Wednesday

UCHAPISHAIJI WA VITABU, MAENDELEO YA TEHAMA NA UCHAPISHAJI

0 comments




Mwandishi
Prof Mbele @masshele
Tangu shughuli ya uchapishaji wa vitabu ilipoanza nchini mwetu, wakati wa ukoloni, kuchapishwa kwa kitabu kulitegemea uamuzi wa mchapishaji. Waandishi hawakuwa na madaraka juu ya mchapishaji bali walikuwa kama watumwa mbele ya mchapishaji. Hali hii haikuwa kwa upande wa vitabu tu, bali hata aina nyingine za maandishi. Watunzi wa mashairi, kwa mfano, au insha, walikuwa chini ya himaya ya wahariri na wachapishaji pia. Ilikuwa ni kawaida kwa waandishi wa mashairi kuanza shairi kwa kumbembeleza mhariri asiwatupe kapuni.

Ukifanya utafiti kuhusu yule mwandishi wetu maarufu, Shaaban Robert, kwa mfano, utaona kuwa pamoja na kipaji kikubwa alichokuwa nacho, hakuwa na madaraka juu ya wachapishaji wake. Hali hii ya waandishi kuwategemea wachapishaji bado haijabadilika nchini Tanzania. Wachapishaji wameendelea kuwa kama miungu, na waandishi wanalalamika sana kuhusu wachapishaji. Malalamiko ni ya namna nyingi, kama vile kucheleweshwa taarifa kuhusu miswada, kucheleweshwa kuchapishwa miswada, kucheleweshwa malipo ya ruzuku ya uandishi, au kutolipwa kabisa.

Sio jambo jema kwa waandishi wetu kubaki na mtazamo tegemezi, tuliorithi tangu zamani. Dunia inabadilika. Mabadiliko hayo yapo pia katika uwanja wa uchapishaji vitabu. Maendeleo ya tekinolojia yamefikia mahali ambapo mwandishi anaweza kujichapishia vitabu vyake bila kutegemea wachapishaji.

Niligundua hayo miaka kumi na kidogo iliyopita, nilipokuwa tayari kuchapisha kitabu changu cha hadithi za waMatengo. Nilikuwa nimesikia na kusoma kuhusu kuwepo kwa tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Nilifanya utafiti, nikaona aina mbali mbali za uchapishaji huo. Hatimaye, niliamua kuchapisha kitabu changu kwenye kampuni mojawapo. Niliendelea kuandika, na papo hapo nikaendelea kufanya utafiti juu ya tekinolojia ya uchapishaji. Hatimaye, nikagundua kampuni iliyonivutia zaidi, na huko ndiko ninachapisha vitabu vyangu.

Ushauri wangu kwa waandishi wa Tanzania na kwingineko ni kuwa badala ya kukaa na kuendelea na jadi ya kuwalalamikia wachapishaji, watafakari suala la kujichapishia wenyewe vitabu vyao. Kitu cha msingi ni kuhakikisha mswada umeandikwa vizuri na kuhaririwa kikamilifu. Kwa kawaida, mswada unachapishwa mtandaoni kama ulivyoandikwa, hata kama una makosa. Hakuna huduma ya uhariri. Hii ndio tahadhari. Vinginevyo, kama mswada umeshakuwa tayari, uchapishaji unaweza kuchukua dakika chache tu, badala ya miezi au miaka, kama ilivyo sasa. Leo hii, kutokana na maendeleo ya tekinolojia, kila mtu anaweza kuchapisha kitabu chake.

No comments:

Post a Comment