Sura ya 2: Mtindo wa kitaaluma
Utangulizi
Uzoefu wa kusoma makala za kitaaluma na kuhudhuria semina mbalimbali umeonyesha kuwa pamoja na maudhui mazuri ya makala hizi kumekuwa na ukiukaji wa kutosha wa taratibu za kimtindo ambazo zina nafasi muhimu sana katika maandiko na majadiliano yoyote ya kitaaluma. Ingawa mwandishi amekuwa akitoa madokezo ya hapa na pale katika semina hizi kuhusu kanuni za kimtindo na makosa yatokanayo na ukiukaji wa taratibu hizi, hata hivyo suala hili bado linahitaji kuchukuliwa kwa uzito wake kamili hasa kutokana na kuongezeka kwa dhima ya Kiswahili baada ya lugha hii kufanywa lugha ya taifa.
Matokeo ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa yamekuwa ni uimarishwaji zaidi wa lugha hii ikiwa ni pamoja na kuipenyeza katika matumizi ya kitaaluma. Masuala ya kitaaluma kwa kawaida hayawi ya nchi moja tu peke yake, bali huhusisha na kushirikisha mataifa mbalimbali. Hii ina maana kwamba tuandikapo makala au vitabu vyetu vya taaluma mbalimbali katika Kiswahili shaiti tuzingatie ukweli kwamba vitasomwa na jumuiya iliyo pana zaidi na sio ya Watanzania tu. Hivyo maandiko ya namna hii lazima yazingatie taratibu maalum za uandikaji ambazo hufuatwa na lugha zote za kimataifa na hata zisizo za kimataifa.
Lengo la sura hii ni kuzichambua sifa na taratibu zinazojitokeza katika mtindo wa maandiko na mazungumzo ya kitaaluma ili zitambuliwe kwa uwazi zaidi na ikiwezekana zitumiwe na wachunguzi na wataalam wa Kiswahili. Mwandishi atajitahidi kudondoa mifano ya sifa na taratibu hizi na ile ya ukiukwaji wake kutoka hasa katika makala za wachunguzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kulisogeza zaidi suala hili kwa wahusika wa ujenzi, ukuzaji na uimarishaji wa Kiswahili.
Mawasiliano ya Kitaaluma
Mtindo wa kitaaluma unatumiwa katika mawasiliano ya kitaaluma ambayo yanapatikana:
(i) katika vitabu vya kitaaluma kwa mfano vya sarufi, hisabati, jiografia, kemia, fizikia, kamusi na kadhalika,(ii) Katika majarida ya kitaaluma kwa mfano, KISWAHILI, MULIKA, LUGHA YETU na kadhalika,(iii) katika utayarishaji na utoaji wa mafunzo shuleni na vyuoni, kwa mfano utayarishaji na utoaji wa mihadhara,(iv) kwenye semina, warsha na makongamano ya kitaaluma,(v) katika kuandaa na kutoa ripoti mbalimbali za shughuli za kitaaluma, kama vile semina, makongamano, ripoti za utafiti,(vi) katika tasnifu na kazi nyinginezo zozote za kitaaluma.
Sifa za Mtindo wa Kitaaluma
Tunapozungumzia sifa za mtindo wa kitaaluma sharti tutofautishe aina mbili za sifa hizi:
1. sifa zisizo za kiisimu,
2. sifa za kiisimu.
Sifa Zisizo a Kiisimu
Hizi ni sifa ambazo ziko nje ya lugha na haziambatani moja kwa moja na lugha. Nazo ni pamoja na:
(i) Mada ya Kitaaluma
Ili mtindo wa kitaaluma utumike sharti pawepo mada ya kitaaluma, vinginevyo utatokea ukiukaji wa taratibu za kimtindo.
(ii) Usahihi na Ukweli wa Mambo Yanayojadiliwa
Katika taaluma inategemewa kwamba mambo yanayojadiliwa yawe ya ukweli mtupu na sio uzushi au uongo. Ingawa jambo hili si rahisi kutekelezwa kila mara, lakini ndilo lengo linalotafutwa katika taaluma.
