Monday

SIFA ZA KONSONANTI, UZIADA KANUNI ZA KIUSILIMISHO NA ZISIZO ZA KIUSILIMISHO

0 comments
SIFA KUU ZA KONSONANTI
Sifa hizi zinazingatia mambo makuu matatu
1.      Jinsi konsonanti zinzvyotamkwa
2.      Mahali ambapo konsonanti hutamkiwa
3.      Hali ya nyuzi sauti
SIFA ZA JINSI YA MATAMSHI
Katika sifa hii konsonanti hugawika katika makundi sita
A.    VIPASUO/VIZUIWA
Wakati wa utamkaji wa konsonanti hizi huwa kuna mzuio wa mkondohewa na kuachiwa ghafula. Konsonanti hizi zimepewa jina hilo kutokana na kwamba katioka kuachiwa ghafla kwa mkondohewa sauti itokeayo huwa kidogo kama ina mlio wa kupasua. Kwa mfano konsonanti /p/, /b/, /t/, /d/, /k/ na /g/.
/p/  kipasuo sighuna cha midomo
/b/ kipasuo ghuna cha midomo
/t/ kipasuo sighuna cha ufizi
/d/ kipasuo ghuna chaa ufizi
/k/ kipasuo sighuna cha kaakaa laini
/g/ kipasuo ghuna cha kaakaa laini
B.     VIZUIO/VIPASUO KWAMIZA
Konsonanti hizi zinapotamkwa hewa husukumwa nje kwa nguvu na kuzuiwa halafu nafasi ndogo huachwa ili hewa ipite ikiwa na mkwaruzo. Kwa mfano, /č/ na ŧ/
C.     VIKWAMIZI
Katika utoaji wa sauti hizi mkondohewa unazuiliwa nusu tu, na hivyo hewa           inapita kwa kujisukuma kupitia katika nafasi au uwazi mdogo uliopo, na hivyo          kusababisha kukwamakwama. Kwa mfano, /f/, /v/, /ө/, /ð/, /s/, /z/,  na /š/.
D.    NAZALI
Ni aina ya konsonanti ambazo hutamkwa kwa kukishusha kimio kwa namna ambayo kiasi kikubwa cha hewa kutoka mapafuni huelekezwa kupitia kwenye chemba cha pua. Kwa mfano, /n/, /m/, /ŋ/ n.k.
E.     VITAMBAZA
Hutamkwa kwa hewa kusukumwa nje na kuzuiwa halafu kuruhusiwa kupita pembeni mwa kizuizi bila mkwaruzo mkubwa sana. Kwa mfano, /l/.


F.     VIMADENDE
Hutamkwa ncha ya ulimi ikiwa imeugusa ufizi lakini kutokana na nguvu ya hewa inayopita kati ya ncha ya hiyo na ufizi ncha ya ulimi hupigapiga kwa harakaharaka kwenye ufizi. Kwa mfano, /r/.
SIFA ZA KONSONANTI ZA MAHALI PA MATAMSHI
Sifa hii inahusu sehemu mbalimbali za chemba ya kinywa ambapo alasogezi na altuli hugusana au hukaribiana katika utamkaji  wa sauti tofautitofauti za lugha. Kuna sifa saba za mahali pa matamshi:
SAUTI ZA  MIDOMO
Wakati wa kutamka sauti hizi midomo huwekwa pamoja. Kwa mfano, /p/, /b/ na /m/
SAUTI ZA MDOMO-MENO
Wakati wa kutamka sauti hizi mdomo na meno ya juu hugusana. Kwa mfano, /f/, na /v/.
3. SAUTI ZA MENO
Wakati wa kutamka sauti hizi ncha ya ulimi hugusana na meno ya juu. Mfano wa sauti hizi ni kama vile /ө/,  / ð,
4. SAUTI ZA UFIZI
Sauti hizi zinapotolewa ncha ya ulimi hugusana na ufizi. Mfano wa sauti hizi ni /t/, /d/, /n/, /s/, /z/, /l/, na /r/
5. SAUTI ZA KAAKAA GUMU
Sauti hizi hutolewa wakati sehemu ya nyuma ya ulimi inapogusana na kaakaa gumu. Kwa mfano /č/, /š/, /ј/, n.k.

