UTANGULIZI
Katika makala haya, nitaeleza umuundo na umuundoleo, tofauti kati ya umuundo na umuundoleo na hitimisho.
Huwezi kuzungumzia nadharia ya umuundoleo bila ya kuhusisha umuundo. Kwa maana hiyo nadharia hizi huzungumziwa kwa pamoja
NADHARIA YA UMUUNDO
Umuundo ni nadharia inayojibainisha kwa kuangalia Ujumla wa uhusiano wa sehemu moja kwa nyingine katika kufanya kitu kizima. Kwa mfano muungano wa maneno hufanya sentensi na sentensi zikiungana zinaunda aya au onesho na onesho kuunda tamthiliya.
Ntarangwi, M (2004) anasema kuwa umuundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi.
Katika miaka ya kwanza ya karne ya 19, mwanaisimu Ferdinard De Saussure aliyezaliwa tarehe 26 Novemba 1857 huko Geneva, Switzerland alikuwa mwanafalsafa na mwanazuoni wa Ki-swiss aliyejishughulisha sana na isimu, alipendekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. Aliiangalia lugha kutoka mfumo rasmi hadi mfumo wa kinadharia. Kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo.
Alizua istilahi `parole'(utendaji) na `langue' (lugha) kwa mujibu wa maelezo yake anasema langue ni sehemu inayowakilisha welewa wetu wa uhusiano uliopo kati ya sauti na maana . anaeleza kuwa lugha ni alama ambayo imeunganisha kati ya kitajwa na kitaja. Kwake amesema alama ni dhana pana na ina pande mbili yaani mtajo (kitu kilichotajwa) na kitajwa (dhana).
Kwa mujibu wa de Saussere ‘parole’ ‘(utendaji katika lugha) huhusu msemaji kwa ujumla katika matumizi yake au uzungumzi ni lugha katika matumizi. Kazi hii ya Saussure ndiyo iliyozaa mkondo unaojulikana hivi sasa kama umuundo. Muundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi. Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao.
Katika miaka ya 1950, mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-Strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii . Hasa alichotaka kuendeleza dhana, kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na cha ndani (deep). Kwa ujumla twaona usomi wa kuitizama jamii kwa uwili unaokinzana (binary opposition) ambao ulisambaa katika nyanja nyingi hapo baadae.
Awali ya hapo, anthropolijia ilizingatia makundi au makabila maalum ya watu ambayo yalizingatiwa kivyao, mifumo ambayo ilidhaniwa kwamba haibadiliki, lakini Levi-strauss alijishughulisha na mifumo inayohimili jamii zote. Strauss alidai kwamba pana muundo maalum ambao waweza kutumia kueleza jamii zote za ulimwengu, kama vile ilivyo na somo la hisabu au la uchumi ambapo pana njia (formula) ambayo yaweza kueleza maswala mengi katika somo hilio. Hapo ndipo dhana za umuundo zilipoingia masomo mbali mbali hasa yale ya sayansi ya jamii na fasihi. Saussure alitoa maelezo ya nadharia changamano kuhusu lugha, na ni misingi ya nadharia zake inayotoa nguzo ya mbinu za umuundo, ( Ntarangwi, 41: 2004).
Ingawa huwa tunatumia lugha kuzungumza kuhusu maisha, Saussure hakulizingatia jambo hilo bali alisisitiza kwamba lugha ni kiungo kamili kinachojisimamia. Kwamba ni kiungo kilicho na masharti na sheria zake. Hivyo basi kuwepo kwa vitu duniani hakuathiri aina ya lugha iliyopo. Isitoshe, alidhamiria kudai kwamba lugha kwa kujisimamia haibadiliki wala vipande vyake haviathiriwi na mabadiliko yoyote ya kijamii.
Katika mkabala huo, neno ni ishara huru inayoelezwa kwa kutofautishwa na nyengine. Lugha ni mfumo wa uhusiano kati ya viungo kadhaaa vinavyoijenga; ni muundo, sio kitu. Dhana hii yaweza kueleweka zaidi tukizingatia maneno ya Saussure ya `kionyeshi' na `kinachoonyeshwa'. Neno katika lugha ndilo `kionyeshi' na dhana inayorejelewa ni neno hilo ndiyo `kinachoonyeshwa'. Kwa mfano neno mtoto ndio kionyeshi picha ya mtoto kama kirejelewa ndio kinachoonyeshwa.
