Thursday

NADHARIA ZA MAANA

0 comments

Waandishi

LUSONGE    KASSIMU   S

BAED/UDSM


02.
KIREI   EWALD T

BAED/UDSM


04.
GANG’OLO BETH  MESHACK
BAED/UDSM


05
PAKATA ELIZABETH
BERNALD
BAED/UDSM

Makala hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni sehemu ya utangulizi, kiini  na sehemu ya mwisho ni hitimisho katika sehemu ya utangulizi maana ya nadharia hufasiliwa kulingana na wataalamu mbalimbali na tukafasili nini maana ya maana kulingana na wataalamu mbalimbali.

Katika sehemu ya pili ambayo ni kiini cha swali tumeeleza nadharia mbalimbali jinsi zikifasili maana. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho .


Dhana ya nadharia imefasiliwa na watalaam mbalimbali kama ifuatavyo,Wamitila(2003:22) hufasili kama nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani: chanzo chake, muundo wake , utendaji kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje.


TUKI (2004:300) wanasema nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani.


Resan (2014:121) akinukuu fasili ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004:300) anafasili nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua  au kutekeleza jambo fulani.


Kiujumla, nadharia ni maelezo yakinifu kuhusu kitu, tajiriba, maarifa na mafanikio au maangamizi yaliyochomoza katika jamii na hivyo nadharia hufungamana na mambo mbalimbali katika jamii kama vile mbinu, maarifa, tasnifu, mikabala na miendeno mbalimbali ya jamii.


Pia maana ya maana kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2007), wanasema neno maana lina fahiwa nyingi watu wa kawaida wanalitumia kwa namna mbalimbali kama vile sababu, dalili, ishara , hafai, ufafanuzi, hali, kejeri na umuhimu.


Kiujumla, maana ni huelezea kitu, jambo au mtu kihali, sababu, dalili, ishara, hafai, ufafanuzi, hali, kejeri na umuhimu.


Nadharia ya maana kama kitajo au kirejeleo, nadharia hii iliasisiwa na Ogden na Richard wakinukuliwa na Resani (2014) wanaeleza  nadharia hii uhusu mahusiano baina ya kiambo cha lugha na vitu au kitu katika ulimwengu wa masilugha. Nadharia hii hudai ya kuwa maana ya kiyambo cha kiisimu ni kitu fulani halisia kinachotajwa na kurejelewa na umbo hilo la kiisimu. Hiyo basi maana ya tamko lolote la kiisimu ni kirejeleo kinachorejelea tamko hilo la kiisimu ambalo husimama badala ya neno hilo la kiisimu.



Kwa mfano,
Neno                                                                    kirejelea
 Mshale………………………………………
Nyota……………………………………………

Cha kuzingatia ni kwamba tamko ambalo maana inarejelewa na kitu halisia lazima liwe la kiisimu yaani liweze kufuata taratibu zote za lugha husika ambapo mtumiaji wa lugha hiyo anaweza kutambua ila likiwa siyo la kiisimu basi hakutakuwa na kirejeleo chenye kutoa maana ya neno hilo.. kwa mfano, neno “anacheza” lina kirejeleo chake katika lugha ya Kiswahili lakini likitamkwa bila kufuata kanuni za kiisimu litashindwa kutoa maana katika kirejeleo husika, kwa mfano “zachenaa” neno halina maana kwa sababu halikufuata utaratibu wa lugha husika.


Ubora wa nadharia hii ni kwamba, moja ni kweli yapo maneno mengi katika lugha ambayo kazi yake ni kutaja vitu mbalimbali. Ni dhahiri ya kuwa lugha zina viambo ambavyo kazi yake ni kurelejea au kutaja kitu au vitu halisia.

Kwa mfano maneno ya nomino mahususi, kama vile kisu, panya, mwanajeshi na shule zote maana zake huelezwa na kirejeleo yaani umbo halisia katika ulimwengu halisi.


Pia nadharia ina umuhimu hasa katika kujifunza lugha husika , kwa mfano mtoto anapojifunza lugha lazima ajifunze kwa kuoneshwa vitu au kutajiwa jina la kitu husika, au kuoneshwa tendo au kutajiwa jina la tendo hilo.


Pia nadharia hii ina mapungufu kama ifuatavyo, moja kuna baadhi ya maneno hayana virejelea vyake katika lugha husika. Kwa mfano maneno kama vile sana, kabisa, tayari, zimwi, ingawa na popobawa. Maneno mengi yanajikita hasa katika fikra ya mtu ( dhana) na ni ya kufikirika( udhahania) na hayana urejeleo.


