KUWA NA VIPINDI VINGI VYA HEDHI NA KUWA NA VIPINDI VICHACHE KWENYE HEDHI
POLYMENORRHEA & OLIGOMENORRHEA
Kwa kawaida mzunguko wa hedhi huchukua siku 21 mpaka 35 lakini wastani wa wanawake wengi huenda siku 28 kama inavyotumiwa katika vitabu vingi.
Kama mwanamke anaenda mzunguko wa siku 21 basi katika mwaka wenye siku 365 ataenda mizunguko 17 (365/21=17) na yule mwenye mzunguko wa siku 35 atakuwa na vipindi 10 vya hedhi( 365/35=10) katika mwaka
Nini husababisha kuona vipindi vingi katika mwezi(polymenorrhea)?
Kuna sababu mbalimbali, zipo sababu za kawaida zisizo za hatari kama msongo wa mawazo, mazoezi makali, matumizi ya dawa mbalimbali na matatizo ya mwanamke akiwa anaanza kuacha kuona siku zake. Sababu zingine ni matatizo/magonjwa kwenye mfumo wa uzazi. Baadhi ya sababu hizo zimeelezewa hapo chini.
- Kuharibika/kutokuwepo kwa uwiano wa vichochezi mwili
Hili linaweza kusababishwa na mambo mbalimbali kama vile chakula unachokula endapo hakina virutubisho vya kutosha, kubadili chakula, kubadili mfumo wa maisha ya kila siku na kubadili ratiba ya kulala kila siku.
Tatizo hili huweza kuwa kubwa na kusababisha mwanamke kuongezeka uzito kubadilika tabia na hulka yake kuhalibika, ni vema kupata ushauri na msaada wa kiafya endapo hili litatokea.
- Kujipandikiza nje ya kizazi kwa chembe za ukuta wa ndani ya mfuko wa kizazi(endometriosis)
Chembe za ndani ya uzazi huweza kujipandikiza katika mayai, nje ya misuli ya mfuko wa kizazi, kwenye mirija ya kupitisha mayai n.k. kuwepo kwa chembe hizi nje ya kizazi husababisha kuvuja kwa damu ya hedhi ndani na madhara yake ni michomo na kushikamana kwa organi ndani ya nyonga. Mwanamke anapata dalili za maumivu makali wakati wa hedhi pamoja kuwa na vipindi vingi vya hedhi katika mwaka.
- Vimbe kwenye ukuta wa uzazi(uterine Fibroids)
Kuwepo kwa vimbe ndani ya ukuta wa kizazi huufanya ukuta unaotengenezwa kila mwezi (kwa ajili ya kupokea yai endapo limechavunshwa)kutokuwa imara na hivo husababisha ukuta huu kuvunjika kabla ya mzunguko kukamilika na mwanamke anakuwa na vipindi vingi vya hedhi.
- Kuanza kukoma kwa Mzunguko wa Hedhi (perimenopause)
Kukoma kwa mzunguko wa Hedhi ni jambo la kawaida kwa mwanamke anapofikia umri zaidi ya miaka 45. Dalili zake ni kama kutokwa na jasho wakati wa usiku, kubadilika kwa tabia au hulka ya mtu na kuwa na vipindi vingi vya hedhi katika mwezi. matatizo haya huletwa kutokana na mabadiliko ya vichochezi mwili(hormone) yanayotokea kwa mwanamke anapokuwa anazeeka.
- Magonjwa ya zinaa
Ni yapi matibabu ya tatizo hili?
Tatizo la kuwa na vipindi vingi vya hedhi huweza kutibiwa endapo sababu imejulikana ni nini, kama tatizo ni msongo wa mawazo, dawa za mpango wa uzazi,mazoezi makali, uzito na mengine, matibabu yake ni kukabiliana na mambo hayo. Na endapo utaenda hospitali basi utapimwa vipimo mbalimbali na kutibiwa tatizo lako.