@masshele
(iii). Taathira na uazimaji
DHANA YA FASIHI LINGANISHI
Ponera (2014) akimnukuu Stallknecht (1961) Fasihi linganishi ni uwanja wa kitaaluma unaoshughulika na fasihi mbili au zaidi zinazohusisha vipengere tofauti vya kitamaduni. Anaongeza kusema kuwa fasihi linganishi hujihusisha na uchunguzi na ulinganishaji wa aina mbalimbali ya sanaa, kwa mfano, uhusiano wa filamu na muziki au fasihi na uchoraji.
Zepetnek (1996) akinukuliwa na Ponera (2014), Fasihi linganishi ni taaluma inayojihusisha na uteuzi, na uchambuzi wa vipengere mbalimbali vya kazi ya fasihi kama vile kanuni, mafundisho, na tamaduni ambavyo vinapatikana katika kazi za fasihi za jamii mbalimbali.
Wamitila (2003), Fasihi linganishi huhusisha uchunguzi wa maandishi ya wakati mmoja, aina moja na katika lugha mbalimbali kwa nia ya kumulika sifa inayohusisha kama athari, vyanzo, sifa zinazofanana tofauti za kiutamaduni. Anaendelea kusema inawezekana kufanya hivyo pia kwa nia ya kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au hata nadharia za kiuhakiki, fasihi ya namna hii iliwekewa misingi na juhudi za wana isimu kuanzia kulinganisha lugha mbalimbali katika karne ya 19.
Boldor (2003) akimnukuu Compbell (1926) Anaeleza kuwa fasihi linganishi ni taaluma inayochunguza uhusiano uliopo baina ya faasihi mbili au zaidi nje ya mipaka ya kitaifa kwa njia ya kulinganisha mfanano na msigano.
Remak (1971), anafasili fasihi linganishi kama uwanja wa kifasihi unaohusika na uchunguzi na mahusiano ya kifasihi nje ya mipaka ya nchi moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo.
Hivyo, fasihi linganishi ni uchunguzi wa maandishi na masimulizi ya wakati mmoja na katika lugha mbalimbali kwa kuhusisha au kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au nadhariaa za uhakiki ambapo kufanana, kutofautiana na hata ubora na udhaifu huzingatiwa.
MKONDO WA KIFARANSA KATIKA KUITAZAMA FASIHI LINGANISHI
Huu ndio mkondo wa kwanza kuibuka na kuanza kushughulikia masuala yahusianayo na taaluma ya fasihi linganishi. Mkondo huu ulianza huko Ufaransa mwishoni mwa karne ya 19 katika chuo cha Sarborne, uliendelea kushika hatamu hadi wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Mkondo huu ulikuwa maarufu kwa jina shule ya Kifaransa (French school) ambapo wadau wake walianzia katika wazo la kutafuta ithibati za chanzo na athari za kazi mbalimbali za kimataifa. Wao walijikita katika kuchunguza jinsi mawazo ya kisanaa pamoja na motifu zake zilivyokuwa zinaenea kutoka sehemu moja hadi nyingine (Ponera 2014).
WAASISI WA MKONDO WA KIFARANSA
Waasisi wa mkondo huu ni Jean Marie Carre, Marius Francois Guyard na Tieghem. Licha ya kuwepo kwa waasisi hawa, pia kuna wanafasihi waliosaidia kukuza na kuendeleza mkondo huu kama vile, Abel Francois Villmain ambaye aliandika kitabu kiitwacho “literature compare”. Wengine ni Jacques Derrida, Piere Bourdien, Lucien Goldman, Auguste Comte, Fredric Mistral na Sullt Prunghomme. Wadau hao walifanya shughuli zao za chini ya jumuiya yao iliyojulikana kama “French Comperative Literature Association (FCLA)” (Ponera 2014).
FASILI YA FASIHI LINGANISHI KWA MKONDO WA KIFARANSA
Wao wanafasili fasihi linganishi kama ni utanzu wa fasihi ambao hujikita katika kutafuta mahusiano mwafaka kati ya fasihi mbili au zaidi ambazo zina asili tofauti kijamii na kiuwasilishaji (kilugha).