6. SAUTI ZA KAAKAA LAINI
Sauti hizi hutolewa wakati sehemu ya nyuma ya ulimi inapogusana na kaakaa laini. Kwa mfano /k/, na /g/.
7. SAUTI ZA GLOTA
Sauti hizi hutokea wakatii nyuzi sauti zinapokutanishwa kwa muda mfupi. Katika lugha sauti hizi ni chache sana. Kwa mfano /h/.
HALI YA NYUZI SAUTI.
Katika kongomeo kuna nyuzi-sauti ambazo zinakuwa katika nafasi za aina mbili wakati hewa inapopita. Ikiwa nyuzi-sauti ziko pamoja yaani zimekaribiana au kusogeana karibu hewa inapotoka kwenye mapafu huzisukuma na kuzitenganisha wakati wa kupia, na hivyo kusababisha msukumo. Sauti zinazotolewa wakati huu zinakuwa na mghuno na huitwa sauti ghuna. Ikiwa nyuzi-sauti hizi zimeachana, hewa hupita kwa urahisi bila kuzuiliwa, na hivyo bila kusababisha msukumo. Sauti zinazotolewa wakati huu huwa hazina mghuno, na huitwa sighuna.
SIFA BAINIFU/ SIFA PAMBANUZI
Sifa katika isimu ni vitu au mambo ambayo yanakibainisha kipengele chochote cha kisarufi au cha kiisimu (Massamba 2004:80).
Sifa bainifu ni nduni zitumikazo kutofautisha kipashio kimoja cha isimu na kipashio kingine cha aina yake. Katika kubainisha vipashio mbalimbali kuna vigezo viwili:
A.    KIGEZO CHA KIFONETIKI
Kigezo hiki huangalia jinsi, mahali, hali ya nyuzi sauti, mwinuko wa ulimi na umbo la midomo katika utamkaji wa sauti mbalimbali za lugha tofauti tofauti.
B.     KIGEZO CHA KIFONOLOJIA
Hiki ni kile kinachoangalia maathiriano ya lugha. Fonolojia nyambulishi ya lugha mahsusi. Hapa sifa za lugha inayochambuliwa huangaliwa zaidi. Kwa mfano, kuna baadhi ya fonimu hupata sifa ya usilabi katika lugha mojawapo na siyo nyingineyo. Mfano, mtu, /m/ inapata sifa ya usilabi. Pia katika nne, /n/ hupata sifa ya usilabi. Aidha, hali hii inalingana na mfumo wa lugha husika.
Wanafonolojia wengi wanakubaliana kwamba wazo la sifa pambanuzi lilianzishwa na shule ya “Mawazo ya Prague”. Hata hivyo mwanazuoni wa kwanza kulibabadua suala la sifa pambanuzi alikuwa ni NIKOLAJ TRUBETZKOY, naye ni mmojawapo kati ya waanzilishi wa Shule ya Mawazo ya Prague. Mwanazuoni huyu alianzisha nadharia ya Upambanuzi (Trubetzkoy 1969:31-83). Madai ya msingi katika nadharia hii ya Trubetzkoy ni kwamba pakiwapo na upambanuzi basi lazima patakuwapo ‘ukinzani’. Naye anauainisha ukinzani pambanuzi katika seti kuu tatu.
SETI YA KWANZA
(a)    Ukinzani uwili
(b)   Ukinzani kiwingi
(c)    Ukinzani kiwiani na
(d)   Ukinzani kipeke
(a)   UKINZANI KIUWILI (Bilateral Opposition)
Ni ukinzani wa sauti ambapo jumla ya sifa bainifu zinazochangiwa na sauti mbili kinzani hupatikana katika sauti hizo mbili peke yake na si kwingineko. Mfano, vipasuo vya midomo [p] na [b] katika Kiswahili ambavyo vinachangia sifa ya kuwa vipasuo vya kinywa vya midomo, hakuna vipasuo vingine vinachongia sifa hiyo.
(b)   UKINZANI KIWINGI (Multilateral Opposition)
Huu ni ukinzani wa sauti ambapo jumla ya sifa bainifu zinazochangiwa na sauti hizo kupatikana katika seti ya sauti nyingine pia. Mfano P na R (herufi) zote zinachangia mkunjo upinde unaoelekea kulia. Lakini haziwezi kuhesabiwa kuwa na ukinzani kiuwili, kwa sababu sizo herufi pekee zenye mkunjo kama huo herufi B nayo inao. Hivyo, ukinzani unaopatikana katika sauti ambazo jumla ya sifa zinazochangiwa nazo hupatikana pia katika ukinzani mwingine na ndio ujulikanao kama ukinzani kiwingi
(c)    UKINZANI KIWIANI (Proportional opposition)
Ni ukinzani wa sauti mbili ambao unawiana na ukinzani wa sauti mbili ambao unawiana na ukinzani wa sauti nyingine mbili. Mfano, ukinzani baina ya [f] na [v] na ukinzani baina ya [s] na [z] katika Kiswahili.
(d)   UKINZANI KIPEKE (Isolated opposition)
Ni ukinzani ambao ni wa kipekee kabisa. Mfano, ukinzani baina ya sauti [r] na [l] katika lugha ya Kiingereza. Katika lugha hii hakuna memba wengine walio na uhusiano wa namna hiyo.
SETI YA PILI
(a)    Ukinzani kibinafsi
(b)   Ukinzani kimwachano taratibu
(c)    Ukinzani kisawa

(a)   UKINZANI KIBINAFSI (Private opposition)
Huu ni ule ukinzani ambapo sauti moja inakuwa na alama za ziada (sifa ya ziada) na sauti nyingine inakuwa haina, mfano kama sauti moja inakuwa na mghuno nyingine inakuwa haina n.k.
(b)   UKINZANI KIMWACHANO TARATIBU (Gradual opposition)
Ni ule ukinzani ambapo memba wa seti wanapishana kwa viwango tofauti vya sifa ileile. Mfano, tofauti iliyopo baina ya irabu [o] na [u].
(c)    UKINZANI KISAWA (Equipollent opposition)
Ukinzani ambapo ukinzani baina ya memba wa kundi moja ni sawa na ukinzani baina ya memba wa kundi jingine, kimantiki; kwa maana ya kwamba ukinzani wao si wa kupishana kwa viwango vya sifa ileile wala hawawezi kuchukuliwa kwamba kama memba mmoja wa kundi ana sifa ya ziada basi mwingine hana. Kwa mfano, sauti [p] na [t] na [f] na [k] katika Kijerumani.
SETI YA TATU
(A) Ukinzani imara (ukinzani usobadilifu)
(B)  Ukinzani usoimara (ukinzani ulobadilifu)
Trubetzkoy pia anaziainisha sifa pambanuzi kwa kuangalia kiasi cha ubainifu wa upambanuzi wa sifa. Mfano, ukinzani baina ya /t, d, l/ katika Kiswahili. /t/ siku zote inakuwa /t/ lakini /l/ inaweza kugeuka na kuwa /d/ mfano, katika u-limi------ n-dimi. Hivyo ukinzani wa /t/ ni imara lakini ule wa /d,l/ si imara (badilifu).
SIFA PAMBANUZI ZA ROMAN JAKOBSON
Huyu ni miongoni mwa wanazuoni waliotumia sifa pambanuzi katika uwakilishi wa vipengele vya kifonolojia na kifonetiki (1952). Aidha, ni mwanzilishi mwingine wa Shule ya Mawazo ya Prague. Katika nadharia yake ya sifa pambanuzi, alianza kwa kubanisha sifa za kimatamshi dhidi ya sifa za kiakustika. Kisha akabainisha sifa za uwili dhidi ya sifa zisouwili. Pia Jakobson na Halle (1956) wakabainisha sifa pambanuzi katika makundi makuu matatu. Nao walijishughulisha zaidi na sifa kinzani katika lugha. Sifa zao zilielemea zaidi katika ‘ukinzani wa kifonolojia kuliko ule wa kifonetiki. Mazoea ya watangulizi wao yalikuwa ni kuziainisha sauti kifonetiki, yaani kubainisha konsonanti, irabu, viyeyusho na vitambaza. Lakini wao walizigawa katika makundi mawili zile zenye ukonsonanti na zile zisizo na ukonsonanti yaani konsonanti na vokali. Wakazigawa tena sifa hizi kuu katika makundi madogomadogo manne

