Thursday

UDSM NEWS :MAFANIKIO YA SERIKALI YA DARUSO 2017/2018 CHINI YA JILILI JOHN JEREMIAH

0 comments


MAFANIKIO YA SERIKALI YA DARUSO 2017/2018 CHINI YA JILILI JOHN JEREMIAH
Awali ya yote ni imani yangu kuwa wana Daruso au wanafunzi wenzangu wa chuo kikuu cha Dar es salaam ni wazima wa afya na mnaendelea vyema katika utekelezaji wa majukumu yenu.
Pili nikiwa kama mwana daruso niliepata uhalali kupitia katiba ya daruso ya 2012 ibara ya 9(1) na pia kwa kutimiza matakwa ya katiba hiyo ya daruso ibara ya 9(2). Hivyo kama mwana daruso halali nimeona ni vyema kutumia haki yangu niliyopewa kupitia ibara ya 10(VI) (C) ya kutoa maoni au kueleza fikra zangu na mawazo yangu binafsi dhidi ya Daruso au uongozi wa daruso.Ni fikra hii au tafakuri hii imejikita katika kuchambua utendaji wa viongozi wetu hawa ambao tuliwapa dhamana ili kututumikia ikikumbukwa kuwa uongozi huu unaelekea kwenye ukomo wake hivyo ni vyema kuchambua utekelezaji wao namna walivyowajibika katika uongozi wao hasa kwa kuangazia mihimili yote mitatu ya daruso yaani serikali ya daruso,bunge la daruso(USRC) na mahakama ya daruso.Na leo nitaanza na mhimili wa serikali ya daruso chini ya mh Rais ndugu Jeremiah Jilili ambae ndie kiongozi mkuu wa Daruso 2017/2018 kwa mujibu wa madaraka yaliyokasimiwa kwake kupitia katiba ya daruso 2012 ibara ya 16(I)(II) pamoja na ibara ndogo ya 2 ya ibara hiyo. Baada ya kufuatilia kwa kina na kuwahoji baadhi ya wana daruso nimebaini kuwa serikali hii imetekeleza mambo makubwa kwa wana Daruso yaliyonipelekea kuandika waraka huu kutokana na kuguswa na utendaji uliotukuka wa serikali hii chini ya Rais wake ndugu Jeremiah Jilili.
Baada ya kusema hayo sasa nijikite kwenye kiini cha waraka huu ambayo ni matokeo ya tafakuri yangu ya kina dhidi ya serikali hii. Rais wa awamu ya 16 wa marekani Abraham lincolin aliepata kutawala taifa hilo kubwa duniani miaka ya 1861 -1865, wakati akitoa falsafa yake juu ya demokrasia aliwahi kusema ‘’ Democracy is the government of the people by the people for the people’’ akiwa na tafsiri kuwa demokrasia ni serikali ya watu iliyopata mamlaka kutoka kwa watu kwa ajili ya kuwatumikia watu, hivyo kwa mujibu wa falsafa hii ya lincolin tafsiri ya serikali dhabiti au kipimo cha kufanikiwa au kutofanikiwa kwa serikali yoyote ni namna serikali hiyo ilivyowajibika kikamilifu kujihusisha na utatuzi wa kero za watu wake na serikali hii hakika imetekeleza haya kikamilifu chini ya uongozi thabiti wa mh Rais Jeremiah Jilili. Waswahili wanamsemo usemao ‘’mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’’ “na ukiona vyaelea basi ujue vimeundwa” hivyo ndugu Jilili na serikali yake hakika wanastahili pongezi.Baada ya kuyasema hayo nijielekeze moja kwa moja kuainisha mambo kadha wa kadha yaliyotendwa na serikali hii chini ya Rais Ndugu Jeremiah Jilili
1.Usaidizi wa usajili kwa wanafunzi 1800
Serikali hii ilifanikiwa kuwasaidia wanafunzi Zaidi ya 1800 waliopaswa ku-discontinue kwa sababu ya kuchelewa kujisajili nje ya utaratibu kwa mwaka wa masomo 2017/2018. Serikali hii ilisimama kidete kuwatetea wanafunzi hawa kwenye uongozi wa chuo na hivyo kufanikiwa kusajiliwa au kupata usajili hii ni hatua madhubuti na ya kuridhisha inayoakisi utendaji wa serikali uliotukuka kwa kujihusisha na utatuzi wa kero au shida za watu wake.
2.Ufunguzi wa Daruso Bar
Hili nalo ni moja kati ya mafanikio mengi yaliyoletwa na serikali hii chini ya mh Rais Jeremiah Jilili ambae alihakikisha anawajibika kikamilifu kutimiza ahadi yake kwa wana daruso alioitoa wakati wa kampeni ambapo suala hili la daruso bar lilikuwa kilio kikubwa cha wana daruso kwa miaka nenda rudi toka kufungwa kwa Bar hiyo takribani miaka minne iliyopita.Na suala hili la daruso bar limekuwa mjadala na mtaji wa kisiasa kwa serikali nne na baadhi ya viongozi kwenye majukwaa ya kampeni za siasa za daruso ila haikufanikiwa kurejeshwa kwa namna moja au nyingine mpaka ndugu Jeremiah Jilili aliposhika hatamu ya Urais wa Daruso alipambana kikamilifu kuhakikisha Daruso Bar inarejea kwa kuushinikiza uongozi wa chuo kuirejesha daruso Bar na katika hilo ndug Jeremia Jilili na serikali yake walifanikiwa na bar hiyo ikazinduliwa rasmi 2/3/2018 na kurejea tena kutokana na uwajibikaji wa serikali hii chini ya Rais Jeremiah Jilili na mpaka sasa inatoa huduma kwa wana daruso na kurejesha burudani iliopotea kwa takribani miaka minne.
3. Nipige tafu
Huu ni mfumo mpya ulioanzishwa au kuasisiwa na serikali hii chini ya Mh Rais ndugu Jeremiah Jilili kutokana na ubunifu,uthubutu,na utashi wa kiongozi huyu wa Daruso na serikali yake.Chini ya uongozi wake serikali ya daruso ilianzisha utaratibu wa wanafunzi kudhaminiwa na serikali yao hata kama hajasajiliwa hudhaminiwa na daruso kupitia form maalumu zinazoitwa Nipige tafu zilizokuwa zinatolewa ofisi ya Waziri mkuu Daruso zinazomwezesha mwanafunzi kupata fedha na kisha kulipa mahitaji ya msingi na kisha kusajiliwa na hapo baadae akishapatiwa fedha zake kurejesha kwenye akaunti ya chuo .Hii imechangia kupunguza usumbufu na adha kubwa wakati wa usajili haswa kwa wale wanufaika wa mkopo waliokuwa wakisubiri fedha hizo kutoka Bodi ya mikopo
4. Mikopo
Pia katika sekta hii serikali ya daruso imepambana kupigania idadi ya wanaonufaika na mikopo UDSM kuongezeka na kufikia jumla ya 13,898 hii ni kutokana na I) 13,596 walipata kutoka bodi ya mkopo , II) 222 wale mwaka wa kwanza ambao fedha zao zilifanyiwa miss-allocation ya chuo na kupelekwa kwingine lakini walisaidiwa na serikali hii na kupata fedha zao, III) 61 walipata kwa msaada wa daruso , IV) 19 walipata kutoka kwenye makampuni mbalimbali.Hakika hii ni tafsiri ya serikali inayoshughulika na shida za watu wake.
5.Cafteria za COICT na JPM hostel
Toka kuzinduliwa kwa hosteli hizo na kuanza kutumika rasmi hapakuwahi kuwapo na huduma za Cafteria na kusababisha kero kubwa kwa wanafunzi wakaazi wa hosteli hizo na sisi sote tulikuwa mashuhuda katika hilo kwa kusababisha wanafuzi hao wakaazi wa hosteli hizo kutembea umbali mrefu ili kupata huduma ya chakula lakini Rais wa Daruso ndugu Jeremiah Jilili na serikali yake walisimama kidete na kulivalia njuga suala hili kwa kupambana na urasimu uliopo ndani ya uongozi wa chuo na hatimae mwishoni mwa mwezi wa pili cafteria hizo zilifunguliwa kwa pamoja katika hosteli hizo na wanafunzi kupata huduma karibu na kutatua kero zilizokuwapo hapo kabla.