Jean Marie Carre anafasili fasihi linganishi kama utanzu wa historia ya kifasihi kwa kuwa hushughulikia ulinganishi wa misukumo ya kijamii au mataifa.
Kwaupande mwingine, wafuasi wa mkondo huu wanaongeza kuwa taaluma hii hainabudi kufanyika miongoni mwa jamii mahususi.
Tieghem anaifasili fasihi linganishi kwa kuitenganisha na fasihi kwa ujumla, yeye anasema kuwa tafiti zote zinazochunguza uhusiano wa sifa jumuishi baina ya fasihi anuai huitwa fasihi kwa jumla. Lakini fasihi linganishi kama uchunguzi wa kazi mbili (vitabu viwili, watunzi wawili, makundi mawili ya vitabu au watunzi).
Guyard kwa upande mmoja anakubaliana na Remaki (remaki alisema juu ya fasihi linganishi na fasihi kwa ujumla hazitenganishiki) kuwa fasihi kwa ujumla na fasihi linganishi hazitenganishiki, zote zinaongozwa na methodolojia ya kiulinganishi. Kwa upande mwingine anakubaliana na hoja ya Tieghem kuhusu fasihi kwa ujumla na fasihi linganishi kuwa mtazamo wake unatoa mawanda mapana na angavu zaidi kuhusu fasihi ya jumla kuliko faishi ya kitaifa na fasihi linganishi.
MISINGI YA FASIHI LINGANISHI KWA MKONDO WA KIFARANSA
(a) Mipaka ya kijiografia na kilugha au kiisimu
Fasihi linganishi inapaswa kuhusisha fasihi za mataifa au jamii mbili ambazo zinatofautiana kijiografia pamoja na kutofautiana kiisimu au kilugha; fasihi ya Kiswahili ilinganishwe na fasihi ya Kirusi, Kitaliano na Kichina, lakini huwezi kufanya ulinganishi baina ya fasihi moja, mfano mtu kufanya ulinganishi kati ya riwaya za Shabani dhidi ya riwaya za Ephrais Kezilahabi.
(b)Uchunguzi uwili.
Fasihi linganishi inahitaji kuhusisha kazi mbili za fasihi, kazi moja haiwezi kufanyiwa uchunguzi wa kiufasihi linganishi, lazima kuwepo na vitu viwili vinavyohesabiwa kijiografia na kiisimu. Hivyo ili kufanya ulinganishi ni lazima kuwepo na kazi mbili zilizotofautiana kiisimu na kijiografia, mtu anaweza kufanya ulinganishi kati ya riwaya za wamitila dhidi ya riwaya za Shark Spear.
(c) Fasihi zenye watunzi mahususi
Katika kufanya ulinganifu ni lazima kazi zinazotumika au zitakazotumika ziwe ni fasihi andishi tu, hivyo kazi za fasihi simulizi ambazo kimsingi watunzi wake hawafahamiki hazitahusika katika taaluma ya fasihi linganishi.
(
d)Taathira ziletwazo na vichocheo nje katika fasihi.
Kwa namna gani fasihi ya taifa moja imeathiri fasihi nyingine, kwa namna gani utamaduni wa taifa fulani umeathiri fasihi na utamaduni wa taifa jingine, matini husika za fasihi hazichunguzwi kiundani, msisitizo upo katika maudhui zaidi kuliko fani.
NYANJA ZA FASIHI LINGANISHI KWA MKONDO WA KIFARANSA
Wanafasihi wa mkondo wa Kifaransa walifanyia kazi katika vipengere vya taathira, Upokezi, Mwigo, Uazimaji na ushirika sawia usioepukika kama nyaja za fasihi linganishi;
USHIRIKA SAWIA USIOEPUKIKA KATI YA NYANJA ZA FASIHI LINGANISHI
Katika Nyanja hizo ambazo ndizo wanamkondo wa Ufaransa walizozitalii zaidi walionyesha ni kwa jinsi gani mikondo hiyo hushirikiana katika kukamilishana.
Ulrich Versstein anatoa rai kuwa kuna taathira, mwigo na uazimaji, lakini pia kunatofauti baina ya michakato hiyo kama ifuatavyo;
Taathira
Kwa mtazamo wa mkondo huu, taathira ni msambao au kusambaa kwa wazo, dhamira, taswira au jadi fulani ya kifasihi toka kazi moja ya kifasihi kwenda katika kazi nyingine ya kifasihi (kwa kujua au kutojua).
Zipo taathira za namna nyingi katika fasihi kama ifuatavyo:
A. Taathira za kifasihi na zisizo za kifasihi
Hizi huchunguza na kufafanua chimbuko la mahusiano sawia baina ya fasihi mbili au zaidi. Mfano, ushairi wa Kiswahili na ushairi wa Kiarabu ni za kifasihi lakini ushairi wa Shabani Robert na utamaduni wa kiislamu si za kifasihi. (hii imepuuzwa sana na mkondo wa Kifaransa kwa maana ya kwamba msanii anatumia taathira zisizo za kifasihi kama malighafi katika kuunda kazi mpya).
B. Taathira za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja
Taathira isiyo ya moja kwa moja hutokea pale moja ya njia zifuatazo zitasababisha mwingiliano baina ya kazi za kifasihi, ziara za mtunzi, mapokeo simulizi ya kijadi, hojaji mbalimbali na shajara za watunzi binafsi. Pia taathira ya moja kwa moja hutokea pale kunapokuwepo na mtaguso halisi baina ya wanaoathiriana. Mitagusano halisi huweza kutokea kwa mtunzi mmoja kusoma kazi ya mtunzi mwingine, mtunzi mmoja kuonana ana kwa ana na mtunzi asilia,au mtunzi mmoja kuwasiliana na mtunzi mwingine kwa njia yoyote ya kimawasiliano.
C . Taathira chanya na taathira hasi.
Kitendo cha mtunzi wa kazi ya fasihi toka taifa fulani kutumia vipengere vya fasihi toka fasihi ya taifa linguine katika kuumba fasihi bora na fanikivu ya taifa lake ni ishara ya taathira chanya, mtunzi wa kazi ya kifasihi pia anaweza kuandika kinyume na kazi fulani au kwa kutengua kanuni na maudhui yaliyoelezwa katika fasihi ngeni itakuwa ni ishara ya taathira hasi katika fasihi.
UHUSIANO WA TAATHIRA NA MICHAKATO MINGINE
Mchakato wa kitaathira unahusiana sana na michakato ya upokezi, mwigo na uazimaji.
(i) Taathira na upokezi
Hakuna taathira zinazoweza kutokea kati ya mtunzi mmoja na mwingine pasipo upokezi wa kazi ya kisanaa toka nje ya mipaka ya kitaifa. Upokezi unaweza kuitwa kuwa ni mchakato mmojawapo kuelekea katika taathira.
Upokezi wa kazi ngeni ya kisanaa katika taifa haina maana wala hailazimishi kuwa hiyo ni ishara njema ya athari chanya. Mchakato wa kiupokezi si wa kiholela au bahati mbaya, bali ni mchakato wenye utaratibu mahususi kwa kuwa unatokea pale tu kazi ngeni inapoleta tija za kiutamaduni na kiitikadi zinazoafikiana na taifa husika.
(ii) Taathira na mwigo
Taathira ni zaidi ya mchakato au kitendo cha kuiga ama kuchukua vipengere fulani vya fasihi ngeni katika fasihi ya taifa mahususi.
(iii). Taathira na uazimaji
Si lazima mchakato wa uazimaji vipengele vya kifasihi toka eneo moja hadi jingine uonekane kama ni uumbaji upya wa vipengele hivyo, ila uazimaji unaweza pia kuonekana kama uumbaji wa dhana na maudhui mapya kabisa lakini yenye kuchimbuka au yenye asili toka katika fasihi ngeni. Muhimu ni kuwa, vipengele vya taathira ya fasihi ngeni katika taifa fulani hubebwa ndani ya matini husika. Mhakiki anapaswa kuchunguza au kuchanganua kwa makini matini nzima na azingatie au atilie maanani mchakato wa taathira katika fasihi husika. Mchakato huo unaanzia katika tafsiri ya kazi ya fasihi ngeni kupitia michakato ya uigaji na uazimaji.