1.      Konsonati halisi
                                                 +konso
                                           -vokali
                                                 /p/

2.      Vokali


-konso
+voka
/a/
3.      Vitambaza


                  +konso
                  +voka
                  /l/
4.      Viyeyusho


                   -konso
                   -voka

                          /y/

SIFA PAMBANUZI ZA CHOMSKY NA HALLE
Sifa zao zilijikita zaidi katika uelekeo wa kifonetiki kuliko walivyofanya Jakobson na Halle. Katika uainishaji wao sifa pambanuzi za sauti za lugha wanazigawa katika makundi matatu.
(i)                 Sauti zenye usonoranti (dhidi ya zile zisizo na usonoranti).
(ii)               Sauti zenye uvokali (dhidi ya zisizo na uvokali).
(iii)             Sauti zenye ukonsonanti (dhidi ya zile zisizo na ukonsonanti)

(i)                 KUNDI LA SONORANTI (dhidi ya zisosonoranti)
Kwa mujibu wa Chomsky na Halle (1968:302) sauti zenye usonoranti hutolewa kwa kuiweka njia ya mkondohewa katika mkao ambao huwezesha ughunishaji wa sauti wa papo hapo, wakati zile zisizo na usonoranti (obstruenti) hutolewa kwa kuiweka njia ya mkondohewa katika mkao ambao hauwezeshi ughunishaji wa papo hapo, mfano, nazali, vitambaza, vimadende na viyeyusho.
(ii)               KUNDI LA V OKALI
Sauti zenye uvokali hutolewa kwa kuweka mkao wa mvungu  wa kinywa katika hali ambayo ubanaji wa mkondohewa hauzidi ule utumikao katika kutamka sauti [i] na [u], na wakati huohuo nyuzisauti zikiwa katika mkao ambao huwezesha ughunishaji wa papohapo.
► Sauti zenye uvokali ni : irabu na vitambaza ghuna, viyeyusho, konsonanti nazali, obstruenti, irabu zisoghuna na vitambaza visoghuna hazina uvokali.
(iii)             KUNDI LA KONSONANTI
Sauti zenye ukonsonanti hutolewa kwa uzuiaji mkali wa mkondohewa katika sehemu ya kati ya njia ya mkondohewa. Sauti zisizo na ukonsonanti hutamkwa bila kuwepo uzuiaji wa mkondohewa wa namna hiyo. Hivyo basi, sauti zenye usonoranti ni: irabu, viyeyusho, nazali, konsonanti na vilainisho. Zenye uvokali: irabu ghuna na vilainisho zenye unazali na konsonanti zisizo na unazali. Baadaye waliona istilahi ya vokali inachanganya wakaanza kutumia istilahi ya USILABI.
SABABU ZA KUCHUNGUZA SIFA BAINIFU/ PAMBANUZI
1.      Kujumuisha vitamkwa vinavyochangia sifa fulani.
2.      Kutenga makundi asilia yanayochangia mahali pa matamshi n.k. mfano, vitamkwa vya msingi vinaweza kuwekwa katika makundi asilia.
3.      Waliona kuwa kuna sifa zitumikazo katika kila lugha duniani, mfano, sifa ya ukonsonanti [+konso]. Nayo huhusisha vitamnkwa vinavyohusishwa msuguano katika utokeaji wake ambao waweza kuwa wa kubana, mwembamba au wa kimadende. Hali hii huletelea makundi kama ya: vizuio, vikwamizi, ving’ong’o, vitambaza na vimadende. Waliona pia kuna uwepo wa usilabi [+sil]. Ving’ong’o, vitambaza huwa na usilabi katika baadhi ya lugha. Waliona kwamba ni vema wabague/ watenganishe kati ya ving’ong’o na vitambaza/ vimadende.
► Sifa ya Usonoranti
Kuna ughuna wa vitamkwa kama vile vyenye usilabi na hakuna mguno kwani mkondohewa hauzuiliwi. Ukonsonanti, usilabi na usonoranti huweza kuletelea aina mbalimbali ya makundi. Vipasuo ndani, vikwamizi kwani kuna vitamkwa vina sifa ya ukonsonanti na hazina usonoranti wala usilabi.