Vyote viwili haviwezi kutenganishwa, lakini umuundo hujishughulisha zaidi na uhusiano wa vionyeshi na jinsi vinavyofanya kazi kuliko kuangalia nje ya mfumo wa lugha, yaani kinachoonyeshwa. Kwa msingi kabisa, Saussure alizingatia zaidi mpangilio wa ndani wa lugha, ule muundo wake na sio mahusiano ya vipande vyake. Wahakiki wanooegemea mkondo wa Saussure huzingatia kwamba matini husika ni mfumo unaojisimamia na hivyo basi huwa hamna haja ya kutumia mambo ya nje ili kuhakiki kazi ya fasihi. wahakiki huzingatia matini kama kiungo kamili kinachoweza kuhakikiwa kivyake. Hivyo basi mhakiki wa umuundo hujaribu kuweka sarufi ya matini pamoja na sheria za jinsi matini hiyo hufanya kazi. Mhakiki anayezingatia zaidi muundo wa lugha ya matini bila shaka hupuuza dhana ya jadi kuhusu kile matini hiyo huweza kutueleza kuhusu maisha; na hivyo basi hufanya mtindo wa kazi yenyewe kiini cha uhakiki wake.
Kwa hivyo wahakiki wanaotumia nadharia ya umuundo hujaribu kuzingatia matini pekee huku wakiepuka kuifasiri kazi ile kulingana na kaida zilizowekwa kuhusu jinsi matini hufanya kazi. Hata hivyo, huenda njia hii isiwe ya kufaa sana kwa sababu huwa inachukulia kwamba kila kitu kimeundwa katika mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine yaliyo nje yake. Ama kwa hakika, hata lugha yenyewe haiwezi kabisa kufanya kazi bila kuathiriwa na mambo mengine kama vile mazingira yake
Wakakiki wa muundo walichunguza upatanishi wa sauti, kiimbo, arudhi na utunzi wa maashairi wanaamini matini ya kifasihi huwa na viwango mbalimbali. Mhakiki anachunguza vipengele hivi kwa viwango tofauti tofauti.
Mkondo huu wa mawazo ya umuundo kuhusu sayansi za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali (duniani) kama vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi na Sasiolojia.
Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Kwa hiyo hata katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake.
Katika kupata maana lazima kuwe na uhusiano wa kipembetatu yaani kuna DHANA, ALAMA na KITAJWA.
Upungufu wa nadharia hii ndiyo uliochochea kuzuka kwa Umuundo- mpya.
NADHARIA YA UMUUNDOLEO
Umuundoleo hutumiwa kuelezea mikabala ya uhakiki iliyozuka kuyapinga au kuyaendeleza mawazo yaliyokuwa kwenye umuundo.
Tunatumia neno Umuundoleo kuonyesha mtizamo wa kimuundo katika fasihi ambao ulitokea baada ya Umuundo. Japo dhana hii haiwezi kupewa maana moja maalum, imehusishwa na maendeleo kutoka au katika kazi za Derrida (1973, 1976), Lacan (1977), Kristeva (1981, 1984, 1986), Althusser (1971) na Foucault (1978, 1979a na b, 1981, 1986). Kazi hizi nazo zilichangiwa na kazi za Ferdinand de Saussure na Emile Benveniste (kuhusu isimu-jamii ya umuundo), kazi ya umarx hasa kupitia nadharia ya itikadi iliyoendelezwa na Louis Althusser, na kazi ya tathimini-nafsi ya Sigmund Freud na Jacques Lacan.
Kazi hizi zimetoa athari mbali mbali kwa nadharia tofauti lakini zote zinazingatia makisio sawa kuhusu lugha, maana, na ubinafsia (subjectivity). Lugha yachukuliwa kama nguzo maalum ya uainishi wa mpangilio wa jamii, maana za kijamii, nguvu na urazini wa kibinafsi. Hii ni kwa sababu ni katika lugha ambapo maana za mpangilio wa jamii na matokeo yake ya kisiasa na kijamii hujengwa na kupingwa.