(iii) Kuwepo kwa Mantiki katika lambo Linalojadiliwa
Maelezo yoyote ya kitaaluma hayafanywi kiholela, bali hufuata mtiririko maalum unaoleta maana kamilifu. Kwa mfano, iwapo inkemia anatoa taarifa yake kuhusu jaribio alilolifanya katika maabara basi taarifa hiyo sharti iwe katika mtiririko maalum wa matukio, mathalani: nia na umuhunu wa jaribio, matayarisho ya jaribio, jaribio lenyewe, matukio yaliyoonekana na sababu zake, mahitimisho yaliyofikiwa.
Ingawa makala nyingi za wataalam wa Kiswahili zimefaulu kuonyesha mantiki katika mtiririko wa uchambuzi wa masuala mbalimbali bado iko mifano michache ya makala ambazo zinaweza kutiliwa wasiwasi kwamba hazijatimiza vema sharti hili. Hebu tuangalie, kwa mfano, makala moja iliyokuwa na kichwa cha habari kifuatacho: “Ukusanyaji wa data ya leksikografia na matatizo yatokanayo: Mifano kutoka lugha ya Kiswahili”. Uchambuzi wa mada hii ulifanywa katika vipengele vilivyofuata mtiririko ufuatao:
1.0.0 Utangulizi.
1.1.1 Maana ya leksikografia.
1.2.0 Historia ya leksikografia.
1.2.1 Leksikografia katika ulimwengu.
1.2.2 Leksikografia katika Tanzania na Afrika Mashariki.
2.0.0 Ukusanyaji wa data.
2.1.0 Data ya leksikografia (n.k.);.
Kwa maoni yetu vipengele 1.2.0 hadi 1.2.2 kwa hali yoyote havihusiani sana na mada iliyotazamiwa kuchambuliwa na kwa hiyo kuwepo kwake hapa kunaelekea kuupa dosari mtiririko mzuri wa mawazo katika makala hiyo.
(iv) Uendeshaji wa Mjadala Bila Kuonyesha Waziwazi Mno Upendeleo wa Mwandishi
Katika taaluma tunatarajia mtaalam ajihusishe na taaluma tu kama ilivyo, bila kuonyesha upendeleo mkubwa wa upande fulani wa hoja yake. Lakini ukweli umedhihirika kuwa upendeleo hauwezi kukosekana kabisa. Kinachotakiwa kusisitizwa hapa ni kwamba katika taaluma upendeleo wa namna hii usizidi mno.
(v) Ujumlisho wa Mambo yanayojadiliwa
Mijadata ya kitaaluma ina mwelekeo wa kuchambua mambo katika ujumla wake na sio kutenga kila kipengele peke yake. Kwa mfano, katika biolojia tunaposema kuwa “fundo (node) ni sehemu ya shina ambapo ndipo majani yanapochipukia” (Mswada wa Biolojia 1981) tuna maana ya mjumlisho wa mashina yote na majani ya aina zote na sio shina maalum pekee na majani yake tu.
Sifa hizi zisizo za kiisimu zina ufungamano wa namna fulani na sifa za kiisimu kwani ndizo zinazoathiri uchaguzi na matumizi ya zana za kiisimu za mtindo wa kitaaluma.
Sifa za Kiisimu
Hizi zmaambatana na higha yenyewe na hujitokeza katika msamiati, sarufi maumbo, fonetiki na miuhdo ya sentensi inayotumika katika mtindo huu wa kitaaluma.
Msamiati
Msamiati unaotumiwa katika mtindo wa kitaaluma una sifa kadha za kipekee ambazo hujitokeza waziwazi. Sifa hizo ni pamoja na:
(i) Matumizi Makubwa ya Istilahi
Ili kuleta usahihi wa mambo mawasiliano ya kitaaluma hutumia zaidi msamiati maalum - yaani istilahi za kisayansi. Kwa mfano:
Silabi ya kawaida katika lugha ya Kiswahili na Kibantu kwa jumla ni KI (Konsonanti - Irabu). Hivyo kwa kawaida neno haliwezi kuishia nakonsonanti, isipokuwa m na s na wala neno haliwezi kuanza namkururo wa konsonanti isipokuwakonsonanti zinazofuatwa na nusu-irabu w au y.