6.Ununuzi wa runinga (Tv)
Pia ukosefu wa runinga katika hosteli za mabibo ,coict,na magufuli kulikuwa ni changamoto kubwa na kero kwa wanafunzi wakaazi wa hosteli hizo hususani wale wapenzi au mashabiki wa mpira wa miguu waliokuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu haswa mida ya usiku kwenda kwenye bar na pub mbalimbali na bado kuingia gharama ili kuweza kuangalia mpira ila kwa sasa wanapata huduma hiyo kwenye hosteli zao za mabibo,magufuli na CoICT.Hosteli zote zimekabidhiwa runinga hizi mpya na za kisasa na mh Rais wa daruso ndugu Jeremiah Jilili,huu ni uthubutu wa aina yake unaotendwa na Rais huyu ndg Jeremiah Jilili japo fedha hizo za kununulia runinga zilitoka nje ya bajeti ya daruso ila zilikwenda kutumika kutatua kero za wana daruso waishio katika hostel za Magufuli na CoICT.
7.Kumalizwa kwa unyanyasaji wa wakaazi wa JPM hostel
Hii pia ni hatua mojawapo kati ya nyingi ambazo serikali hii chini ya Mh Rais ndg Jeremiah Jilili ilichukua ili kupigania usawa na haki kwa wana daruso waliokuwa wakinyanyaswa au kudhalilishwa haswa katika hosteli za Magufuli. Ikikumbukwa kuwa hosteli za Magufuli ni mpya na wanafunzi wakaazi wa hosteli hizo 2017/18 ambao zaid ya 95% ni wa mwaka wa kwanza hivyo baadhi ya sheria na taratibu za chuo walikuwa hawazifahamu kutokana na ugeni wao ndani ya chuo hiki hivyo sababu hii kupelekea kunyanyaswa kwa namna moja au nyingine na baadhi ya walezi na walinzi(Auxiliary Police) baada ya serikali ya daruso kupata taarifa hizi waliitisha kikao kilichowahusisha wanafunzi wakaazi wa hosteli hizo,walezi,pamoja na viongozi wa Daruso ambapo kikao hicho kilifanyika 6/1/2018 na wanafunzi walipata fursa za kutoa kero zao na miongoni mwa kero hizo ilikuwa ni pamoja na kuzuiwa kuingia hostelini hapo nje ya saa sita kamili usiku ambapo ni kinyume na By law kifungu cha 5.2 (I)-(XV),pili ni wanafunzi kupigishwa magoti na walinzi (Auxiliary Police),kunyimwa kuingia na chakula ndani ya geti na wengine vyakula vyao kumwagwa na walinzi hao,baadhi ya walezi kuchukua rushwa kwa wanafunzi na wengine kuwatoza wanafunzi faini kubwa kinyume na taratibu halali za chuo.Baada ya wanafunzi kutoa kero zao serikali ya Daruso chini ya Rais Jeremiah Jilili ilitoa tafsiri ya sheria za chuo pamoja na msimamo wao kama serikali ya wanafunzi na kuanzia siku ile hapakuwahi tena kutokea kwa kero hizo.Hii ni kutokana na utetezi wa serikali hii kwa watu wake pamoja na kusimamia misingi ya haki na sheria.
8.Mgawanyo sahihi wa fedha kwa ndaki,shule na taa sisi zote kwa mujibu wa bajeti ya Daruso 2017/2018
Pia serikali hii chini mh Rais ndugu Jeremiah Jilili ilihakikisha inaufuata na kusimamia utaratibu wa kutoa 30% ya bajeti yake kwenye ndaki,shule na taasisi zake kwa mujibu wa katiba ya Daruso hii yote ni kwa minajili ya utekelezaji wa ahadi,sera na dira ya serikali ya 2017/2018 kwa wana daruso na hii yote ni kutokana na usimamizi mzuri wa mh Rais ndug Jeremiah Jilili ambae alichukua hatua hiyo kwa lengo la kupunguza urasimu kwenye serikali yake katika kuwahudumia watu wake au wana Dauruso.
