- Mafanikio ya chochote unachokifanya ili kukuletea tija katika maisha yanatagemea zaidi mapenzi uliyonayo juu ya kile unachoweka mkono wako kufanya.
- Licha ya kuanzisha bidhaa au huduma bora waanzilishi wana sababu ya kujenga timu zao.
Ukosefu wa ajira, uthubutu na nia ya kuwa na biashara binafsi ni mambo kadhaa yanayochochea uanzishwaji wa kampuni zinazochipukia nyingi zinazoanzishwa na vikundi vya vijana nchini.
Malengo makuu ya kuanzishwa kwa kampuni hizo sehemu kubwa ni kujikwamua na hali ya kiuchumi na hata kusaidia jamii katika mambo mbalimbali. Mfano, kupitia teknolojia baadhi ya vijana wamebuni programu za simu ama kompyuta ambazo zinasaidia kujifunza kwa wanafunzi wa chekechea hadi elimu ya juu kama Ubongo Kids na zinginezo.
Kila mwanzilishi ana sababu za kuanzisha bidhaa au huduma. Hata hivyo, ni sababu gani hufanya vijana wengi kufanya shughuli za ujasiriamali wanazozifanya?
Mmoja kati ya wapiga picha maarufu nchini kutoka mradi wa kupiga picha wa K15 Photos, Emannuel Feruzi ameiambia Mashele, kuwa licha ya kusomea masuala ya programu za kompyuta, amependelea zaidi kupiga picha kiubunifu na kuifanya kazi hiyo kuchukua takriban asilimia 80 ya shughuli zake.
Sababu kuu ya Feruzi kuanza kupiga picha miaka minane iliyopita ni kupenda kupiga picha za mtoto wake na baadaye aliifanya kazi ya kupiga picha kama biashara rasmi.
“Nilipenda kupiga picha za mwanangu na hadi sasa uhandisi ni kazi ninayoifanya mara moja moja,” amesema Feruzi licha ya ukweli kuwa uhandisi ni miongoni mwa dili zinazolipa kwa waliofanikiwa kupata kazi au miradi ya kufanya.
Kinachomfanya Feruzi aendelee kuishi kwenye kazi yake licha ya kuwepo na ushindani mkubwa ni mapenzi alionayo juu ya kazi yake huku akieleza kuwa kama pesa zikikuangusha au timu yako ikikuangusha ni upendo juu ya kazi yako tu ndio utakaobaki kuiendesha kazi hiyo.
“Nimeanguka nikaamka mara nyingi tuna pengine ni zaidi ya mtu yeyote. Upendo juu ya kazi yangu ndiyo uliofanya niendelee kuifanya,” amesema.
Wengi hufikiri kuwa kuanzisha kampuni ni rahisi lakini kuna jambo nyuma ya kuipenda kazi unayoifanya licha ya kuwa kila anayeanzisha kitu huwa ana mapenzi nacho.

Mwasisi wa programu tumishi (Apps) zinazosaidia masuala ya elimu, “My elimu “ na “Mtabe” Given Edward (25) amesema msukumo juu ya mambo ya programu ulianza tangu akiwa mtoto na msukumo huo ulizidi kukua kadri alivyokua akiongeza miaka kwenye maisha yake.
Kwake yeye kufanikiwa kwa shughuli zake ni kwa sababu ya kupangilia vizuri timu yake kuweka sawa mpango kazi wake na zaidi kuwa na uhakika wa bidhaa yake.
Amesema wengi wanaoshindwa kuendeleza kampuni zao ni kwa sababu tofauti ikiwemo kushindwa kuelewa nini wanafanya.
Ufanye nini basi ukitaka kuanzisha kampuni yako au biashara?
Kwa watu wote waliofanikiwa katika biashara zao watakubali ya kwamba kuanzisha biashara ni zaidi ya mtaji na pia ni zaidi ya mapenzi ya kazi hiyo. Yafuatayo ni makusanyo ya maswali ya kuzingatia pale unapohitaji kuanzisha biashara yako.
Dhamira yako ni nini?
Kwa mujibu wa Lucy Odiwa (35), ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya “Women Choice” inayotengeneza taulo za kike (pedi) na hata za watoto ambazo zinaweza kutumika kwa zaidi ya miaka miwili, mafanikio ya kazi yake yamefuatia dhamira aliyokuwa nayo ya kuhakikisha mtoto wa kike hakosi masomo pale anapokuwa kwenye siku zake.
“Sababu ya period (hedhi), niliwahi singizia naumwa ili nisiingie darasani. Historia hiyo ilikua ni msukumo wa mimi kutafuta mbadala wa pedi za kutumia mara moja,” amesema Odiwa.