
Muonekano wa ukurasa wa Facebook App ambao unatoa sababu za kwanini mtumiaji anapokea matangazo kwenye ukurasa wake.Picha|Mtandao.
- Sasa kuwawezesha watumiaji wake kufahamu kwanini matangaza ya biashara au habari zinawafikia katika kurasa zao.
- Hayo ni miongoni mwa maboresho yanayofanywa na Facebook ili kuwarahisishia watumiaji wake upatikanaji wa huduma bora zinazokidhi mahitaji yao.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inasogeza huduma zake karibu na watumiaji, mtandao wa Facebook umefanya maboresho katika programu yake tumishi (Facebook App) ambapo mtumiaji ataweza kupata sababu zinazoeleza kwanini tangazo au habari imewekwa kwenye ukurasa wake.
Hatua hiyo huenda ikatatua changamoto ya watumiaji wa mtandao huo kupata matangazo bila ridhaa yao au bila kujua sababu za tangazo husika kuwekwa kwenye ukurasa.
Maboresho hayo yanajikita katika mambo mawili ya "Kwa nini ninaona chapisho hili?"( Why am I seeing this post?) na "Kwa nini ninaona tangazo hili?" (Why am I seeing this ad). Ikiwa na maana kuwa yanashughulikia kuchambua aina ya matangazo na habari zinazoingia kwenye ukurasa wa watumiaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja wa bidhaa wa matandao huo, Ramya Sethuraman inaeleza kuwa wamezindua "Kwa nini ninaona chapisho hili?"( Why am I seeing this post?) ili kuwasaidia kurasa za watumiaji wa mtandao huo kudhibiti kwa urahisi habari kutoka kwenye kurasa za marafiki au makundi ya mtandao huo.
Akizungumzia maboresho ya "Kwa nini ninaona tangazo hili?" (Why am I seeing this ad) amesema ni zana iliyozinduliwa mwaka 2014 ambapo imeboreshwa baada ya kupokea maoni kutoka kwa watumiaji wao kuhusu usumbufu wa matangazo wanaoupata katika kurasa zao.
Kwa maboresho hayo, mtumiaji atajua kwa undani kuhusu matangazo ya kibiashara yanayokuja katika ukurasa wake na kama hajaridhishwa anaweza kuchukua hatua muhimu ikiwemo kudhibiti matangazo yasitokee tena katika ukurasa wake.
Ili kupata huduma hiyo mtumiaji wa App hiyo atalazimika kwenda sehemu ya kulia ya ukurasa wake ambayo matangazo na habari kutoka makundi mbalimbali huwekwa na atajulishwa sababu za kila tangazo analiona.
Kati hatua nyingine, Facebook yenye watumiaji zaidi ya 1.5 bilioni imeeleza kuwa inataka kuona watumiaji wake wanakuwa huru wakati wakitumia mtandao huo na kama misingi ya uendeshaji itakuwa imekiukwa wanaweza kuchukua hatua.