Tena yaonekana kwamba idadi kubwa ya msamiati huu maalum ni maneno yaliyokopwa (yaliyoazimwa) toka lugha za kigeni. Matumizi ya maneno haya yanaimarisha usahihi wa maelezo yanayolengwa kwa sababu kubwa mbili:
1. Maneno haya hayaongezewi maana nyingine za ziada na watumiaji wa Kiswahili kwa kuwa hayakuambatana na utamaduni wao na, kwa hali hii yanatumiwa kwa maana moja tu.2. Mengi ya maneno haya ni ya kimataifa na hivyo yanarahisisha mawasiliaho kati ya wanataaluma kutoka nchi mbalimbali zinazotumia lugha tofauti. Kusema kweli utumiaji wa istilahi za kimataifa katika mawanda ya kitaaluma unachukuliwa na wanaisimu wengi kuwa ni jambo la maendeleo katika lugha. Kwa mfano katika nyanja za fonolojia istilahi zifuatazo za kimataifa zinatumika katika Kiswahili: fonolojia, fonimu, foni, alofoni, mofimu, alfabeti, homografu, toni na kdhalika.
(ii) Matumizi ya Maneno Katika Maana Moja tu
Maneno yanayotumika kwenye mtindo wa kitaaluma kwa kawaida hutumiwa katika maana moja tu (na mara chache sana katika maana mbili). Kwa hiyo endapo neno fulani lina maana nyingi basi ni maana moja tu ndiyo inayoweza kukubalika katika matumizi ya majadiliano ya kitaaluma. Kwa mfano neno “maji” lina maana kadha katika Kiswahili:
1. Maji ya kawaida ya kunywa, kupikia n.k. ambayo yamefasiriwa katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu(1981:149) kama “Kitu kiowevu kisicho na rangi, ladha wala harufu, ambacho ni mchanganyiko wa hewa aina ya oksijeni na haidrojeni na hugeuka mvuke wakati kikipata joto na kuwa barafu wakati kikipoa sana, huonekana kwenye bahari, mito, chemchemi n.k.”.2. Pombe, k.m. Jumapili tuliyakatamaji barabara huko Safari Resort.3. Hali ya kulewa, k.m. Sikuweza kuzungumza lolote la maana na Juma kwani nilimkuta yuko majikabisa.4. Hali ya kuwa na hamu sana ya kitu (jambo) fulani lakini usikipate katika ukamilifu wake. Kwa mfano katika methali: Mkania majihayanywi.
Kati ya maana zote hizi ni ile maana ya kwanza tu ndiyo inaweza kutumika katika mtindo wa kitaaluma.
(iii) Matumizi ya Maneno Katika Maana Pana na za Ujumla
Maneno mengi katika mtindo wa kitaaluma hutumika kwa maana pana na za ujumla. Kwa mfano katika fasiri:
Msuli ni mkusanyiko wa tishuzinazotanuka na kurudi, hivyo huleta mwendo katika sehemu zamwili, (Mswada wa Biolojia 1981).
Maneno “msuli”, “tishu”, na “mwili” yana mana ya msuli kwa ujumla, tishu kwa ujumla, mwili kwa ujumla, na sio msuli maalum kabisa wa mtu, mnyama, ndege au mdudu tunayemfahamu, na kadhalika.
(iv) Kurudiwarudiwa kwa Msamiati na Istilahi
Hali ya kurudiwarudiwa kwa msamiati na istilahi zilezile hujitOkeza saha katika mawasiliano ya kitaaluma. Kwa maneno mengine ukubwa wa matini (habari inayoandikwa) unaongezeka sio tu kwa kujitokeza maneno mapya bali kwa kurudiarudia maneno yaliyokwishatumika tayari. Kwa mfano:
Lugha ni kitu kilichojengwa au kutengenezwa kwa vitamkwa vingi. Ni “sauti za nasibu”, maana yakesauti zilizozuka tu kwa bahati, bila ya uamuzi wa kikao maalum chawatu wakajadiliana na kuamua wawe na sauti hizi au zile wanapozungumza. Hata hivyb watuwameapokea sauti hizo, wanajifunza, na wamekubaliana kuzitumia katika mazungumzo yao.
Sarufi Maumbo
(i) Matumizi Mapana ya Wakati Uliopo wa Kudumu
Idadi kubwa ya vitenzi vinavyotumika katika maandiko ya kitaaluma huwa katikawakati uliopo wa kudumu. Kwa mfano:
1. “Vokali (o) nyepesi hutamkwa kwa kuinua kidogo sehemu ya nyuma ya ulimi huku midomo imewekwa mviringo”.2. Jua huchomoza asubuhi nahuzama (huchwa) jioni.
