Wakati lawama nyingi zikiangukia kwa mlinda mlango wa Yanga, Mcameroon, Youthe Rostand wakati ligi ya msimu uliomalizika ikielekea mwisho, uongozi wa Yanga umeanza harakati za kumpata mbadala wake, imeelezwa.
Ukiachana na Kamati ya Utendaji pamoja na Usajili ndani ya Yanga kusema inaendeleza usajili wake wa kimyakimya ili kutopigiwa chapuo na baadhi ya timu ambazo zimekuwa zikisubiri Yanga itaje wachezaji kisha isajili, sasa wameanza mazungumzo na Deo Munish.
Deo Munish maarufu kama Dida, ameanza kufuatiliwa na mabosi wa Yanga kuja kuhakikisha anachukua nafasi ya Rostand ambaye ameonekana kushuka kiwango kiwango chake tofauti na wakati akianza kuitumikia klabu hiyo.
Mchezaji huyo ambaye anasakata kambumbu lake katika klabu ya Chuo cha Pretoria, Tucks FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Afrika kusini, ananyatiwa kuhakikisha anarejea jangwani kuchukua nafasi yake.
Dida aliondoka Yanga baada ya mkataba wake kumalizika na kuelekea huko Afrika Kusini baada ya kucheza kwa mafanikio akiwa na mabingwa hao mara 27 wa ligi kuu bara.