Friday

TABARUKU: BURIANI KWA MWALIMU SAMUEL MUSHI MFASIRI WA MFALME EDIPODE

0 comments

Profesa Stephen Mushi
Tarehe 23/7/2011 Mwalimu Samuel Mushi alipiga dunia teke na akaenda  zake mbinguni.
 Alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali taifa ya  Muhimbili.
Leo ni siku ya Waalimu duniani. Mtandao Huu(Masshele kiswhili) unatambua mchango Na kazi kubwa wanayofanya waalimu. Hivi Leo tuadhimishe siku hii kwakumkumbuka Mwalimu, Stephen Mushi.
Alikuwa na miaka sabini na miwili (alizaliwa 1939). Hata hivyo, jambo la muhimu ni kuwa alifanya mchango wake na sasa waliobaki nao wafanye wao.
Mushi alikuwa
mwana-lugha mkuu na mkongwe  ambaye kuaga kwake bila shaka ni hasara kubwa kwa jumuia na wazalendo wa Kiswahili na hasa fani ya fasihi. 
Wengi labda hawamfahamu mwalimu Mushi kwa jina, hasa  Kenya alipokuwa anafundisha na hata Tanzania, lakini wengi wameshasikia hadithi ya mfalme Edipode ambayo mwalimu huyu aliitafsiri mnamo mwaka wa 1971. Hadithi hiyo, baada ya kutafsiriwa na mwalimu Mushi, ilienea sana na kuwafikia watu wengi ambao hawangepata fursa ya kuisikia kwa vile wangetatizwa kuelewa ile iliyo kwenye hati za lugha za kimombo. Ufanisi huo ulikuwa hakikisho tosha kuwa fasihi haina mipaka na hamu ya wanadamu wote kusimuliwa hadithi nzuri ipo. Pia hadithi yoyote ile yawezafikia kila mtu, bora mbinu za kuieneza na kueleza ziwe mwafaka. Kwa wale wajifunzaji wa fasihi hasa fasihi linganishi (Comparative literature) watakuwa wamewahi kusikia  hadithi ya mfalme Edipode
Hadithi bila shaka ilikuwa ya Sophocles ambaye tunamwita Sofokile, ila mwalimu Mushi aliipa msisimko wa Kiswahili hata kuifanya ionekana ngano ya hapa nyumbani na wala si ya ughaibuni. Lakini, hiyo sio kazi pekee aliyoifanya mwalimu huyu. Hata kabla ya kuswahilisha Sophocles, alikuwa ameshaswahilisha William Shakespeare -mchezo wa Makbeth akiwa na umri wa miaka 29 tu, na Tufani mwaka mmoja baadaye (1969). Hata hivyo tamthilia hizo hazikufana sana Tanzania na hats  Kenya   kwa kufuatia maudhui yao ambao yalilenga sana ushirikina. Kazi hizo alizifanya labda akifuata katika nyayo za mtangulizi wake -Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa ameshaswahilisha Juliasi Kaizari (1963).
Katika ustadi wa utafsiri fasihi huenda Mushi alimpiku mwalimu Nyerere. Sababu ya kunawiri kwa Mushi kushinda Nyerere (kwa mtazamo wangu) ni kwamba Mushi aliegemea sana fasihi ilihali huyo wa awali aliegemea sana siasa. Mushi alitafsiri akiwa na nia na kutumbuiza na kuongozwa na uhondo wa fasihi, yaani aliwasilisha pamoja na kuwakilisha. Mwalimu Nyerere naye alitamani sana kuangazia maswala ya kisiasa yaliyomo kwenye maandiko husika. 