Katika lugha ya Kirusi, kwa mfano, imethibitishwa kuwa kwenye mtindo wa kitaaluma idadi ya vitenzi vinavyotumika katika wakati uliopo ni kubwa mara tatu zaidi ya vitenzi katika wakati uliopita. Wakati uliopo wa kudumu una dhana ya kuonyesha kwamba jambo linalojadiliwa limethibitisbwa (kisayansi) kuwa lipo, ni la kweli na litaendelea kudumu.
(ii) Matumizi ya Wakati Uliopita
Aidha vitenzi katika wakati uliopita hutumika kwa kiasi cha kutosha. Kwa mfano:
Ukweli ni kwamba majadiliano kuhusu maandishi ya Kiswahiliyalianza tangu Kiswahili kianze kusanifishwa wakati Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilipoundwa mwaka 1930.
(iii) Matumizi Maalum ya Wakati Uliopo
Matumizi ya wakati uliopo huwa ya aina yake. Kwa kawaida wakati uliopo huwa na maana ya wakati uliopita. Kwa mfano:
Nkwera (1978:XI) anaeleza kuwa lengo la kitabu chake ni kuwasaidia wazalendo wanaojiandaa kwa mitihani ya Kiswahili ya kiwango cha kidato cha IV na VI na wala sio kitabu cha kujifunzia Kiswahili kwa wageni wa lugha hii.
(iv) Matumizi Mapana ya Nafsi ya Tatu
Kuhusu matumizi ya nafsi katika mtindo wa kitaaluma imeonekana kuwa nafsi ya tatu ndiyo inayotumika zaidi hapa. Kwa mfano:
Fasihi imelinganishwa na kiookinachoonyesha maisha ya jamii; pia mwonzi wa jua unaomulikajamii iendavyo na iendako kwa nyakati mbalimbali.
(v) Matumia ya Nafsi ya Kwanza - Wingi
Vilevile mtindo wa kitaaluma hutumia sana nafsi ya kwanza - wingi. Kwa mfano:
Katika makala hii tunakusudiakukiangalia kipengele hicho kwa uangalifu zaidi. Tunatarajia kutoa vidokezo muhimu ambavyo vyaweza kuwasaidia wachungnzi kufanya uchunguzi uliokanulika. Hivyo basi hatutarajii (kwa makala hii) kukamilisha vipengele vyote vinavyohusu suala hili. Shabaha yetu kubwa ni kuonyesha vigezo ambavyo vyaweza kutumika katika kuzingatia suala la lafudhi ya Kiswahili.
Utumiaji wa nafsi ya tatu na nafsi ya kwanza-wingi unapendelewa zaidi katika mtindo wa kitaaluma kwa sababu unaficha hali ya “ubinafsi” wa mwandishi. Hali hii inapunguza upendeleo wa mwandishi na kuufanya mjadala wa kitaaluma uonekane bayana. (Kadhalika ingefaa tudokeze kuwa taratibu hizi za nafsi hutumika zaidi katika maandiko ya kitaaluma kuliko hali inavyokuwa wakati wa mazungumzo au majadiliano ya ana kwa ana).
Kwa hali hii matumizi ya nafsi ya kwanza-umoja katika makala za kitaaluma kama vile:
1. “Jambo la pili ambalo nimejaribukulizingatiakatikamakala haya ni kwamba utafiti wa kushiriki na kushirikisha ni mbinu ya kutafuta ukweli”,2. “Najaribu kutazama viambishi vilivyotumiwa katika istilahi za sayansi na kutoa mapendekezo machache yawezayo kuwasaidia wanasayansi wenzetu wanapounda istilahi. Marejeo yaliyotumiwa na eneo la uwanda vimewekewa mpaka. Tegemeo langu ni kwamba tukichambua zaidi viambishi vichache tutapata faida kubwa zaidi,3. Viungo nomino hivi nilivyovitajahufanya kazi ya kiarifu katika tungo.
yanaleta mkwaruzo wa hali fulani yanaposikika na hasa kusomwa katika mijadala ya kitaaluma.
