Sunday

MAENDELEO YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI

0 comments
Historia ya Tamthiliya ya Tanzania.
Kabla ya kuja kwa Ukoloni tamthiliya haikuwepo nchini. Aina za sanaa za maonyesho zilizokuwepo zilitofautiana na tamthiliya hii iliyoingizwa na tamaduni ngeni. Chuo kikuu huria cha Tanzania (1997:39).
Bertoncini,1989, kama ilivyodondolewa na Wafula,Richard,(1999:3) anafafanua kuwa: Tamthiliya kama utanzu wa fasihi- andishi katika lugha ya Kiswahili imeanza kushughulikiwa juzu juzi, mchezo wa kuigiza ulioandikwa ulikuja na wakoloni. Mgeni aliyejihusisha na uigizaji hapo mwanzomwanzo aliitwa Graham Hyslop mnamo mwaka 1936 alitunga filamu iliyoitwa, “Akili ni mali” Tamthiliya ilianza Tanzania wakati wa Ukoloni miaka ya 1920, tamthiliya hizo zilizo nyingi zilikuwa za kidini.

Tamthiliya zilizoandikwa ili zigezwe jukwaani hazikuwepo kabla ya Ukoloni. Badala yake, zilikuwepo tamthiliya zisizoandikwa, ziligezwa au kufaraguzwa kwa ajili ya kuonyeshwa kwenye shughuli maalum, kwa mfano, kwenye sherehe za jando na unyago, mazishi, kutawazwa kuwa mtemi, arusi na michezo ya watoto. Tamthiliya hizo zilikuwa na sifa kadhaa za kitamthiliya, yaani hadithi, vitendo, wahusika, na waigizajiwao na dialogia. Kadhalika zilkuwepo na sifa saba za sanaa za maonyesho, nazo ni:

 i) Dhana inayotendeka          v) hadhira
ii) Uwanja unaotendewa         vi) kusudio la kisanii
iii) Watendaji                           vii) muktadha wa kisanaa
iv) Ubunifu (umathilishaji)

Muhando Mlama na Balisidya 1976:4 na Mlokozi, M . M.(1996:189).
Tamthiliya hizo hazikuwa na ploti ya Ki- Aristotle wala matini yaliyoandikwa. Hivyo zilikuwa ni tamthiliya – simulizi. Mulokozi, M.M.(1996:203).
Anaendelea kudondoa kwa kutolea mfano michezo ya watoto katika kuigiza , umama, mtoto wa kike au wakiume n.k.  Mchezo huu ni tamthiliya halisi yenye kumathilisha maisha.


Tamthiliya andishi ya Kiswahili
Tamthiliya za Kiswahili zilizoandikwa kwanza kabla ya kuigizwa jukwaanizilianza kutokea miaka ya 1950.  Tamthiliya za mwanzo zilikuwa za kidini. Kwa mfano, ilichapishwa tamthiliya ya Frank, C.(1951) iliyoitwa“Imekwisha” (Mulokozi,M.M. 1992:205).

Tamthiliya za mwanzo zisizokuwa za kidini zilianza kutungwa kati ya 1952 na 1956. Shughuli za tamthiliya wakati huo zilisimamiwa na Graham Hyslop, Mwingereza aliyekuwa katika utumishi wa serikali ya kikoloni ya Kenya. Pia alianzisha kikundi cha maigizo kwa ajili ya askari mwaka 1944, na miaka ya 1950 alianza kutunga michezo ambayo iliigizwa na kikundi chake. Michezo ya mwanzo katika lugha ya Kiswahili ni“Afadhali Mchawi” (1957), na“Mgeni Karibu” (1957), hata hivyo Hyslop alianza kuzunguka katika shule na vyuo mbalimbali nchini Kenya akifundisha muziki na uigizaji.
Miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo wa Hyslop waliokuwa wakisoma “Alliance high school” ni Henry Kuria, Kimani Nyake, Gerishon Ngugi na B.M.Kurutu. Tamthiliya ya Kuria,‘Nakupenda Lakini’ (1954) iliigizwa kwa mara ya kwanza 1957, ya Nyake , ‘Maisha ni Nini’ iliigizwa mwaka 1955, ya Gerishon Ngugi, ‘Nimelogwa nisiwe na Mpenzi’(1961) iliigizwa mwaka 1956, na ya  Kurutu ‘Anatakiwa Polisi’mwaka 1957, kwa mujibu wa Ngugi wa Thiong’o(1981:39) kama ilivyodondolewa na Mulokozi,M.M. (1996:205).

Kwa ujumla tulipopata uhuru, tamthiliya zote za Kiswahili zilizochapishwa zilikuwa zimeandikwa na Wakenya. Watanzania hawakujitokeza katika uwanja huu hadi baada ya uhuru. Kwa mujibu wa Mulokozi,M.M.(1996:205).