Pia nadharia hii haifanyi kazi katika maneno yenye uhusiano wa kihomonomia, yaani umbo moja la leksimu lenye  kuwakilisha leksimu zenye maana zaidi ya moja.
Mfano 1.
Paka(i) – ni mnyama mdomo aina ya mamalia
Paka (ii) – ni kitendo cha kutia rangi au mafuta kitu chenye asili ya utambarare
Mfano 2.
Kaka (i) – ganda la yai
Kaka(ii) – ndugu wa kiume
Kaka (iii) – ugonjwa wa vidole
Mfano wa 3
Shinda (i) – shika nafasi ya kwanza
Shinda (ii) baki mahali siku nzima
Shinda (iii) – isiyojaa sawasawa
Kwa mifano hiyo hapo juu inadhihirisha wazi kuwa uwepo wa kiyambo kimoja cha kiisimu kinaweza kuwa na maana zaidi ya moja.


Pia nadharia hii haifanyi kazi katika maneno yenye uhusiano wa kipolisemia, Yule (1985) anasema polisemia ni hali ya neno moja kuwa na maana nyingi zinazouhusiana. Pia Lyon (1977) anasema polisemia ni sifa ya neno moja kuwa na maana nyingi zinazouhusiana. uhusiano uliopo baina ya maneno katika polisemia inatokana na mnyumbuliko wa maana moja ya msingi.
Mfano 1.
Kichwa
Ni sehemu ya juu ya mwili wa mwanadamu au kiumbe hai yenye macho, pua, mdomo na kadhalika.
Injini ya gari moshi inayokokota mabehewa
Kiongozi
Mtu hodari sana
Mfano wa 2.
Abudu
Heshimu
Sali
Nyenyekea
Pia nadharia hii haiwezi kufanya kazi katika maneno yenye uhusiano wa kisinonimia ( visawe),  yaani viambo zaidi ya moja yenye maana iliyosawa au ni maneno yenye maumbo tofauti lakini huwa maana sawa. Na hii inatokana na ukopaji wa misamiati, jinsi au jinsia tofauti wa maneno kijografia, urasmi na kadhalika
Mfano,
fedha, pesa, hela, ankara.
Mapenzi, mahaba, kupendana
Mjinga, bwege, mpumbavu, fala, pimbi.
Pia udhaifu mwingine ni kwamba katika lugha fulani huwa kuna viambo ambavyo hurejelea kitu kilekile kimoja.
Kwa mfano.
Jemedali mkuu wa majeshi.
Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.


Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mume wa Bi. Janeti.
Vyote hivi vinarejelea kitu kimoja, na si kweli kwamba kila kiambo kina kirejelea chake mahususi bali kila vyote vinarejelea kitu kilekile kimoja ambacho ni Rais Magufuli.
Nadharia nyingine ni nadharia ya maana kama dhana au taswira, kwa mujibu wa Resani (2014) nadharia hii iliasisiwa na wanaisimu kama vile Sapir na de Sassure, nadharia hii inafafanuliwa kuwa maneno ya kiyambo ni dhana au taswira inayoibuliwa na kiyambo hicho akilini mwa mwanalugha pindi kiyambo hicho kinapotumika.

Hivyo basi mzungumzaji wa lugha huwa na taswira katika akili yake ikirejelewa kitu halisia katika ulimwengu wa masilugha.Dhana inayojemgeka akilini mwa watu ni ile dhana inayotokana na Imani, mitazamo na misimamo ya mtu juu ya  jambo au kitu fulani.



Chanzo: Resane (2014) ukurasa wa 125
Ubora wa nadharia hii ni kwamba maneno yote dhahania yanapata kurejerewa maana zake, kwa sababu maana ya kitu au jambo linadhihirishwa akilini mwa mzawa wa lugha husika. Kwa mfano maneno ambayo hayana ubainifu wa moja kwa moja kiuhalisia ( maneno dhahania ) kama vile zimwi, shetani, usingizi, njaa, ukorofi, upepo, popobawa na mungu na kadhalika yote yanapata kurejelewa maana ambazo mzawa wa lugha huwa nazo akilini mwake.


Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba, neno moja linaweza kubeba dhana zaidi ya moja katika akili ya msikilizaji. Kwa mfano katika maneno yenye uhusiano wa kihomonomia, yaani umbo moja la leksimu lenye  kuwakilisha leksimu zenye maana zaidi ya moja.
Mfano 1.
Paka (i) – ni mnyama mdomo aina ya mamalia
Paka (ii) – ni kitendo cha kutia rangi au mafuta kitu chenye asili ya utambarare.
Hivyo ni vigumu kwa mtumiaji wa lugha kujua kuwa paka inayowakilishwa na mzungumzaji akilini mwake ni paka  yenye maana ya kuweka rangi au mafuta au mnyama.
Udhaifu mwingine ni kwamba hakuna picha ya jumla ya kitenzi, hasa kitenzi “kupiga” picha alionayo msemaji ni ya kitendo maalumu cha kupiga ama kwa kiboko, ngumi, kofi, teke au mpira nakadhalika. Pia kitenzi “cheza” kina maana zaidi ya moja , kwa mfano cheza  mziki au ngoma , cheza  soka (mpira wa miguu), rede  au kucheza kutingishika kutokana na mtetemeko wa kitu.


Nadharia hii imejikita katika moja ya maneno ambayo nomino hasa dhahania na kuacha aina nyingine za maneno kama kielezi na viunganishi, vihusihi na  vivumishi. Hivyo basi hakuna taswira au dhana ya baadhi ya aina za maneno kama vile sana, ni, na, lakini, kwa, kuliko na kadhalika.


Pia udhaifu mwingine wa nadharia hii ni kwamba, nadharia hii haiwezi kutoa maana katika sentensi na nahau. Kwa sababu dhana au taswira inajengwa katika neno na sio sentensi.
Kwa mfano
Jangala ameshikwa na usingizi mzito leo asubuhi
Shika msukani
Hivyo, hakuna taswira ya moja maana katika sentensi ya mwanzo kuna taswira zaidi ya moja pia katika nahau kuna taswira zaidi ya moja.Na ili upate maana yake lazima uzingatie muktadha wa nahau hiyo au sentensi hiyo. Hivyo kwa mfano (i) utatafsirika kama uchovu wa jangala, uzeme, au usingizi kweli na mfano (ii) maana yake ni kuongoza au kuwa mstari wa mbele na maana zote hutegemea muktadha ili kufasiliwa.
Nadharia ya maana kama  matumizi, kwa mujibu wa Resani, (2014 :127), anasema mwanafalsafa anaye husishwa moja kwa moja na nadharia ya maana kama matumizi  ni Ludwig Wittgestein mwaka 1930 alitamka kuwa “ maana ya neno ni matumizi yake katika lugha” (Philosophical Investigation 1963:43). Msisitizo wa nadharia hii upo katika maana ya neno au kisemo kilichotumika katika muktadha maalumu. Hivyo maana ya neno ni matokeo au athari inayotokana na matumizi.


Mfano maana ya kikombe; ni kifaa kinachotumika kubebea kitu cha hali ya kiminika
Ubora wa nadharia hii ni kwamba, ni rahisi kwa mtoto au mtu yeyote anayejifunza lugha. Kwa sababu mtoto anapojifunza lugha hujifunza maana ya viambo vya lugha kutokana na jinsi viambo hivyo vinavyotumika na wanalugha wa jamii.


Husaidia kupata maana ya maneno ambayo hayana ujazo wa kisemantiki. Kwa mfano maneno kama viunganishi, vihisishi na hata vielezi vinapata maana kupitia matumizi yake katika sintaksia ya lugha. Mfano katika katika sentensi neno “na” linakuwa na maana ya kiunganishi au kihusishi kutokana na matumizi yake katika sentensi.
Pia ubora wanadharia hii pia ni kwamba inaweza kutoa maana hasa katika methali na nahau na aina nyingine za tungo za kifasihi kwani nadharia hujikita zaidi katika muktadha. Kwa mfano, ukisema “ haba na haba hujaza kibaba” hivyo methali hii huwa na maana ambayo imejikita kimuktadha hasa kwa wafanyabiashara na hata wanajamii wengine ila hutafsiriwa tofauti kulingana na utofauti wa  kimuktadha.


Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba  hufanya maana ya neno iwe mali ya kundi fulani. Kwa mfano chombo cha moto chenye kufanana na baiskeli chenye kubeba vitu au abiria, kwa jamii nyingine hufahamu kama pikipiki lakini jamii nyingine huita toyo na wengine bodaboda hii hufanya utofauti katika maneno hurejelea matumizi sawa.