(vi) Kutotumiwa kwa Nafsi ya Pili
Mintarafu nafsi ya pili, kwa kawaida haitumiki katika mtindo wa kitaaluma, hasa katika maandiko. [Labda kwa nadra nafsi hii ya pili inaweza kutumika wakati wa mazungumzo (ya kitaalamu) baina ya wataalam wawili, mmoja akiuliza ama akijadili maoni ya mwenzake].
(vii) Matumizi ya Viambishi na Vipashio Maalum
Kuna viambishi na vipashio kadha ambavyo aghalabu hujitokeza sana katika mtindo wa kitaaluma kwa sababu vinatumika kuundia istilahi za kisayansi. Na istilahi hizi hutumiwa sana katika taaluma. Kwa mfano:
“-ia”
|
kwa maana ya “taaluma ya” k.m. fonolojia, biolojia, ekolojia, n.k.
|
“m-”
|
kwa maana ya “mtaalam wa” k.m. mchumi, mkemia, mganga, mfizikia n.k.
|
“mwana-”
|
kwa maana ya “mtaalam wa” k.m. mwanafonolojia, mwanakamusi, mwanasarufi, mwanaisimu n.k.
|
Mifano ya viambishi vingine ambavyo vimependekezwa katika Mswada wa Biolojia (1981) ni:
-fite (mesofite),
-fita (gamefita),
-fiti (sporofiti),
epi- (epiglotisi), n.k.
Fonetiki na Ortografia
(i) Tahijia na Matamshi Kufuata Taratibu za Sarufi
Kwa kawaida tahijia na matamshi ya maneno mengi (isipokuwa istilahi ndefu zinazojumlisha maneno kadha kwa mfano D.D.T., P.P.F.) yanayotumika katika mtindo wa kitaaluma hufuata taratibu na kanuni za sarufi. Kwa mfano hatuandiki, mathalani katika majibu ya mtihani kuwa kiongozi wa kijeshi wa Ghana niJ.J. badala ya Jerry Rawlings (angaliaDaily News, 22 Januari, 1982:2) au mji mkuu wa Tanzania ni Dar. Hata hivyo vifupisho vya baadhi ya mashirika ya kimataifa k.m. UNESCO, OPEC na vyama vya kisiasa k.m. FRELIMO, PLO, MPLA n.k. yaonekana vimezoeleka kutumika bila kubadilishwa katika lugha nyingi. Hali kadhalika haitakuwa sahihi kutumia lafudhi ya “Pwagu na Pwaguzi”, kwa mfano, wakati wa mhadhara kwenye thieta (darasani) au wakati wa semina. Mazingira haya ya kitaaluma yanahitaji lafudhi sanifu.
Miundo ya Sentensi
Matumizi ya Sentensi Changamano za Kiima na Kiarifu
Sentensi nyingi zinazotumika katika mtindo wa kitaaluma huwa changamano na zina kiiina na kiarifu (prediketa) vinavyojipambanusha waziwazi kabisa. Kwa mfano:
“Makala hii imezingatia kipengele cha lafudhi katika viwango vinne”
| |
kiima
|
kiarifu
|
(ii) Matumizi ya Tungo za Kauli ya Kutendwa
Aghalabu hutumika sentensi za kauli ya kutendwa. Kwa mfano:
Kwa vile katika mifano hii ving'ong'o vimetenganishwa na konsonanti mdomo ifuatayo kwa mpaka wa kimofimu, itabidi tuiangalie mifuatano hii kama fonimu mbili pekee.
(iii) Matumizi ya Nafsi ya Mtendaji Isiyosisitizwa
Aidha kuna matumizi mapana ya sentensi ambazo ingawa zinaonyesha nafsi ya mtendaji, lakini mtendaji huyu hapatiwi uzito anaostahili (hatiliwi maanani sana). Badala yake kinachotiliwa maanani zaidi ni tendo lenyewe lililofanyika. Kwa mfano:
Ilidhihirika kuwa istilahi zilizopo ni chache sana hivyo hazitoshi kutafsiri dhana za kifonolojia zilizo katika sayansi hiyo; pili ilidhihirikakuwa kuna istilahi tete nyingi ambazo hutumiwa kuwakilisha dhana moja, ...