SIFA BAINIFU/ PAMBANUZI ZIJENGAZO FONIMU ZA KISWAHILI SANIFU
Konsonanti ni aina ya vitamkwa vitokanavyo na msogeano wa kubana, mwembamba, au wa umadende wa ala za matamshi. Kifonetiki, konsonanti huainishwa kufuatana na kubanwa kabisa kwa mkondohewa katika chemba au kufuatana na kuwepo kwa upenyu mwembamba kiasi cha kuleta msuguano. Katika uchanganuzi wa kifonetiki, sifa bainifu za konsonanti huainishwa kwa kutumia sifa zote hata zile zisizo za lazima, tofauti na uchanganuzi wa kifonolojia ambapo uainishaji wa sifa bainifu huhusisha sifa zile za lazima tu nazo ni:  namna ya kutamka, mahali pa kutamkia, hali ya nyuzi sauti, mkao wa kilimi, mkao wa ulimi,  na mfumo wa mkondohewa.
A.    SIFA YA JINSI YA MATAMSHI
(i)                 Sifa ya usilabi  [+sil]
Irabu za Kiswahili zina sifa ya usilabi, ving’ong’o katika mazingira maalumu vinakuwa na sifa ya usilabi hasa katika mazingira ya kisarufi.
(ii)               Mghuno/ughuna [+ghuna]
Nyuzisauti zinapotetemeshwa sauti zitolewazo huwa na mghuno; konsonanti ghuna, vilainisho, irabu, ving’ong’o n.k.
(iii)             Ukontinuanti [kont]
Wakati wa kutolewa sauti hizi kuna kuwa na msogeano mpana au mwembamba. Mfano, vikwamizi, irabu, ving’ong’o, viyeyusho na vilainisho n.k.
(iv)             Unazali [+naz]
Wakati wa kutolewa kwa sauti hizi hewa huzuiliwa kupita mdomoni na kupitia puani, mfano, [m, n, ŋ,ň]
(v)               Utambaza [+tambaz]
Hii huhusika na vitamkwa ambavyo wakati wa kutolewa hewa huzuiliwa na kupita pembeni mwa ala sauti mfano [l]
(vi)             Stridenti
Sifa pambanuzi inayohusu sauti zitamkwazo kwa msikiko wa kelelekelele kuliko sauti nyingine. Mfano, [s], [z], [š], [ ], [f], [v], [ts]. Hutamkwa kwa kulazimisha mkondohewa kupita katika sehemu mbili kwa namna ya msuguano ambao hutoa sauti ya kukwamizwa yenye msikiko wa juu.
(vii)           Umadende [+mad]
Ni vile vitamkwa vitolewavyo wakati ala sogezi hugongagonga kwenye ala nyingine tulivu, kwa mfano [r].
2. SIFA ZA MAHALI PA MATAMSHI
(a) Ukorona [+kor]
Huhusisha vitamkwa ambavyo wakati wa kutolewa bapa/ ncha ya ulimi huhusika na kuna kuwa na msogeano wa kubana au mwembamba wa ala za matamshi, mfano, sauti za meno, ufizi, kaakaa gumu.
(b) Uanteria [+ant]
Huhusisha vitamkwa vinavyotolewa kwenye ufizi na mbele ya ufizi /t/, /d/, midomo, meno na ufizi.
© Umeno [+meno]
Huhusisha vitamkwa vitolewavyo kwenye meno mfano [th na dh]
(d)   Uglota [+glot]
Huhusisha kitamkwa kinachotolewa kwenye glota katikati ya nyuzisauti mfano [h]
3 SIFA BAINIFU ZIHUSUZO KIWILIWILI CHA ULIMI
(i)                 Ujuu [+juu]
Hii inahusu vitamkwa ambavyo wakati wa kutolewa, ulimi hunyenyuliwa juu ya chemba ya kinywa mfano, [i,u ts ny]
(ii)               Uchini [+chini]
Hii huhusisha vitamkwa ambavyo wakati wa kutolewa, ulimi unakuwa chini ya kinywa mfano [a].
(iii)             Unyuma [+nyuma]
(iv)             Hii hujihusisha na vitamkwa ambavyo hutolewa sehemu ya nyuma ya chemba ya kinywa, mfano, [u, o, k, g, ng].




SIFA BAINIFU NYINGINEZO
UWEKEVU
Katika kubainisha fonimu. Tumia sifa chache kadri iwezekanavyo bayana katika kubainisha fonimu. Mfano,
-          ughuna na usighuna
-          ukontinuanti/ uendelezi/ vifulizwa
-          uanteria
-          ukorona

/p/                                /b/                                /t/                     /d/
-gh                               +gh                              -gh                   +gh
-kont                            -kont                            -kont                -kont
+ant                             +ant                             +ant                 +ant
-kor                              -kor                              +kor                 +kor

(II) UZIADA
Kuwepo au kutokuwepo kwa sifa fulani kunatabirika kutokana na kuwepo au kutokuwepo kwa sifa nyingine. Hususani zile ambazo si muhimu kubainisha fonimu. Kwa mfano,
/i/
+sil
+juu                                                              +sil
+son                                                             +juu
-chini                                                           +son
+mbele
-nyuma
+ghuna
+kont
Sifa za ziada za /i/ ni:
+kont
-chini
-nyuma
+mbele
+ghuna

Sifa za ziada hubainishwa kwa kutumia mantiki. Na huwa si muhimu kubainisha fonimu. Sifa inaweza kubainishwa kwa kutumia uwili unaokinzana. Mfano,
+kont = [-kont]
Mwanamke                             Mwanamme
[+ke/ -me]                    [+me, -mke]
Mfano, nazali zote zina ughuna. Pia sauti ambazo ni sonoranti zina sifa ya ughuna. Mantiki inatumika kubainisha sauti zenye sifa ya uziada. Mfano, nazali haiwezi kuwa madende a kiyeyusho.


