Sunday

KAMA ULIVYO SIKIA YANGA WAMECHEZEA TENA HUKO KENYA

0 comments

NAKURU, Kenya -Mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga, wameondolewa kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-1 kutoka kwa timu ya Kakamega Homeboyz kutoka nchini Kenya.
Mabao mawili ya mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Allan Wanga na moja la kipindi cha pili kutoka kwa Wicklif Opondo yalitosha kuizamisha meli ya wana jangwani hao ambayo ilikosa mahali pa kutia nanga licha ya kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Matheo Anthony.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa utulivu wa aina yake huku kila timu ikijaribu kusoma mbinu za mpinzani wake kwa ukaribu lakini walikua ni Kakamega Homeboys walioanza kufika langoni mwa Yanga licha ya mashuti yao kushindwa kulenga lango
Yanga nao walijibu mapigo kwa kufanya mashambulizi kupitia kwa Juma Mahadhi, Baruad Akilimali lakini hata hivyo mabingwa hao mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania bara walishindwa kutikisa nyavu za wapinzani wao.
Dakika ya 27, Mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na beki Haji Mwinyi ulishindwa kupenya ukuta wa Kakamega huku Tshishimbi akishindwa kuunganisha vyema mpira uliorudishwa na ukuta wa Kakamega.
Wangá angáa
Alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Allan Wanga aliyefunga goli la uongozi kwa upande wa Kakamega mnamo dakika ya 20 ya mchezo baada ya kuunganisha vyema krosi ndefu iliyopigwa kutoka katikati ya uwanja kwa shuti la kubetua lililomzidi maarifa nyanda wa Yanga, Youthe Rostand.
Allan Wanga (11) akishangilia moja ya mabao mawili aliyofunga dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa robo fainali ya SportPesa Super Cup (Picha-SPN)
Huku wakitumia vyema makosa ya walinzi wa Yanga ambao walishindwa kujipanga, dakika 11 baadae, Allan Wanga aliiandikia Kakamega goli la pili kwa mkwaju wa penati baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na mlinzi wa Yanga, Haji Mwinyi.
Baada ya kufungwa magoli ya haraka haraka, Yanga waliibuka usingizi ambapo dakika ya 39 Matheo Anthony aliiandikia Yanga goli kwa kwanza baada ya kupiga mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja kufuatia mlinzi wa Kakamega kuunawa mpira sentimita chache kutoka eneo la hatari
Hadi mpira unakwenda mapumziko, Kakamega walikuwa mbele kwa mabao 2-1 huku mashabiki wa Yanga waliokuwa safarini, wakiwasili kwenye dimba la Afraha kwa hoi hoi, nderemo na vifijo licha ya timu yao kuwa nyuma.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ambapo alitoka Baruan Akilimali na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Ajib ambapo dakika moja baadae chupu chupu Kakamega wapate bao la tatu baada ya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa langoni mwa Yanga kushinda kuzuiwa licha ya mlinda mlango Youthe Rostand kuwa makini kuzuia hatari hiyo.
Yanga walifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Amis Tambwe na Yusuph Mhilu lakini tatizo la kupoteza pasi liliendelea kuwatafuna na hivyo kuwapa Kakamega nafasi ya kushambulia mara kwa mara kwa mipira ya kushtukiza.
Msumari wa mwisho
Ni mashambulizi hayo ya kushtukiza ambayo yaliipatia Kakamega goli la tatu dakika ya 81 baada ya mchezaji aliyeingia kutokea benchi, Wicklif Opondo kupasia nyavu akimalizia pasi kutoka magharibi ya uwanja baada ya mlinda mlango Youthe Rostand kutoka langoni na kuukosa mpira.
Kakamega hawakuridhika na magoli hayo kwani waliendelea kulishambulia lango la Yanga kama nyuki na dakika ya 87 nusura wapate bao la nne lakini shambulizi lao liligonga mwamba
Hadi dakika 90 zinamalizika kwenye dimba la Afraha, Kakamega walitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 3-1 na kuiondosha Yanga kwenye michuano hiyo ikiwa pia ni timu ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali