Tuesday

TADIYE, DTBi wafungua milango kwa vijana, wanawake kupata mitaji ya biashara

0 comments

Ujasiriamali na biashara ndogo ndogo ni shughuli zinazowasaidia wanawake kujipatia kipato na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Picha| Mtandao.

  • Ni kupitia shindano la andiko bora la biashara ambapo washindi watapata ruzuku ya mitaji unaofikia hadi kiasi cha Sh20 milioni. 
  • Wanafaika wa fursa hiyo ni vijana wabunifu na wanawake wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Dar es Salaam.  Mradi wa uwezeshaji wa vijana (TADIYE) kwa kushirikiana na atamizi ya Teknohama ya Dar es Salaam (DTBi) wamefungua mlango kwa vijana wabunifu pamoja na wanawake wadogo wanaoishi kwenye mazingira magumu kupata mitaji ya kuendeleza biashara zao ili kujikwamua kiuchumi. 
Fursa hiyo imetolewa kupitia shindano la andiko la biashara ambapo mipango bora ya biashara isiyopungua 20 ina nafasi ya kujishindia ruzuku ya mtaji unaofikia hadi kiasi cha Sh 20 milioni. 
Kwa mujibu wa taarifa ya shindano hilo ilitolewa leo (Aprili 2, 2019) inaeleza kuwa fursa hiyo inatolewa kwa muombaji kujisajili na kupata mafunzo ya ujasiriamali kupitia mfumo wa “BESP” wa mradi wa TADIYE unaowapa walengwa wa mradi nafasi ya kushiriki katika shindano la andiko bora na la ubunifu.
“Vijana wenye mawazo bora ya ubunifu pamoja na wanawake wadogo wanoishi kwenye mazingira magumu wataandaa na kuwasilisha mawazo yao yatakayofanyiwa uchambuzi kutumia kamati maalumu ya wabobezi wa maswala ya biashara na ujasiriamali,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 
Sifa za muombaji ni lazima awe mwanaume au mwanamke mwenye umri wa miaka 15 hadi 35, lazima awe anatokea Tanzania bara au visiwani Zanzibar na awe uwezo wa kuzungumza wa Kiswahili au Kiingereza. 
Sifa nyingine ni kujisajili na kupata mafunzo kupitia mfumo wa BESP na kukamilisha angalau masomo matano ikiwa ni pamoja na somo la uandaaji wa mpango wa biashara wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT)  kama chombo au kiwezeshi cha wazo hilo. 
Pia wazo pendekezwa lazima liendane na sheria na taratibu za Tanzania na kama litaibuka na ushindi, muombaji atatakiwa kutumia fedha hizo kutekeleza mradi wake na si vinginevyo.


    Muombaji atawasilisha maombi yake kupitia mfumo maalum wa uwasilishaji maombi unaopatikana kwenye tovuti ya mradi wa TADIYE (BOFYA HAPA
    Mradi huo wa uwezeshaji vijana  ulianzishwa kwa lengo la kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana hasa wanawake wadogo wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia elimu na ujuzi wa kijasiriamali kidigitali.
    Ili kuweza kufikia malengo yake, DTBi na washirika wake walikuja na mfumo wa kibunifu ujulikanao kama “BESP App” unaotumika kutoa elimu ya ujasiriamali mtandaoni kwa kutumia simu ya mkononi.
    Mfumo huo una masomo au madili nane ambazo zimetengenezwa kisanifu kuweza kukidhi mahitaji ya walengwa wa maradi wa TADIYE.

    No comments:

    Post a Comment