MAKUNDI ASILIA YA FONIMU ZA KISWAHILI
1.      VIPASUO/ VIZUIO
Hutamkwa kwa kuzuia kabisa mkondohewa utokao mapafuni kasha kuachiwa ghafula.
/p/                    /d/                    /b/                                /t/                     /k/
-kont                -kont                -kont                            -kont                -kont
-gh                   +gh                  +gh                              -gh                   -gh
+anteria           +ant                 +ant                             +ant                 +ant
-kor                  +kor                 -kor                              +kor                 +juu
                                                                                                                  +nyuma
2.      VIKWAMIZO/ VUKWAMIZWA/ VIKWAMIZWA
/f/                     /v/                    /th/                   /dh                   /s/      
+kont               +kont               +kont               +kont               +kont
-gh                   +gh                  -gh                   +gh                  -gh
+meno             +meno             +meno             +meno             +kor
-kor                  -kor                  +kor                 +kor                 -meno

/sh/                   /γ/                                /h/
+kont               +kont                           +kont
+kor                 +gh                              +glot
-gh                   +unyuma                     -gh
-juu                  +ujuu
-nyuma

3.      VING’ONG’O
/m/                                           /n/                    /η/                               /ny/
+nazal                                      +nazal              +nazal                          +nazal
+ant                                          +kor               -sil                               -sil
+sil                                            -sil                 +unyuma                     +juu
-kor                                                                  -kor                              -nyuma
+ghuna                                                            -ant                              +kor
+midomo                                                         +juu                             -ant

4.      VILAINISHO- Sonoranti
/l/                                 /r/
+son                            +son
+kor                             +kor
+tambaz                      +mad
+ghun                          +ghuna
-unazal                         -nazal

5. IRABU [+sil]

/i/                     /u/                    /e/                    /o/                    /a/
+sil                  +sil                  +sil                  +sil                  +sil
+juu                 +juu                 -nyuma            +nyuma           +chini
-nyuma            +nyuma           -chini               -juu                  -juu
                                                -juu                  -chini

6. VIYEYUSHO [-sil]
/w/                               /j/
-sil                               -sil
+juu                             +juu
+nyuma                       -nyuma

UMUHIMU WA SIFA BAINIFU
1.      Husaidia kugawa fonimu katika makundi asili.
2.      Husaidia kutofautisha kati ya kundi moja la fonimu asilia na jingine.
3.      Husaidia kuonesha maathiriano yanayotokea katika lugha.
4.      Hurahisisha katika uandishi wa kanuni kwani zinaandikwa kwa ufasaha na bayana.
5.      Huonesha mwenendo au tabia ya lugha Fulani kwa sababu tunaelewa baadhi ya fonimu hubadilika kutokana na muktadha wa fonimu au kimatumizi mfano, nazali ina sifa ya usilabi na isiyo na usilabi.
6.      Husaidia kuonesha muundo wa ndani wa sauti fulani.
MODULI YA 5:  KANUNI NA MICHAKATO YA KIMOFOFONOLOJIA
Ni mabadiliko yanayoonekana ya fonimu moja au mbili. Kila lugha ina mfumo wake wa kifonolojia. Hakuna lugha zinafanana idadi zake za fonimu na alofoni. Katika lugha kuna mfanano wa sifa bainifu zinazoelekeana kati ya lugha moja na nyingine kwa mfano, sifa za ujuu, ughuna n.k. Ila si katika lugha zote kwa sababu ya ufanano huo ni kwa sababu alasauti (viungosauti) vya kutolea sauti hufanana kwa binadamu wote.
Aidha, kila lugha ina mifumo yake asilia ya kifonolojia (Natural phonological processes) ijapokuwa hutofautiana.
MICHAKATO ASILIA
Ni taratibu zinazoonesha maathiriano ya sauti katika lugha nyingi duniani. Inaitwa michakato asilia kwa sababu ipo katika lugha zote duniani.
AINA ZA MICHAKATO
Michakato ya kiusilimisho
Michakato isiyo ya kiusilimisho

MICHAKATO YA KIUSILIMISHO
Ni ile inayohusu kufanana kwa kiasi kikubwa kwa vitamkwa kutokana na ujirani (kukaribiana kwake) yaani hupata baadhi ya sifa za kipande sauti chenziye kilicho jirani. Mfano,
MICHAKATO ISIYO YA KIUSILIMISHO
Ni ile inayohusu vitamkwa au sauti ambazo hazifanani kwa kiasi Fulani wakati wa mchakato.
KANUNI ZA KIFONOLOJIA
Ni maandishi rasmi yanayowakilisha michakato asilia. Kanuni hizi zimejikita katika nadharia za Morris Halle na Noam Chomsky waliobainisha muundo wan je na wa ndani wa maneno.
UMBO LA NDANI
Umbo kama lilivyo katika lugha husika ambalo haliwezi kuonesha mchakato.
UMBO LA NJE
Umbo linaloonesha lugha katika utendaji wake (uhalisia wake). Nalo linatuwezesha kujua mchakato.
MICHAKATO YA KIUSILIMISHO
I.                   UNAZALISHAJI WA IRABU (Vowel nasalization)
Ni mchakato ambao irabu hupata baadhi ya sifa za nazali kutokana na yenyewe kutangamana na konsonanti ambayo ni nazali. Mfano,
/muwa/                                  [mũwa]
/nuru/                                    [nũru]
/mama/                                  [mama]
/pãn/                                      [pãn]
/pen/                                      [pẽn]
Irabu zinazotangamana na nazali nazo zinapata sifa ya unazali.
II.UTAMKIAJI PAMWE NAZALI (Homorganic nasal assimilation)
Ni usilimisho unaohusu konsonanti ambayo ni nazali kutamkiwa mahali pamoja na konsonanti inayofuatia. Mfano, mbuzi, ndama, ŋgoma.
III UKAAKAAISHAJI
Ni aina ya usilimisho ambapo konsonanti ambayo hapo awali haikuwa na sifa ya ukaakaa hupata sifa hiyo kutokana na kufuatiwa na kiyeyusho au irabu. Mfano
Ki+a+ku+l+a                                    kya:kula
Ki+etu                                              kyetu