Udhaifu mwingine ni kuwa neno linaweza kuwa moja ila likawa na utofauti wa maana au utumizi wake kutokana na mabadiliko ya kimuktadha. Kwa mfano neno kaka , katika muktadha wa kifamilia ni ndugu mkubwa wa kiume mwenye kutoa msaada kwa ndugu wengine wadogo, ila katika muktadha wa hospitali ni ugonjwa wenye kunyong’onyesha vidole. Pia neno Mpira ni kitu cha kufungia vitu au  ni kitu cha uduara chenye kutumika katika michezo mbalimbali.

Udhaifu mwingine ni kwamba kitu au kifaa hutenezwa kwa matumizi fulani lakini jamii inaweza kukipa kifaa au kitu hicho matumizi mbadala tofauti na kusudia lake. Hivyo nadharia hii huhalalisha tabia ya mabadiliko ya maana kutokana na matumizi. Kwa mfano, poda ilitenezwa kwa matumizi ya urembo lakini jamii hutumia kama dawa ya kuondoa vipele au chunusi pia hutumika kuulia wadudu kama sisimizi. Hivyo hutupa mkakasi katika kutoa maana ya neno hilo kimatumizi.
Nadharia ya kichocheo, kwa mujibu wa Resani (2014) nadharia hii imeasisiwa na mtaalamu Broomfield (1933) na Skiner na Watson, nadharia hii imejikita hasa katika kuchunguza maana ya umbo la kiisimu na hali ambamo msemaji hutamka umbo hilo na mwitiko huibuliwa na msikilizaji. Maana ni kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji. Mtaalamu huyu anadai kuwa maana ya kisemo kuwa katika neno uneni.

Nadharia hii huonesha kuwa maana lazima ipatikane kutokana na kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji. Lakini maana huegemea zaidi katika mwitiko wa msikilizaji namna atakavyopokea kichocheo hicho
Kwa mujibu wa broomfield anaeleza vitu vitatu yaani kichocheo tamko na mwitiko. Kama ifuatavyo

Ubora wa  nadharia hii ni kwamba nadharia imejikita zaidi katika ujaribizi  wa utafiti wa kisayansi, ambapo ulijikita katika utabia ambao umejikita katika mkondo wa mawazo wa upositivisti wa kimantiki. Yaani akili ya mtu au mawazo yanaibua tendo au utabia ambao mtu anafanya kutokana na mwitiko unaotokana na kichocheo.
Ubora wa nadharia hii pia mwitiko hutoka katika akili ya mwanadamu na lugha pia hufuata mfumo wa ubongo, hivyo huonesha uhusiano baina ya lugha na mfumo wa ubongo wa mwanadamu.

 Hivyo kila kisemwacho huchanganuliwa akilini mwa msikilizaji na hutolewa maana yake.
Udhaifu wa nadharia hii ni vigumu kuoanisha tamko na mwitikio sahihi au mwitiko sahihi. Kwani mwitiko hutegemea uelewa wa tamko na kichocheo chake. Mfano “toka nje”  ambapo maana yake humaanisha ingia ndani ila msikilizaji anaweza kuelekea nje kutokana na uelewa wake.


Pia mtazamo huu unaweza kueleza maana za semo chache tu za lugha kwa kuwa hali nyingi sana za matumizi zimechangamana. Semo nyingi sana katika lugha hazidhibitiwi na kichocheo chochote katika miktadha zitokeamo. Mfano, mtu aliuzwapo swali si lazima hajibu au si lazima hatoe jibu lililotazamiwa.


Pia baadhi ya maneno hayana mwitiko wake katika lugha. Hasa maneno kama nomino. Kwa mfabo kisu, panga , paka, na kadhalika. Mzumzaji anaweza kutumia neno lakini lisiathiri chochote kwa msikilizaji.

Kiujumla, maana ya maana haiwezi kupatikana katika nadharia moja tu bali kwa kutumia nadharia mbalimbali  kama zilizotajwa hapo juu na nadharia nyingine mbalimbali kama vile uelekezi, masharti ukweli na ujinasishaji na kadhalika. Hii yote huonesha kuwa maana ya maana ni fahiwa nyingi inaweza kudokeza sababu, kusudi, ishara, urejeleo, maelekezo au ufafanuazi na ukweli . hivyo ni vigumu kueleza manana ya maana kama ilivyo.







                  MAREJELEO.
Habwe. J na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publisher.
Resani,M (2014). Semantiki na Pragmantiki ya Kiswahili. Dar es Salaam:Karljamer Print
                              Technology.
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu: Dar es salaam. TUKI.
Wamitila, K.W (2003). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Kenya Focus
Publication.
masshele.blogspot.com

No comments:

Post a Comment