfa), Kihindi (Khi), Kihispania (Khs), Kijerumani (Kje), Kilatini (Kla), Kiingereza (Kng), Kireno (Kre) na hata Kituruki (Ktu). Kamusi zote za KKS3 na KK21 zimetoa mifano kadha kutoka lugha mbalimbali kwa kutumia vifupisho vya kila lugha husika. KKS3 imezingatia vifupisho vya etimolojia ya vidahizo kwa kutumia alama ya (>)kama vile (>Kar) huku KK21 ikitumia alama ya (/ /) kama tunavyoona kama vile (/Kar/).
2.1.3 Vipengele Vingine vya Lugha Kienzo ya Msimbo
Mitindo yote inayojitokeza katika utungaji wa kamusi kwa ujumla hurejelewa kama lugha kienzo na hutumiwa na wanaleksikografia ili kuweza kutoa fasili au maelezo yanayofaa ya vidahizo katika kamusi husika (Bwenge, 1995). Kuna lugha kienzo ya mjazo na lugha kienzo ya msimbo ya kuonyesha siri ya utoaji fasili ya kidahizo kwa kuangazia kanuni na mbinu za fasili. Hata hivyo, kuna vilevile matumizi mengine ya vipengele vya lugha kienzo ya msimbo yanayotokana na matumizi ya vifupisho, tarakimu, herufi, alama, picha, michoro na kadhalika kama tunavyoona katika utungaji wa kamusi hizi mbili za KKS3 na KK21. Tazama mifano katika jedwali 16:
Jedwali 16: Mifano ya vipengele vingine vya lugha kienzo ya msimbo
Vifupisho
KKS3
KK21
agh., ele, fiz, kb, kd, kem, kh, ki, kl, k.m., kt, ku, k.v., ksh, kv, kw, kz, ms, mt, nh, n.k., nm, sie, taz, uk.
Kaj, Kar, Kbr, Kch, Kfa, Khi, Khs, Kje, Kla, Kng, Kre, Ktu, Kmw, Kgo, nm, kt, kv, kl, ku, ki, kh, kw, agh., k.m., n.k., k.v., taz. <ele>, <sie>, (mse), (nah), (met), (bah), (zam), (ush), (sir), (sih)
Tarakimu
KKS3
KK21
1, 2, 3, ... kutenga maana za maneno na tarakimu 1 2 3 4za kipeo za kuonyesha vidahizo homonimu
1, 2, 3, ... kutenga maana za maneno na tarakimu 1 2 3 4za kipeo za kuonyesha vidahizo homonimu
Herufi
KKS3
KK21
(a), (b), ...katika mabano mduara kutenga maana tofauti za misemo au nahau
(Haipo katika kamusi hii)
Alama
KKS3
KK21
, ; . : ! ( ) [ ] / / ~ / n.k
, ; . : [ ] <> ( ) / /
Picha na michoro
KKS3
KK21
Kuna michoro 175 na majedwali 5
Kuna michoro na picha nyingi
3.0 HITIMISHO
Kamusi hizi mbili zinalingana katika kuonesha idadi ya vidahizo jumla na vidahizo vipya licha ya kuwa na idadi tofauti, mpangilio wa vidahizo kialfabeti kutoka A-Z na kuandikwa kwa kutumia rangi iliyokoza japo tofauti. Vidahizo sinonimu huonyeshwa kwa kutumia koma, homonimu kwa namba za kipeo (1 2 3) huku polisemi zikionyeshwa kwa tarakimu za kawaida (1, 2, 3.); tahajia za kila kidahizo zimeonyeshwa huku kamusi ya KK21 ikikosa kushughulikia suala la matamshi. Kategoria za vidahizo vyote na wingi wa vidahizo nomino zimeonyeshwa katika kamusi zote huku uelekezi wa vitenzi ama elekezi au sielekezi pia umeangaziwa. Vinyambuo vyote vimezingatiwa kama vidahizo kamili katika kamusi zote huku kanuni na mbinu za utoaji fasili za vidahizo zikizingatiwa vyema. Kamusi zote zimeonyesha matumizi ya vifupisho, tarakimu, alama mbalimbali, picha na michoro ili kurahisisha utoaji wa fasili za vidahizo.