Ni bayana pia Mushi alichagua hadithi zenye rutuba kubwa ya fasihi kushinda wengi waliomtangulia. Ingawa hivyo si kusema kuwa hapawezijitokeza mwandishi mwingine akazisimulia kazi hizo na zinginezo kwa ubora kumshinda. Hata mwenyewe alikiri katika utangulizi wa Tufani kwamba “…napenda kusema kama ikiwa upungufu wa tafsiri yangu utauudhi baadhi ya wasomaji kiasi cha kuamsha cheche za shauku ya kutoa tafsiri nzuri zaidi ya mchezo huo au kuifuatisha hadithi ya mchezo huo kwa ukamilifu zaidi…hakuna atakayefurahi kunishinda.”
Mchango wa Mushi kwa fasihi haukukomea hapo kwa vile ni yeye aliyekuwa na ujasiri mkubwa kutohoa na kubuni majina mengi ambayo hayakuwepo kabla yake, hasa katika msamiati wa fasihi ya kutafsiriwa. Hakuogopa kumwita Zeus- Zeo, Sophocles- Sofokile, Oedipus- Edipode, na Thebes- Thebe. Msamiati huu unasaidia sana wandishi wa badaye kuandika kwa upesi zaidi bila kusumbuliwa ama kusumbuka kubuni majina mapya kuzungumzia mambo au watu wale. Kwa wale ambao wamejaribu kuandika au kuzungumzia fasihi hizo kama Dkt. Richard Wafula  wanafamu na kufaidi mchango huo wa Mushi kwa makini.
Mushi alipanua mipaka ya utungaji  mashairi. Kwa kufasili Edipode akitumia mizani sita badala ya nane ama kumi na sita, amekomboa wandishi wengi ambao walikuwa wamefungiwa katika kanuni ambazo wakati mwingine hazitoshelezi tafsiri kikamilifu. Ingawa  Stephen Mushi alichangia pia katika uandishi wa mambo mengine kama siasa (vitabu thelathini na moja hivi) lakini, ni kwenye nyanja ya fasihi ambapo nyota yake inang’a na haina mpizani wa dhati. Jinsi tu vile riwaya ya Kusadikika ya Shabaan Robert bado inashikilia upeo kama fasihi bora ya kiasili, tamthilia ya Mfalme Edipode ya Samuel Stephen Mushi inashikilia nafasi hiyo ya kuwa fasihi- tafsiri bora kufikia leo.
Aidha profesa mushi atakumbuka kwa mchango wake mkubwa katika siasa kwa kutoa mitazamo yake iliyojaa mawazo huru, Mushi hakusita kutoa mtazamo wake kila alipo tafutwa na kuulizwa juu ya jambo fulani katika siasa. Naweza kukiri kuwa Mwaka 2011 tulimpoteza mtu muhimu sana kwa Tanzania na kule Kenya alipokuwa akifunza, na mbaya zaidi mwaka huo huo ndipo Mwanamama , mwanamke wakwanza kupata shahada ya uzamivu Wangari Maathai mwanasiasa na Mwana mazingira aliaga dunia pia,
Kwa kumalizia Mwalimu Mushi nimemtungia Shairi lifuatalo
Mwalimu twa kukumbuka
Twakuombea kwa rabuka
Kila kona wasikiaka
Kwasababu ulisumbuka
Edipode ikatafsirika
Fasihi linganishi ikalinganika
Na sisi maarifa tukayashika

Edipode yasimulika
Kweli lugha uliipika
Maudhui yakapangika
Wahusika majina ukayasuka
Mengi yote yakasukika
Mtindo ukautika
Ukawa waimbika

Wasomi wakajumuika
Kazi yako kuifunguka
Zawadi na Rughumbika
Wakaapa kwa hakika
Maarifa waliyashika

Kwaheri profesa Mushi mchango wake nimkubwa sana katika Fasihi linganishi.

Mwisho. Mwandishi hajapata kumfahamu Profesa Mushi zaidi ya kumsoma kupitia kazi zake na machapisho mbalimbali.
info.masshele@gmail.com
 MSIKILIZE PROFESA MUSHI AKITOA MTAZAMO WAKE KUHUSU KUJIUZULU KWA ROSTAM
  BOFYA >HAPA<

No comments:

Post a Comment