Mwalimu yeyote anapaswa kujifunza utengenezaji na matumizi ya zana, kwani ni nyenzo muhimu sana katika kazi ya kufundisha na kujifunza.
Nini maana ya Zana za Kujifunzia na Kufundishia?
“Zana ni kitu chochote kinachopangwa na kutumika katika kuinua kiwango cha elimu”.
Je, mwalimu anaweza kuwa Zana?
NDIYO, Mwalimu pamoja na vifaa vingine anaweza kuwa zana kwa sababu vifaa vya kufundishia pamoja na mwalimu vimepangwa na kutayarishwa kwa madhumuni ya kuboresha tendo la kujifunza na kufundisha.
Je, unadhani Mwanafunzi anaweza kujifunza pasi kuwa na Mwalimu?
NDIYO, Mwanafunzi anaweza kujifunza kwa kutumia zana pekee bila ya mwalimu (Resource-based learning) lakini mwalimu atashindwa kufundisha bila ya mwanafunzi ingawa anazo zana za kufundishia.
JIPIME
Mwalimu anaposimama mbele ya darasa na zana zake, Je, madhumuni na lengo lake ni kuinua kiwango cha wanafunzi kujifunza au kuinua kiwango chake cha kufundisha?
KUMBUKA
Lengo hasa la kutumia zana katika kufundisha ni kukuza na kuinua kiwango cha kujifunza cha mwanafunzi.
Aina mbalimbali za Zana za Kujifunzia na Kufundishia
Zana za Kufundishia na Kujifunzia zimegawanyika katika makundi matano (5);
- Vitu Halisi
Kutokana na mpangilio wa piramidi, vitu halisi ni bora zaidi kwa Kufundishia kuliko kifaa cha aina nyingine ile.
Kwa kutumia vitu halisi mwanafunzi anajifunza kwa udadisi, kuchunguza, na kugundua. Pia vitu halisi vinampa mwanafunzi nafasi kubwa ya kujifunza kwa vitendo na kutumia milango mingi ya fahamu kwa wakati mmoja. Katika Piramidi vitu halisi vimewekwa kwenye kitako cha piramidi kuonesha umuhimu wa utumiaji wa vitu halisi wakati wa kujifunza na kufundisha.
- Bandia/Maumbo (Model)
Kwa ukosefu wa vitu halisi, maumbo/vitu bandia huchukua nafasi ya pili. Mwanafunzi anapata kuona, kusikia, kuhisi kana kwamba anatunmia vitu halisi. Bandia ni igizo la vitu halisi, hivyo huchangia iasi Fulani cha ukweli.
- Televisheni, Video na Sinema
Televisheni inachangia katika kuonesha vitu kama vilivyo, kwa hali hii kuna ukweli ndani ya televisheni. Televisheni inamwezesha mwanafunzi kusikia na kuona matendo wakati ule ule yanapofanyika.
- Chati, Picha, Mabango, Grafu na Ramani
Zana hizi hutoa mawasiliano ya kuona tu. Mwanafunzi anajifunza kwa kutumia macho yake tu.
- Radio, Santuri, Tepu-Rekoda
Zana hizi humsaidia mwanafunzi kujifunza kwa kusikia. Vipindi maalum hutayarishwa kwa ajili ya shule au wanafunzi wanaosoma kwa masafa.
JIPIME
Toa sababu ya mpangilio wa zana za kujifunzia na kufundishia kupangwa kwa umbo la piramidi.
Mgawanyo wa Zana za Kujifunzia na Kufundishia
Zana za Kujifunzia na Kufundishia zinaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili (2);
Zana za Ziada
Hizi ni aina ya zana zinazomsaidia mwalimu kuchapuza somo lake. Kwa kutumia zana za ziada mwanafunzi hapati fursa ya kujifunza kwa vitendo yale mambo anayojifunza, bali mwanafunzi hubaki kusikiliza tu. (mfano radio, tepu rekoda na santuri).
Zana Unganishi
Hizi ni aina ya zana zenye msaada mkubwa wakati wa ufundishaji. Zanan unganishi hazimsaidii mwanafunzi katika kujifunza tu bali zinamsaidia mwanafunzi kufanya kwa vitendo yale anayojifunza.
Asante kwa kusoma masshele blog