TAMTHILYA WAKATI WA UHURU
Tamthilya ya kizungu iliendelea kuigizwa hata baada ya uhuru, mashuleni na katika kumbi maalum za maonyesho kama ‘Little Theatres’. Hata hivyo, umaarufu wake ulipungua kiasi, hususan kwa upande wa Tanzania. Mulokozi, M.M.(1996:207)
Anaendelea kufafanua, licha ya tamthiliya za kizungu, hali kadhalika tamthiliya za kiafrika zilianza kuandikwa kwa lugha za Kigeni na zingine za kiafrika, zilifasiriwa kwa Kiswahili, kwa mfano, “I will marry when I want” (1982) ilifasiriwa kwa Kiswahili, “Nitaolewa nikipenda” (1982) na Ngugi wa Thiong’o na Ngugi wa Mirii.

Watanzania waliathiriwa sana katika masuala ya sanaa za maonyesho za kigeni kiasi kwamba waliweza kujishirikisha kikamilifu katika kutunga tamthiliya na kuzionyosha majukwaani. Tamthilya hizi hazikuwa na maana yenye uzito wowote kwa tamaduni zao.  Tamthiliya hizo ziliongelea juu ya jamii ambayo watanzania hawakuifahamu wala kuielewa wao walivutiwa na mavazi ya washiriki, matumizi ya taa za rangi na kadhalika, 

Mlama, P.(1987:119) vol.54/2 jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili .
Mlama , P.(1987:119- 120) anasisitiza, kutokana na tamthiliya za kimagharibi kutokidhi mahitaji ya watanzania ndipo ilipowapelekea wasanii hao kuanzisha vichekesho.
Mlama, P.M.katika makala ya semina ya kimataifa ya uandishi wa Kiswahili iii,(1983:206- 207), afafanua kuwa drama ililetwa Tanzania na Waingereza. Drama iliigizwa mashuleni ambapo wengi wa walimu walikuwa Waingereza. Madhumuni ya kuigiza drama haikuwa na uzito mkubwa.  Hasa Waingereza walikuwa na kitu cha kupitisha muda, wakati ambapo walikuwa hawna la kufanya. Waliona kuendesha drama kwao ni jambo borakwani ilihusu utamaduni wa kwao na kuweza kujikumbusha kwao. Kwa mfano tamthiliya za William Shakespeare, Julius Ceasar, Macbeth, n.k. hazikuwa na maana muhimu kwa watanzania kwani walioshiriki walikuwa wanakariri tu maneno bila kuelewa yale waliyoyasema, mara nyingi tamthiliya hizi zilikuwa na lengo la kuburudisha tu.

Mlama , naendelea wakati drama hii ya kigeni ilpoendelea kushika mizizi chini ya udhamini wa wazungu. Iliibuka aina nyingine ya drama, hii ni ile ijulikanayo kama, “vichekesho”hii ilitokea kwasababu watanzania ambao walivutiwa kutumia vipaji vyao vya kisanaa kuonyesha tamthiliya, lakini hawakuwa na ujuzi wa ndani wala iwezo wa utunzi na uonyeshaji wa tamthiliya kiasi cha kutoa kazi sawa na zile za wataalam wa 

Kiingereza. Badala yake walianzisha kitu kinachofanana na tamthiliya lakini ambacho waliweza kutunga na kuonyesha kutokana na uwezo wao wenyewe. Juhudi zao zilitoa aina ya drama iliyojulikana kama “vichekesho”.

Hii haina maana kuwa vichekesho vilikuwa duni kuliko drama ya wageni.  Bali vichekesho vilitoa drama iliyokuwa na tabia kisanaa tofauti na drama yenyewe. Kwa mfano, vichekesho havikutegemea tamthiliya ilyoandikwa bali, tungo zake zilitungwa palepale wakati wa kutenda, vichekesho vilihusu maisha ya kawaida ya Tanzania ya wakati ule, wakati ile drama nyingine ilihusu jamii za Ulaya. Mfano wa kichekesho cha wakati huo ni “Mshamba wa Kioo”

Baada ya uhuru vichekesho vilichukua sura tofauti kidogo. Badala ya kuwasuta “washamba” vilianza kuwasuta “wazungu weusi” Waafrika wanaoringia elimu au vyeo vyao na kudharau utamaduni wao. Kwa mfano, G. Uhinga, 1968, pia viliongelea masuala mbalimbali kwa mfano , matatizo ya kifamilia, ukosefu wa kazi, ukimwi,  uhalifu na udanganyifu waganga wa jadi n.k.M.M.Mulokozi(1996:206)
Naye Lihamba,(1985:281) kama alivyodondolewa na M.M. Mlokozi(1996:206) anasisitiza; vipo vichekesho vya kisiasa vyenye kuzungumzia siasa ujamaa, ubinafsi wa uongozi, matatizo ya kuanzisha vijiji vipya n.k. Anaendelea kusisitiza,
“Beside their informality and flexibility, these plays have two major Other characteristics: they have displayed a strong alignment with the political and social issues after Arusha and have a strong comedic bias.  The tendency to favour comedic elements or play for laugh has endowed.  The plays with the collective name of vichekesho.  This has been irrespective of the nature of the content and the performance objectives.”