Uazimaji hutazamwa kama ufafanuzi wa mwigo katika mawanda mapana. Uazimaji unaweza kuwa upangiliaji upya wa vipengele bora vya fasihi ngeni katika namna ambayo haipendezeshi zaidi fasihi ya taifa. Katika uazimaji, mtu anafananishwa na mtafsiri ambae anafungwa na umbo la matini chanzi au asilia, lakini katika uigaji, mtunzi hafungwi na umbo la matini asilia. Michakato yote miwili katika fasihi linganishi inaweza kufikiriwa kwa namna mbili;
(a). Ubunifu wa kisanaa
Fasihi iliyoathiriwa hupokea au huchukua mbinu mpya toka katika fasihi ngeni (iliyoathiri).
(b). Wizi wa kitaaluma
Kuazima vipengele vya fasihi toka fasihi ngeni pasipo kurejelea vyanzo husika, hali hii huitwa wizi wa kitaaluma.
UBORA WA MKONDO WA KIFARANSA KATIKA FASIHI LINGANISHI
(i). Mawazo yao mengine yalihusu kuithamini lugha kama nyenzo muhimu katika utendaji wa sanaa yoyote, hivyo mtu anapofanya ulinganifu wa kazi za kifasihi lazima awe na umilisi wa lugha ya kazi husika.
(ii). Waliamini kwamba kila jamii ina kaida zake za kimaisha, hivyo nivyema kuzingatia historia au utamaduni wa mtunzi wa kazi husika unapolinganisha na kazi zingine za kifasihi.
(iii). Waliamini kuwa fasihi linganishi ni lazima ionyeshe ulinganifu mkubwa wa kijiografia kutoka jamii ya msanii mmoja hadi jamii ya msanii mwingine.
(iv). Pia waliamini kuwa fasihi linganishi ilenge mambo yanayotendeka kila siku katika jamii kwa lengo la kuonesha ubora, uzuri, ubaya na namna ya kuboresha kaida za utamaduni, lugha, siasa na uongozi katika jamii.
(v). Mkondo huu ndio ulitoa nafasi au mwanya kwa mikondo mingine au mataifa mengine kujikita zaidi katika fasihi simulizi.
MAPUNGUFU YA MKONDO WA KIFARANSA KATIKA FASIHI LINGANISHI
(i). Mkabala huu umemakinika zaidi na vichocheo vya nje vinavyoathiri fasihi za mataifa mawili au zaidi, hatimaye umeifanya taaluma ya fasihi linganishi itawaliwe au iongozwe na mbinu za zamani za kiuchunguzi au za kihistoria na kichanya.
(ii). Mkabala huu umening’iniza fasihi linganishi katika mipaka ya kiisimu na kimahali baina ya fasihi, unawafanya wanafasihi waendelee kuichunguza fasihi katika mlengo wa kimagharibi.
(iii). Mkabala huu unatenganisha au unashindwa kuweka bayana mpaka au mipaka baina ya fasihi kwa ujumla na fasihi linganishi.
(iv). Mkondo huu hauruhusu kazi za kifasihi zitokazo katika taifa moja kufanyiwa uchunguzi linganishi.
(v). Misingi inayoelekezwa na mkabala huu inatenganisha baina ya vichocheo nje na vichocheo ndani (fani na maudhui) vya kazi ya fasihi. Hatuhitaji kuchunguza kwa undani matini zenyewe za kifasihi, bali tunapaswa tuchunguze mambo yatokayo nje ya jamii husika na namna yalivyochochea kuibuka na kufifia kwa vipengere anuai vya kifasihi.
MAREJELEO
Ponera, S. A. (2014), Utangulizi wa Nadharia ya Fasihi Linganishi: Dar es salaam. Tanzania.
Remak. H.H. (1971) “Comparative Literature :Its definition and function’’ (Method and Parspective), Edited by Newton.B.Stalknecht and Horst Frenz, USA October 1973.http://www.ocia.org
Rene H.H. Wellek, First Edition (1949) Theory of Literature , Translated into Arabic by Muhy Uddin Subhi, Published by Suprome Council for Literatures, Arts and Social Science ,Domascus 1972.
Wamitila K.W (2003), Kamusi ya Fasihi,Istirahi na Nadharia, Nairobi: Kenya.