IV.  UYEYUSHAJI
Ni sauti isiyo kiyeyusho inaathiriwa na kuwa kiyeyusho, sauti mbili zinapokutana inatokea sauti moja mfano, irabu zinapotokea katika mazingira Fulani hubadilika na kuwa kiyeyusho. Mfano,
Mu+eupe                                mweupe
Mu+ana                                  mwana
Mu+alimu                              mwalimu
V. MVUTANO WA IRABU/ MUUNGANO WA SAUTI
Sauti mbili hukutana au kuungana hasa irabu ya juu na chini na kupata irabu ya kati. Mfano,
Ma+ino                                  meno
Ma+iko                                  meko
Ma+ini                                   maini
Ma+iti                                    maiti
Hakuna mabadiliko yanayotokea katika mjumuisho wa fonimu.
KANUNI YA KONSONANTI KUATHIRI NAZALI
Mazinrira fulani ya utamkaji konsonanti huathiri nazali iwe inafanana na konsonanti inayofuatia.
Mfano,
M+buzi                                              mbuzi
N+dugu                                             ndugu
N+goma                                             ngoma
N+gombe                                           ŋng’ombe
Konsonanti inayofuatia nazali ndiyo inayoathiri nazali.
NAZALI KUATHIRI KONSONANTI
Yaani nazali ndiyo inayoathiri konsonanti ili konsonanti hiyo ifanane na nazali, mfano,
U+limi                                    ulimi
N+limi                                    ndimi
U+refu                                    urefu
N+defu                                   ndefu
Katamba anasema kuwa mchakato huu ni uimarishaji wa sauti karibu kuna sauti ambazo ni ndefu.

TANGAMANO LA IRABU
Ni usilimisho baina ya irabu na irabu, yaani huathiriana kiasi kwamba hulazimika kufanana. Kufanana, kupeana sifa zinazofanana. Kwa mfano,
Paka                                        pakia
Pika                                                   pikia
Soma                                                 somea
Tupa                                                  tupia
sema                                                  semea

Mofimu ya utendea hubadilika kutokana na irabu inayofuatia mzizi wa neno. Irabu a,i na u] mofimu yake ya utendea ni /i/
Irabu [e,o] mofimu yake ya utendea ni [e].
MICHAKATO ISOUSILIMISHO
A.UDONDOSHAJI
Kitamkwa ambacho awali kilikuwa katika neno kinaondoshwa au kinaangushwa. Mfano
Mu+tu/                                   /mutu/- [mtu]
Mu+totohh                                 /mutoto/- [mto]        
Udondoshaji sio katika irabu tu bali hata konsonanti hudondoshwa.
Waliokuja                                             walokuja
Amekwishakula                                   ameshakula
I am going                                            I’m going
I have no food                                     I’ve no food

B.UCHOPEKAJI
Uingizaji wa sauti ambazo hazikuwepo katika neno. Mfano
Kiarabu                                    Kiswahili
Aql                                           akili
Saqf                                          sakafu
Bakhat                                      bahati
C. TABDILI
Ni mchakato ambao kwao sauti mbili zilizo jirani hubadilishana nafasi. Mfano
Nga+wa+reng+a+o = ngwaareengao ‘wanachukua’
Nga+wa+jo+reng+a = ngwaajoreenga = ‘watachukua’
Nga+wa+reng+a = ngwaajoreenga = wanachukua
Ka+wa+tsi+reng+a = ‘hawachukui’






VIARUDHI/ VIPAMBASAUTI
Hizi ni sifa ambazo huambatishwa katika vitamkwa na kuleta maana. Sifa hizi huambatana na vitamkwa asilia kama vile: silabi, neon, kirai na sentensi (vipashio ambavyo ni vikubwa kuliko foni na vinatumika katika mfumo wa lugha). Viarudhi hujumuisha jiografia ya mzungumzaji.
►KIIMBO
Ni upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti katika usemaji. Kutokana na kiimbo tunaweza kumtambua mzungumzaji kama anauliza swali, ombi, amri, maelezo, kejeli au mshangao.
AINA ZA VIIMBO
(i)                 Kiimbo cha maelezo kwa mfano, Mtoto anakula
(ii)               Kiimbo cha kuuliza kwa mfano, Mtoto anakula?
(iii)             Kiimbo cha kuamuru kwa mfano, Nenda nje
(iv)             Kiimbo cha mshangao kwa mfano, khaa! Mtoto anakula
(v)               Kiimbo cha kejeli, Mtoto anakula

► KIDATU
Hii ni sifa ya kiarudhi ambayo hubainishwa na kupanda na kushuka (mpandoshuko) kwa kiwango cha sauti. Kidatu hudokeza maana ya msemaji (kwa msikilizaji). Hali hii hutokana na kasi ya msepetuko wa nyuzi za sauti ndani ya koromeo.
AINA ZA KIDATU
(i)                 Kidatu cha juu
(ii)               Kidatu cha kati
(iii)             Kidatu cha chini
Kwa ujumla kidatu ni kiwango cha juu, cha kati au cha chini katika usemaji.
►LAFUDHI
Ni tofauti ya mzunguzaji kutokana na mazingira na jiografia aliyotoka mzawa wa lugha. Lafudhi huonesha lugha yake ya kwanza.
Mpare neno supu ►thupu
Mnyakyusa chai ► kyai
Mmkonde ► Athumani Achumani
►MKAZO
Ni msisitizo / utamkaji wa silabi au neon kwa kutumia nguvu nyingi, hali ambayo huifanya silabi au neno hilo kusikika kuliko silabi nyingine katika neno husika au neno katika tungo.
AINA ZA MKAZO
(i)                 Mkazo mkuu
Huifanya silabi husika kusikika Zaidi kuliko silabi nyingine katika neno, kirai, kishazi au sentensi. Alama ᾽ ndiyo hutumika kuwalikisha mkazo huu.
(ii)               Mkazo wa kawaida
Hauna msikiko mkubwa kama mkazo mkuu ῝ ni alama itumikayo katika unukuzi wake.
Mkazo unaweza kutokea mwanzoni, katikati au mwishoni mwa neno. Kila lugha huwa na utaratibu wa uwekaji wa mkazo. Katika lugha ya Kiswahili mkazo huwekwa katika silabi ya pili kutoka mwisho wa neno.
► WAKAA
Ni muda unaotumika katika utamkaji wa fonimu fulani. Wakaa unaweza kuwa mfupi, kawaida na mrefu. Wakaa mrefu huonyeshwa kwa nukta mbili.
Mfano, paa► pa:

► TONI
Mgullu (1999) anasema toni ni kiwango cha kidatu pamoja na mabadiliko yake ambayo hutokea wakati mtu anapotamka silabi au maneno. Katika lugha za toni (tonal languages) mabadiliko ya toni hubadili maana za maneno. Hata hivyo ikumbukwe kwamba si kila lugha ina toni, lugha ya Kiswahili kwa mfano na Kinyakyusa (hazina) toni bali zina mkazo. Ni sifa inayowakilisha kiwango pambanuzi cha kidatu cha silabi katika neno au sentensi na ambayo huweza kubadilisha maana ya neno au sentensi hiyo kisemantiki au kisarufi. Tunaweza kupata aina mbalimbali za toni kutokana na utamkaji.
Toni huweza kuwa ya kupanda (rising tone), ya kushuka (falling tone), ya kupanda shuka (rise-fall) na kushuka panda (fall-rise). Wanasimu wengi husema kwamba hapo kale lugha zote za Kibantu, Kiswahili kikiwemo, zilikuwa na toni lakini kutokana na mabadiliko na nyakati ndipo zingine zimepoteza toni hizo. Hili linaonekana katika Kiswahili kwa maneno: barabara na barabara
AINA ZA TONI
Kmsingi kuna aina kuu mbili za toni, yaani toni za kisarufi na toni za kileksika.
(i)                 TONI ZA KISARUFI
Hizi ni zile ambazo zinapotumika katika maneno hazina athari yoyote katika maana bali hufanya kazi za kisarufi kuonyesha aina ya tendo, nyakati n.k. Mifano mizuri ya toni za aina hii ni zile za lugha ya Kiruri
Okutema                                     kata
Okutemera                                  katia
Okutemeranira                            katiana
KISAFWA
Alya                                            anakula
Álya                                            amekula
(ii)               TONI ZA KILEKSIKA
Hizi ni zile ambazo zinapotumika katika maneno hubadili maana ya maneno. Hii ni kusema kwamba neno lile lile huweza kuwa na maana tofauti tofauti kutokana na tofauti ya toni.
KISAFWA
Gula                                            nunua
Gula                                            subiri
Shila                                           kile
Shila                                           nenda/ondoka
Lila                                             lile
Lila                                             lia

SILABI
Ni dhana ya kifonolojia ambayo huwakilisha umbo la matamshi ambapo sauti moja au zaidi hutamkwa kwa mara moja kama fungu moja.
Silabi ni kipashio cha kifonolojia ambacho ni kikubwa kuliko fonimu lakini kidogo kuliko neno katika mfumo wa darajia.
AINA ZA SILABI
1. SILABI HURU/WAZI
Ni silabi ambazo mara nyingi huishia na irabu. Msikiko wake ni mkiubwa.
SILABI FUNGE
Ni silabi ambazo huishia na konsonanti. Msikiko wake ni hafifu. Aghalabu irabu huchukuliwa kama kilele cha silabi. Aidha, irabu ni vitamkwa ambavyo vikitolewa hakuwi na mzuio wa hewa.
NAMNA YA KUWAKILISHA MUUNDO WA SILABI
Kuna wananadharia wanaosema kuwa silabi inaweza kuwasilishwa kwa namna mbalimbali. Pike na Pike (1943) wanasema kuwa muundo wa silabi una matawi na darajia. Baadhi ya wanataaluma wanaona kuwa silabi ina mwanzo na kilele. Wengine hudai kuwa silabi ina upeo na ukingo/mpaka/margin (sehemu ya mwanzo au ya mwisho wa silabi. Kuna wanazuoni wengine kama vile Halle, Harris na Vernaud wanasema kuwa silabi ina vitamkwa vinavyobeba sifa bainifu. Aidha, silabi zenye matawi na darajia zina tia.
Katamba (1996:176) anasema kuwa suala la kuainisha silabi kwa vigezo huru na funge ni la kimapokeo ama kijadi. Hivyo basi tunatakiwa kuangalia silabi husika kama ni nzito au nyepesi.
SILABI NZITO
Ni ile silabi ambayo upeo wake una tawi linalogawanyika.
Kwa mfano;


$lah$

                                                                            6

Mwanzo wa silabi                                                                       upeo wa silabi ah
l
                                                                        Kiini cha silabi                        ukingo wa silabi
                                                                               a                                                     h

SILABI NYEPESI
Ni ile silabi ambayo upeo wake haugawanyiki kwa mfano ba, ma da ,fa ja n.k.
                                                                                    6

                                       Mwanzo wa silabi                            upeo wa silabi
                                                   M                                               a