Tafsiri:
Hata hivyo baadhi ya vichekesho vya Radio Tanzania, kwa mfano,  “mahoka” kipindi kilichoanza mwaka 1974 na “pwagu na pwaguzi” mwaka 1979 hukejeli na kukemea tabia mbovu za baadhi ya watu, wakiwemo viongozi wa kisiasa. Tasnifu ya Lihamba(1985) imeonyesha kuwa baada ya Azimio la Arusha nchini Tanzania vikundi vya ngoma na maigizo kama ishirini na nane(28) mara kwa mara vilionyesha maigizo yaliyohusu siasa. 

Baadhi ya maigizo hayo yalitukuza siasa ya ujamaa na kutangaza kampeni mbalimbali za wanasiasa. Lihamba, (1985:498- 502). Hata hivyo kwa sasa vichekesho hutangazwa katika vituo vya redio na televisheni, na huonyeshwa kwenye kumbi za starehe.

Baada ya uhuru, utunzi wa tamthiliya ulipamba moto zaidi, hasa upande wa Tanzania. Mashindano ya utunzi na uigizaji yaliendeshwa na Youth Drama Association nchini Tanzania yaliwawezesha watunzi chipukizi kujitokeza, akiwemo Ebrahim Hussein ambaye tamthiliya yake ya kwanza , “wakati ukuta” 1969 ilishinda tuzo katika mashindano hayo. Wakati huo huo ndipo walipojitokeza watunzi waliohitimu chuo kikuu cha Dar es Salaam. Baadhi yao ni Ebrahim Hussein mwenyewe, Penina Mhando(Mlama), N.Ngahyoma na G. Uhinga.

Miaka ya 1970- 1974 ilishuhudia kuchapishwa kwa tamthiliya nyingi za Kiswahili. E.Hussein alichapisha, Kinjeketile(1969), Mashetani(1971), Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi(1976), Arusi(1980) na Ukingo wa Thim(1989).
Penina Mhando, alichapisha “Hatia”(1972), Tambueni Haki Zetu(1973), Pambo(1975), Nguzo mama(1982), Lina Ubani(1984); Pia watunzi wengine waliojitokeza kipindi hiki ni Emmanuel Mbogo, “Giza Limeingia”(1980), Tone la mwisho,(1981), Ngoma ya Ngwanamalundi(1988), Morani, (1993); watunzi wengine ni M. M. Mlokozi, S.A. Mohamed, E. Semsaba na E. Kezilahabi.

Orodha hii ya watunzi inatosha kueleza kuwa utunzi wa tamthiliya ya Kiswahili umepiga hatua kubwa tangu mwaka 1970. Kimaudhui tamthiliya hizo zilianza kusawiri mazingira ya waswahili kwani kwa kuchunguza suala la maudhui tunaweza kuzigawa tamthiliya za Kiswahili za miaka ya 1960- 1994 katika migogoro kama ifutavyo:
Kuna migogoro ya kitamaduni: Dhamira hii inajitokeza katika umbo la mgongano wa  utamaduni wa kijadi na kiafrika na utamaduni wa kizungu au kati ya mjini na shamba, dhamira hii imejadiliwa zaidi katika baadhi ya kazi za E,Hussein, wakati ukuta na kwenye ukingo wa thim.

Pia matatizo ya kijamii kwa mfano, mapenzi, ndoa, ufukara, urithi, n.k, vimejadiliwa zaidi katika tamthiliya ya,Nakupenda Lakini  na Nimelogwa nisiwe na Mpenzi.
Si hizi tu bali wasanii wa tamthiliya wa kipindi hiki waliangalia jamii jinsi inavyoishi na kuweza kutunga kazi zao kusawiri mazingira husika. Kwa mfano maudhui katika tamthiliya yalikuwa pia; ukombozi na utaifa, ujenzi wa jamii mpya, mfano tamthiliya ya E. Mbogo, Giza Limeingia, na E. Hussein, Mashetani. Mwanamke na matatizo ya kijinsia mfano Nguzo Mama(Mhando), Machozi ya Mwanamke(Ngozi), na falsafa ya maisha mfano E.Kezilahabi

No comments:

Post a Comment