Hapa jambo muhimu ambalo linatiliwa mkazo ni kwamba “ilidhihirika”. Suala la nani aliyedhihirisha hivyo hatulitilii maanani sana, linachukua nafasi ya pili katika mawazo yetu, na sio nafasi ya kwanza.
(iv) Matumizi Mapana ya Viungo (vya Sentensi)
Ili kuleta mtiririko mzuri wa mawazo yenye mantiki tungo katika mtindo wa kitaaluma hutumia viungo maalum, kwa mfano:
pamoja na hayo,
zaidi ya hapo,
kwa hali hii,
hivyo; kwa hiyo,
hii ina maana kwamba,
kufuatana/kulingana na,
aidha, vilevile, hali kadhalika, vivyo hivyo,
kama tulivyosema,
hebu sasa tuangalie,
kwa upande mwingine, na kadhalika.
(v) Matumizi Mapana ya Sentensi za Taarifa
Kwa kawaida katika mtindo wa kitaaluma sentensi zinazotumika kwa wingi ni zile zinazotoa taarifa. Sentensi za swali hutumika kwa nadra sana na aghalabu huwa zina lengo la kumfanya msomaji atilie maanani jambo fulani au ajitayarishe kwa wazo linalofuata.
Mambo Mengine ya Kuangalia Katika Mtindo wa Kitaaluma
(i) Jinsi ya Kuandika Warejewa na Kunukuu Marejeo
Kuna taratibu maalum za kuyaandika majina ya wataalam wanaorejewa pamoja na maandishi yao.
Ndani ya makala/kitabu mara nyingi utaratibu huu hufuatwa: Bloomafield (1933:5) au (Lyons 1977:678) - yaani linatajwajina la mtaalam (bila vyeo au daraja zake), mwaka alioandika kitabu au makala yake na, ikiwezekana ukurusa uliorejewa. Kwa mfano:
1. Mathalan, mwanaisimu wa Kimarekani Bloomfield (1933:5)anakumbusha kuwa...2. La muhimu kupita yote ni kuwa, baadhi ya lugha huwa hazina vijiumbo vinavyoonyesha nyakati katika tendo. (Lyons 1977:678).
(Iwapo linarejewa gazeti au jarida basi huandikwa kwa mfano (Mambo Leo 20 Januari 1940:5) au Kiswahili, Toleo 37/2, Septemba 1967).
Kwa kulingana na hoja hii kuandika majina ya wataalam waliorejewa kwa kuambatisha sifa, vyeo ama daraja zao kama vile:
1. Ama kwa hakika tumechochewa na fikra zilizotolewa na wanaisimu wa Kiswahili walioandika juu ya mada hii. Baadhi yao ni SheikhMohamed Ali (1976);2. Uzoefu umeonyesha kwamba mambo haya mawili hayaji kwa njozi, sala, nia njema au kutegemea fadhila na zawadi kutoka kwa mataifa makubwa ya kibepari (Othman 1982) ila kutokana na uongozi sahihi unaomilikiwa na tabaka la wafanyakazi wenyewe, kama alivyoeleza Ndugu Sokoine (1976) katika utangulizi wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano,...,3. Amesema Mzee Broomfield katika Sarufi ya Kiswahili kuwa sarufi ya lugha ya watu hutengenezwa na watu wenye lugha yao tu;4. Profesa W.H. WHITELEY ametabiri kuwa kuongezeka kwa maneno mapya katika ngeli ya III na ya V katika Kiswahili kutaifanya lugha hiyo ibadilishe muundo wake na kuwa na upatanisho hafifu wa kisarufi;
hakurandani na utaratibu maalum ambao ungefaa ufuatwe. Hali kadhalika kudondoa warejewa kwa namna hii: Nkwera (1978:dibaji) badala ya ukurasa halisi wa dibaji hiyo au (L. Hyman, 1975 uk. 105) kunakengeua urari uliokusudiwa kuwepo katika kuandika marejeo ya kitaaluma.