Ingawa kamusi hizi zinalingana katika masuala anuwai, tofauti huonekana katika taarifa kuhusu mnyambuliko kwamba KKS3 huonesha tu viambishi vya kutumiwa katika mnyambuliko wa vitenzi anuwai, hali inayoelekea kutatiza wasomaji; wakati KK21 inaonesha namna ya kunyambua vidahizo vitenzi katika hali kadha mtindo unaoelekea kurahisisha mafunzo ya vitenzi vya Kiswahili. Kwa jumla, kamusi zote zinaelekea kuzingatia kwa namna moja au nyingine vipengele vya nadharia ya metaleksikografia kama vile uzingativu wa fasili za vidahizo kiothografia na kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki/kimaana, kiensaiklopidia na hata kiuhusiano. Hata hivyo, KK21 haijaonesha namna tunavyotamka vidahizo husika.
MAREJELEO
Bakhressa, S. K. (1992). Kamusi ya Maana na Matumizi. Nairobi: Oxford University Press
BAKITA (1987). Kamusi ya Agronomia na Ufugaji. Dar es Salaam: Educational Services Center Ltd.
Bright, W. (mh.) (1992). International Encyclopedia of Linguistics. Vol.1. New York: OxfordUniversity Press.
Bussmann, H. (1996). Routledge Dictionary of Language and Linguistics. London: Routlege.
Bwenge, C. M. T. (1995). “Lugha Kienzo ya Kamusi katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu,” katika Msingi wa Utungaji wa Kamusi. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: TUKI. uk.61-87.
Chomi, E. W. (1995). “Sarufi katika Kamusi ya Kiswahili,” katika Msingi wa Utungaji wa Kamusi. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: TUKI. uk.88-105.
Crystal, D. (1987). The Cambridge Encyclopedia of Language. Cambridge: CambridgeUniversity Press.
Frawley, W. J. (mh.) (2003). International Encyclopedia of Linguistics. (2nd ed.). Vol.1. Oxford: OxfordUniversity Press.
Fromkin, V., Rodman, R. na Hyams, N. (wh.) (2007). An Introduction to Language.(8th ed.). United States: Thomson Wordsworth.
Gibbe, A. G. (1977). Homonymy, Synonymy and Antonymy in Kiswahili: A Lexical Study. Tasnifu ya Uzamili, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.
Habwe, J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Hatch, E. na Brown, C. (1995). Vocabulary, Semantics and Language Education. Cambridge: CambridgeUniversity Press.
Kiango, J. G. (2008). “Sarufi ya vinyambuo vitenzi vya Kiswahili: mitazamo mbalimbali kuhusu kanuni za unyambuaji,” katika Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika. Chuo Kikuu cha Moi: Moi University Press. uk. 45 - 58.
Kihore, Y. M., Massamba, D. P. B. na Msanjila, Y. P. (2009). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA) Sekondari na Vyuo. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Lyons, J. (1981). Language and Linguistics. An Introduction. Cambridge: CambridgeUniversity Press.
Makoti, V. S. (2007). “Matumizi ya Kiswahili nchini Kenya katika Redio na Runinga,” katika Kiswahili na Elimu Nchini Kenya. Nairobi: Twaweza Communications & CHAKITA.uk.20-27.
Mbaabu, I. (1996). Language Policy in East Africa. Nairobi: Educational Research & Publications.
Mdee, J. S., Njogu, K. na Shafi, A. (2011). Kamusi ya Karne ya 21. Nairobi: Longhorn.
Mgullu, R. S. (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili.Nairobi: Longhorn Publishers.
Mojela, M. V. (2006). ‘Polysemy or Homonymy? A Case Study of the Challenges Pertaining to the Lemmatisation of Polysemous and Homonymous Lexical Items in the Compilation of a Sesetho sa Leboa-English Bilingual Dictionary,’ katika 11th International Conference of the African Association for Lexicography 3-7, July. Republic of South Africa: University of Venda for Science and Technology, Thohoyandou, uk 35-36. http://afrilex.africanlanguages.com/afrilex2006.pdf
Polome, E. C. (1967). Swahili Language Handbook. Washington: Centre for Applied Linguistics.
Prinsloo, D., Chuwa, A. R., & Taljard, E. (2000). ‘The lexicons of Africa,’ katika African Voices: An Introduction to the Languages and Linguistics of Africa. Southern Africa: Oxford University Press. uk.220-244.
TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la tatu. Nairobi: Oxford University Press.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la pili. Nairobi: Oxford University Press.
TUKI (1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la kwanza.Nairobi: Oxford University Press.
TUKI (2001). Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza. Dar es Salaam: TUKI.
Wiegand, H. E. (1983). On the Structure and Contents of a General Theory of Lexicography. Kutoka http://www.euralex.org/elx_proceedings/Euralex 1983/2007_Herbert (Kupakuliwa 27-2-2017).
Yule, G. (1996). The Study of Language. (2nd ed.).Cambridge: CambridgeUniversity Press.