Mwanzo wa silabi ndio una msukumo wa matamshi. Hivyo basi silabi ma ni huru ni ni nyepesi kwani haina tawi linalogawanyika.
Kila lugha ina muundo wake wa silabi kulingana na idadi ya fonimu zilizopo.
MUUNDO WA SILABI HURU ZA KISWAHILI
Muundo wa irabu pekee kwa mfano katika ua, oa, au
Muundo wa nazali pekee kwa mfano katika mganga, mtoto, mdogo
Muundo wa konsonanti na irabu kwa mfano katika kaka, dada, debe, baba, raha
Muundo wa konsonanti konsonanti na irabu kwa mfano
(a)    Kipasuo+kiyeyusho+irabu kwa mfano, pweke
(b)   Kikwamizo+kiyeyusho+irabu kwa mfano, swaga
(c)    King’ong’o|+kiyeyusho+irabu kwa mfano. Mwaka
(d)   Kikwamizo+kipasuo+irabu kwa mfano spika
(e)    Kipasuo+kiyeyusho+irabu kwa mfano, bweka
Konsonanti konsonanti kiyeyusho na irabu kwa mfano;
(a)    Nazali+kipasuo+kiyeyusho+irabu kwa mfano pingwa
(b)    Nazali +kipasuo+ kiyeyusho+irabu kwa mfano pandwa, undwa
(c)    Nazali+ kikwamizo+kiyeyusho+irabu kwa mfano chinjwa
MUUNDO WA SILABI FUNGE
Aina hizi za silabi haziishii na irabu. Pia huwa hazisikiki na huweza kutokea mwanzoni, katikati au mwishoni mwa neno
MWANZONI MWA NENO
1.      Silabi zenye ukingo /l/ kwa mfano
Alfajiri, almasi, halmashauri, hulka n.k.
2.      Silabi zenye ukingo /s/ kwa mfano
Askari, askofu, desturi, mustarehe, rasmi, hospital, taslimu, wastani n.k.
3.      Silabi zenye ukingo /k/ kwa mfano
Daktari, bakshishi, iktisadi, takribani, aksante, maksai, muktadha, nuksi, nukta n.k.
4.      Silabi zenye ukiongo /r/ kwa mfano
Ardhi, karne n.k.
5.      Silabi zenye ukingo /n/ kwa mfano
Ankra
6.      Silabi zenye ukingo /m/ kwa mfano
Hamsini, mamsapu, alhamudullilah, hamsa n.k.
7.      Silabi zenye ukingo /p/ kwa mfano
Aprili, kaptula, kapteni
8.      Silabi zenye ukingo /b/ kwa mfano
Biblia, kabla, rabsha n.k.
9.      Silabi zenye ukingo /j/ kwa mfano;
Majhununi
SILABI ZENYE UKINGO ZINAZOTOKEA KATIKATI YA NENO
Kwa mfano, mfalme, daftari, eropleni n.k.
SILABI ZENYE UKINGO ZINAZOTOKEA MWISHONI MWA NENO
Kwa mfano jehanam, inshallah n.k.
Kwa ujumla maneno mengi yanayotumia silabi funge mengi ni ya kukopa.
DHIMA YA SILABI
-          Silabi ni kipashio cha msingi ambacho kina dhima ya kifonotaktiki (kanuni ambayo inamruhusu mzungumzaji kutumia mfuatano unaokubalika na kumkataza mfuatano usiokubalika. Kwa mfano, katika Kiswahili hakuna silabi inayoundwa kwa mfuatano kappa. Hivyo basi, muundo wa silabi hutusaidia kujua mfuatano sahihi kulingana na lugha husika.
-          Silabi inatumika kama mawanda ya kanuni za kifonolojia.
-          Silabi ni kama muundo wa kipande sauti changamano. Silabi hupambanua/hudhibiti mfuatano wa sifa thabiti.
-          Silabi ni kipashio ambacho hutumika kuunda vipashio vikubwa zaidi katika taaluma ya fonolojia kama vile toni, shada/mkazo. Pia inatumika kubainisha maana ya kifonolojia, kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili tunaweka mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho wa neno.
SIFA MAJUMUI ZA LUGHA KATIKA FONOLOJIA
Madhumuni makubwa ya fonolojia ni kuweka wazi baadhi ya sifa majumui zinazojitokeza katika lugha asilia. Hii inatokana na ukweli kwamba kuna tofauti za wazi zinazojitokeza katika fonolojia ya mifumo mbalimbali ya lugha asilia, bado kuna sifa fulani ambazo zinaelekea kuchangiwa na lugha zote. Sifa zinazoelekea kuchangiwa na lugha zote asilia ndizo zinazoitwa sifa majumui za lugha.
AINA ZA SIFA MAJUMUI ZA LUGHA
(a)   SIFA MAJUMUI HALISI ZA LUGHA
Hizi ni zile sifa za kiisimu ambazo ni za kawaida katika lugha zote za binadamu. Kwa mfano, lugha zote za binadamu huwa na irabu na konsonanti katika orodha ya sauti zake; ingawa idadi ya irabu na konsonanti hizo huweza kutofautiana toka lugha moja hadi lugha nyingine. Vilevile, lugha zote asilia zina silabi, ingawa muundo wa silabi unaweza kutofautiana toka lugha moja hadi lugha nyingine; katika lugha zote asilia irabu na konsonanti hupangiliwa katika silabi.
(b)   SIFA MAJUMUI PANA ZA LUGHA
Hizi ni zile sifa ambazo hupatikana katika lugha nyingi, ingawa sio zote. Kwa mfano, wanaisimu wengi hukubaliana kwamba lugha nyingi za binadamu huwa zina angalau irabu tano. Pamoja na huo ukweli kuna ukweli mwingine kwamba kuna baadhi ya lugha chache ambazo zina irabu saba au zaidi, na kuna lugha nyingine zenye irabu tatu.
(c)    SIFA MAJUMUI TABIRIFU ZA LUGHA
Hizi ni zile sifa ambazo kuwapo kwa sifa moja ya msingi huashiria kuwepo kwa sifa nyingine ambayo inahusiana na hiyo sifa ya msingi. Kwa mfano ikiwa katika lugha kuna tonijuu basi kutakuwa na tonichini pia.

No comments:

Post a Comment