Baada ya makala (ama kitabu) kuisha ndipo orodba kamili ya marejeo hutolewa kwa kufuata utaratibu huu: jina la mwandishi (majina hufuata alfabeti), mwaka kilipoandikwa kitabu au makala, jina la kitabu au makala, shirika lililochapisha na mahali lilipo. Yawezekana pia kutaja kwanza mahali lilipo shirika la uchapishaji kabla ya kulitaja shirika lenyewe. (Hata hivyo utaratibu huu haufuatwi na majina, mathalani ya utamaduni wa Kichina, Kikorea, Kivietnam na nchi nyingine za Mashariki ya Mbali. Katika utamaduni wa nchi hizi majina yote hutajwa kwenye marejeo, k.m. Mao Tse Tung, Li Pei n.k.). Mwaka unaweza kuwa katika mabano au bila mabano. Majina ya vitabu na majarida hupigiwa msitari chini ambapo makala huwekewa vifungua na vifunga semi. Kwa mfano:
1. Abdalla, A. (1973) Sauti ya Dhiki,Oxford University Press, Nairobi, Dar es Salaam, Lusaka, Addis Ababa.2. Bloomfield, L. 1933 Language,George Allen and Unwin Ltd., Museum Street, London.3. Mkude, D.J. (1980) “Umuhimu wa Kiimbo katika Sanifi”. Makala iliyosomwa kwenye Semina ya mabadiliko ya mfumo wa lugha ya Kiswahili, Iringa, Septemba 1980.
Kukiuka utaratibu huu wa kuorodhesha marejeo kwa kiasi fulani kunapunguza ubora wa maandiko ya kitaaluma ingawa hakuathiri kwa vyovyote maudhui ya maandiko yenyewe.
(ii) Kuangalia Usahihi wa Msamiati na Istilahi Zinazotumika
Kwa kuwa taaluma inasisitiza sana juu ya usahihi wa mambo, katiku mtindo wa kitaaluma sharti kuwepo na uangalifu mkubwa wa usahihi wa msamiati na istilahi zinazotumika, kwani bila hivyo dhana inayokusudiwa katika mjadala inaweza kupotolewa. Mathalani matumizi ya maneno “Wazalendo” na “Mazingara” katika mifano ifuatayo yanapotoa dhana iliyokusudiwa na kwa hivyo kupunguza ubora wa maandiko kwa kiasi fulani:
1. Sarufi na Fasihi ni muhtasari wa m.iarnlalio ya somo la Kiswahili kwa kidato I - VI shule za sekondari na vyuo.... Aidha yatarajiwa kuwasaidia wazalendowanuojiandaa kwa mitihani ya Kiswahili ya kiwango cha kidato cha IV na VI”2. Kapinga (1977), Yahya-Othman (1976), Nkwera (1978) na Mkude (1980) pia ni miongoni mwa wanaisimu wazalendo waliowahi kufanya uchamhuzi juu ya tungo za Kiswahili.
Mzalendo ni “mtu anayependa nchi yake na yuko tayari kuifia” (Kamusi ya Kiswahili Sanifu 1981:206) na si lazima kuwa watahiniwa wote na hao wanaisimu waliotajwa wawe wazalendo. Na je, kama mwanafunzi si mzalendo ina maana hataruhusiwa kukitumia kitabu cha Sarufi na Fasilhi?Kusema kweli katika masuala ya kitaaluma hatujali sana utaifa wa mtu isipokuwa utaalam wake tu na mchango wake katika kukuza na kuendeleza taaluma kwa ujumla. Ubaguzi katika taaluma haupendelewi.
Inapendekezwa kuwa uchunguzi utanyike katika mazingara ya lugha hiyo ili kumpa mchunguzwa nafasi ya kujibu maswali katikamazingara yake mwenyewe.
Bila shaka mwandishi wa makala hapa alitaka kuelezea juu ya “mazingira”, kwani mazingara ni mamho ya ujanja fulani unaohusiana na uchawi.
(iii) Matumizi ya Lugha Safi ya Kiswahili
Lazima kuwepo na jitihada kubwa ya kutumia lugha safi ya Kiswahili bila kuichanganya mara kwa mara na lugha za kigeni. Matumizi ya “i.e.” na “e.g.” katika maandiko ya kitaaluma kama vile:
1. “Katika kuchunguza sauti, inapendekezwa kuwa mchunguzi atayarishe orodha ya maneno katika lugha inayoeleweka kwa mchunguzi na mchunguzwa (i.e.Kiswahili, na pengine Kiingereza, iwapo lugha ya jamii fulani inachunguzwa)”:2. “Wachunguzwa hawana budi wawe na sifa zifuatazo': (IV) Wasiwc na matatizo yoyote katika matumizi yao ya lugha (e.g. kigugumizi, kithembe na kadhalika)”;
hayaleti sura nzuri katika ujenzi wa Kiswahili cha taaluma.
