LUGHA ya Kiswahili imezidi kupata mashiko baada ya kuwa moja ya lugha duniani zinazofundishwa katika mataifa zaidi ya 15. Katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kiswahili ni lugha rasmi baada ya kukubalika na kupitishwa na Bunge la Afrika Mashariki.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC), Profesa Kenneth Simala, alisema ni jambo jema kuona Kiswahili kikiungwa mkono na mataifa ya kigeni duniani.
akaongeza kuwa mafanikio ya Kiswahili katika nchi zilizo nje ya Afrika Mashariki, yatategemea juhudi zinazofanywa na nchi za Afrika Mashariki, ambako ndio nyumbani kwa lugha hiyo adhimu duniani.
“Maamuzi ya Bunge la Afrika Mashariki ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, yanalazimisha nchi zote wanachama kuwa na sera ya Kiswahili ambayo itaangazia maendeleo ya lugha hiyo katika nchi husika,” alisema Simala.
Alisema maamuzi mengine yaliyofanywa na chombo muhimu katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni yale yaliyofanywa na baraza la mawaziri ya kuzitaka nchi zote wanachama kuwa na mabaraza na vyama vya Kiswahili. Hatua hii itasaidia kuratibu maendeleo ya lugha ya Kiswahili pamoja na kuandaa wataalamu wa lugha.
Kupitia mabaraza na vyama vya Kiswahili, serikali itakuwa na fursa ya kuchukua walimu walioiva, ama kufundisha ndani ya nchi, au kufundisha nje ikihitajika. “Kinachotakiwa sasa ni kwa marais wa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuonesha nia ya dhati ya kukuza lugha ya Kiswahili, hali ambayo itaongeza kasi ya ukuaji wa lugha hii ndani na nje ya Afrika Mashariki,” aliongeza Simala.
Aidha, Simala alisema kuna haja ya kuwa na ushirikiano wa hali ya juu kati ya nchi na nchi katika kuendeleza lugha ya Kiswahili. Hali hiyo itasaidia kupenyeza Kiswahili hata katika maeneo ambayo yalikuwa magumu kupitisha lugha hii.
Simala alizitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zisaidie kuendeleza Kiswahili, kwa kuandaa wataalamu wa lugha kwa sababu maendeleo ya lugha yoyote, yanataka uwepo wa wataalamu wa lugha husika.
Ili kuepuka kupata wataalamu feki, ambao badala ya kutoa mchango wa kuendeleza Kiswahili, badala yake wanasaidia kudidimiza lugha hiyo, nchi zinazoinukia katika Kiswahili zinashauriwa kushirikiana na nyingine zilizoendelea katika lugha hiyo ili kupata wataalamu wenye uwezo wa kusaidia katika ukuzaji wa lugha.
Mbali na Afrika Mashariki, Kiswahili kimezidi kupata mashiko katika nchi mbalimbali barani Afrika na duniani, kutokana na kutumika kama lugha ya kufundishia.
Nchi hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Cameroun, Afrika Kusini, Madagascar, Misri, Ghana na Nigeria kwa upande wa Bara la Afrika. Katika Bara la Asia Kiswahili kimepata bahati ya kutumika kama somo katika nchi za Urusi, China, Japan, Korea, Iran na India wakati katika Bara la Ulaya lugha hiyo inatumiwa Ujerumani, Ufaransa, Uingereza Italia na nchi nyinginezo za ulaya katika vyuo na vituo mbalimbali vya kujifunzia lugha.
Rwanda imeridhia lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi sambamba na Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza. Hivyo, Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya nne katika taifa hilo, na kitatumika katika mawasiliano ya kiutawala.
Dhamira ya kuifanya lugha adhimu ya Kiswahili kuwa rasmi na ya kipekee ndani ya (EAC) inaelekea kutimia, baada ya nchi nyingine ndani ya jumuiya, Sudan Kusini kuifanya lugha rasmi ya kufundishia shuleni. Na katika kuhakikisha inatimiza azma hiyo, Serikali ya Sudan Kusini inakusudia kuingia mkataba ya Tanzania ili iweze kupatiwa walimu wa kufundisha Kiswahili nchini humo.
Nchini Burundi, Kiswahili kimepitishwa kuwa lugha rasmi na serikali ya nchi hiyo imetangaza ajira za walimu wa Kiswahili zaidi ya 1,000, ambapo inahitaji wapewe mafunzo na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.
Nchini Afrika Kusini, serikali imeingiza lugha ya Kiswahili katika mitaala ya shule za nchi hiyo ili kuwezesha kufundishwa shuleni. Lengo la nchi hiyo ni kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika mawasiliano.