Ni kupitia lugha ambapo hisia na maana yetu ya kibinafsi (ambayo inatufasili) hujengwa. Aidha, lugha haielezi ubinafsi wa kipekee wa mtu bali hujenga ubinafsia wa mtu kwa njia zilizojengeka katika miundo ya jamii yake. Katika Umuundo-leo, ubinafsia sio hali yenye umoja au isiyobadilika, bali hubadilika kila mara ili kuchukuana na hali halisi ya kihistoria na kisiasa ili kudumisha nafasi ya mhusika katika jamii.
Umuundo-leo, kama nadharia nyinginezo ina makisio fulani kuhusu lugha, ubinafsia, ufahamu, na ukweli. Nguzo zake, ambazo zatokana, kama tulivyotaja hapo juu, na mwanaisimu wa kiimuundo Ferninard de Saussure, ni kwamba lugha, badala ya kudhihirisha uhalisi wa kijamii uliopo, huwa yatujengea uhalisi huo wa kijamii. Kwa hivyo sio uhalisi wa kijamii wala ulimwengu asilia huwa na maana zinazodhihirishwa ni lugha. Lugha mbali mbali pamoja na matumizi mbali mbali ya lugha moja huugawa ulimwengu na kuupa maana kwa njia tofauti ambazo haziwezi kupatana ili kuunda kigezo kimoja kinachodhihirisha uhalisi wa jamii. Kwa mfano, maana ya tajiri hutofautiana katika lugha mbali mbali na hata kati ya miundo tofauti ya lugha moja, na hutegemea matumizi na muktadha wa matumizi hayo. Ndipo sasa hapana maana moja ya neno au fungu la maneno.
Miundo yote ya umuundo-leo huchukulia kwamba maana hujengwa katika lugha na huwa yule anayezungumza lugha hiyo hawezi kuhakikisha maana hiyo. Kwa hivyo tofauti na maoni ya Saussure, maana huzaliwa na kuundwa kwa njia mbali mbali.
Hata hivyo nadharia hii hukubaliana na wazo lake kwamba lugha haimuliki maana; bali maana hukuzwa katika lugha na kwamba ishara hazina maana ya kivyake bali hupata maana katika mkururo wa lugha pamoja na tofauti yake na ishara nyingine. Dhana hii ni muhimu sana kwa sababu yadhihirisha lugha kama chombo cha kijamii ambacho chapingwa na kung'ang'aniwa.
Kulingana na nadharia hii basi, neno 'mama' kwa mfano, huwa halina maana ya kindani inayotokana na lugha husika bali huwa na maana za kijamii zilizotokana na lugha hiyo na ambazo zinakinzana na kubadilika kulingana na mazingira na kipindi cha kihistoria.
Kwa hivyo kinyume na maoni ya wanamuundo kama vile Levi-Strauss walioshikilia kwamba maana ya kisa, kwa mfano, ipo katika matini na maana hiyo hiyo hutokea katika matini nyengine yoyote, nadharia hii yaeleza kuwa maana ya kisa ni amali ya msomaji/msikizi (hadhira) na kwamba pana fasili mbali mbali za kisa hicho kulingana na muktadha. Hivyo basi kwa umuundoleo twaweza kueleza kuwepo kwa wingi wa maana pamoja na mabadiliko yake kwa kuona maana sio kama iliyojengwa katika ishara zisizobadilika bali kama iliyo katika viashiria (signifiers) ambapo kiashiriwa (signified) hubadilikabadilika. Hapo ndipo alipojikita Derrida ambaye aliingiza
dhana ya muktadha katika kueleza maana katika lugha na matini. Wahakiki wanaozingatia nadharia hii basi huongozwa na dhana ya kubadilika kwa maana katika miktadha mbali mbali na hivyo basi kuwashurutisha kuzingatia muktadha wa kazi hiyo kama nguzo ya kueleza kazi hiyo. Mtaalamu huyu anazuka na dhana maarufu ya utofauti (difference), kwa maoni yake maana hutokana na mikakati au mbinu mbili muhimu, ‘tofauti’ (difference) na ‘uahirisho’ Wamitila (2002:179 ) anaiita kuwa ni tofahirisho ambalo linafumbata dhana mbili hizi.
Wanamuumo wanaangalia muktadha wa kiusemi au kimazungumzo na huweza kubadilika kutegemea mukatadha wa kiusemaji. Ikiwa muktadha wa kiusemi utabadilika maana nayo inabadilika.
TOFAUTI KATI YA MUUNDO NA UMUUNDOLEO