(iv) Kutotumia Sana Tasfida, Nahau, Mafumbo na Misimu
Kwa kawaida katika mtindo wa kitaaluma hazitumiwi sana tasfida, nahau, mafumbo na misimu kwa sababu kwa kufanya hivyo taarifa inayokusudiwa inafikiwa na kueleweka mara moja.
Sifa Hasi za Mtindo wa Kitaaluma
Kutokana na mengi yaliyojadiliwa hapo nyuma imedhihirika kuwa kuna sifa kadha ambazo ni hasi katika mtindo huu. Sifa hizo ni:
1. kawaida ya kutotumika (sana) kwa nafsi ya pili,2. kawaida ya kutotumika kwa sentensi za mkato,3. matumizi rtiachache sana ya tasfida, nahau, mafumbo, methali na misimu,4. matumizi finyu ya lugha mguso (lugha hisishi) - yaani ile lugha inayogusa hisia za mtu na kujaribu kuathiri maoni yake kuhusu kitu au jambo linalojadiliwa.
Suala la Lugha Mguso Katika Mtindo wa Kitaaluma
Kuna hali ya uvutano baina ya wanaelimumitindo kuhusu kutumika au kutotumika kwa lugha mguso katika mawasiliano ya kitaaluma. Baadhi yao wanadhani kuwa mguso wa lugha haujitokezi sana katika mtindo huu kwa sababu lengo kubwa katika taaluma ni usahihi na ukweli tu wa mambo yanayojadiliwa. Nia ya mtaalam hapa sio kusisimua au kuibua hisia na maono ya wale wanaomsoma au kumsikiliza, bali kutoa taarifa tu kama ilivyo. Wengine wana maoni kwamba, pamoja na kutoa tu hiyo taarifa ya kitaalam, mtaalam yafaa vile vile atumie kwa kiwango fulani lugha mguso ili kuwavutia wasomaji na wasikilizaji wake katika hayo anayoyajadili.
Upekuzi wetu wa vitabu na makala nyingi za kitaaluma umeonyesha kuwa lugha mguso haitumiki sana katika maandiko haya, lakini lugha hii haiwezi kukwepeka kabisa katika maandiko ya kitaaluma. Na hapo inapotumika inaelekea kuwa na mvuto wenye nguvu. Tuangalieni mifano hii:
1. Katika majadiliano haya imedhihirika bayana kuwa, pana umuhimu wa kuwepo juhudi za makusudi kusanifisha lafudhi ya Kiswahili. Kushindwa kukamilisha kazi hiyo muhimu ni kama kumvalisha mtoto shati bila kaptura.2. Katika sentensi hizi mbili, tena fupi, mwandishi ameeleza mengi kuhusu maisha ya mtu katika mafunzo ya kijeshi. Anaeleza harakati za jeshi katika kuvua na kuviza ugoigoi na kiburi na ubishi.Harakati za kumvisha mtu joho la utii kwanza.
Kwa hali hii tunaweza kusema kuwa lugha mguso inafaa wakati fulani kupenyezwa katika mijadala ya kitaaluma hasa mijadala hiyo ikiwa ni ya malumbano ama ile inayohusu mada ambazo ni mpya kabisa katika mawanda mbalimbali ya sayansi. Majadiliano ya namna hii yanahitaji mvuto wa hali fulani kwa wasomaji ambao unalazimisha kutumia lugha iliyo tajiri kabisa kwa miguso, maono na mbinu nyingine za kupamba lugha.
Hitimisho
Sura hii imechambua sifa na taratibu maalum za mtindo wa maandiko na mazungumzo ya kitaaluma. Sifa na taratibu hizi pamoja na kukiukwa kwake zimeonyeshwa kwa kudondoa mifano hai kutoka katika maandishi kadha ya wataalam wa Kitanzania, hasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Madondoo haya hayakunukuliwa kwa nia mbaya. Yamenukuliwa ili kuonyesha hali halisi ya uandishi wa makala za kitaaluma katika Kiswahili ilivyo
Massheleblog