9. Michezo
Pia katika sekta hii serikali hii ya daruso chini ya ndg Jeremiah Jilili haikuwa nyuma ilishiriki kikamilifu kwa kuitisha na kuendesha mabonanza ikiwa na lengo la kuwaleta pamoja wana Daruso ikizingatiwa kuwa michezo ni afya,ajira na burudani. Na mabonanza hayo ni kama vile bonanza la Vodacom lililoleta jezi pair 4, mipira 4,na fedha taslimu sh laki nne(400,000/=) walizopatiwa washindi wa mpira wa miguu na basket ball,pia kulikuwa na bonanza la Haloteli nalo lilitoa jezi pair 4,fedha taslimu sh laki nne(400,000/=) na pia waliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni mbili(2,000,000/=) kwa ajili ya kuwalipia ada wanafunzi wa chuo hiki wenye shida mbalimbali.kupitia mabonanza haya yalipelekea wanafunzi kujiimarisha kimichezo na kuibuka washindi wa jumla kwenye mashindano ya TUSA huko Dodoma kuanzia tarehe 14-21/12/2017 na kupata medali 6 na vikombe 6.Ukiachilia hayo pia serikali hii chini ya ndugu Jeremiah jilili kwa sasa inaendesha mashindano ya michezo ya vitivo ambayo imeanza kutimua vumbi toka tarehe 15/4/2018 -22/4/2018 ambayo inahusisha soka kwa wanaume na mpira wa pete kwa wanawake ambapo mshindi wa kwanza kwa kila mchezo atapata sh laki tatu(300,000/=) na kikombe,mshindi wa pili ataibuka na sh laki mbili (200,000/=) mshindi wa tatu sh laki moja na nusu (150,000/=) pia mfungaji bora kwa kila upande ataondoka na sh elfu thalathini (30,000/=) vivyo hivyo kwa mchezaji bora na mlinda mlango bora. Na ikumbukwe kuwa michuano hii inafanyika kwa mara ya kwanza toka 2014 hivyo serikali hii chini ya mh Rais ndg Jeremiah Jilili amefanikiwa kuifufua michuano hii na kuirejesha tena Burundi kwa wana daruso iliopotea toka 2014.
10. Mengineyo
Pia serikali hii ya Daruso imefanikiwa kutekeleza mambo mbali mbali yenye tija na mlengo wa maendeleo kwa wana Daruso mathalani kupitia wizara ya katiba na sheria ya Daruso serikali hii imekuwa ikitoa msaada wa haraka sana pale wanafunzi wenzetu walipokuwa wakifikishwa au kupeleka mashauri yao mahakamani au polisi,pia kupitia wizara ya habari ya Daruso Serikali hii pia imekuwa ikitoa fursa kwa wanafunzi mbali mbali kuhudhuria na kushiriki vipindindi mbalimbali kama vile malumbano ya hoja,pia kupitia wizara ya elimu serikali hii ilifanikiwa kuitisha makongamano mbali mbali ya elimu yaliyopelekea wanafunzi wenzetu baadhi kupata scholarship na wengine kufadhiliwa masomo yao.
11.Ushiriki wa shughuli za kijamii
Chini ya uongozi wa mh Rais ndugu Jeremiah Jilili serikali ya Daruso siyo imekuwa tu ikiwajibika kwa watu wake bali pia imekuwa sehemu ya wana jamii wa taifa letu la Tanzania kwa kushiriki kwa namna moja au nyingine mfano serikali hii ilitoa tamko la kupongeza jitihada za makusudi zilizochukuliwa na mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli alipounda kamati za kuchunguza kiwango cha makinikia na pia serikali hii kupitia tamko hilo ilitoa ushauri wa mambo kadha wa kadha kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya katika sekta hiyo nyeti ya madini pamoja na nyingine kwa maslahi mapana Zaidi ya Taifa letu.Pia serikali hii imekuwa ikiungana na watanzania wote kupinga,kukemea,na kulaani vikali matukio ya kinyama yenye taswira mbaya kwa taifa letu kama kupigwa risasi kwa mh Tundu Lissu na Akwilina Akwilini mwanafunzi wa chuo cha usafirishaji NIT.
Lakini pia Serikali ya JILILI JEREMIAH JOHN iliweza kukusanya Rambirambi za ajali ya watoto wa lucky Vicent iliyotokea mkoani Arusha tarehe na kufanikiwa kukabidhi 2000000 za kitanzania na pia serikali hii chini ya mh Rais ndg Jeremiah Jilili alifanikiwa kuanzisha ushirikiano na viongozi mbali mbali kama Poul Makonda Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Mama Mariah Nyerere mjane wa baba wa taifa.
12. Umoja na mshikamano
Katika hili hakika serikali hii chini ya ndg Jeremiah Jilili inastahili pongezi za dhati kwakuwa imekuwa ikihimiza umoja na mshikimano kwa wana Daruso wote kama kauli mbiu ya serikali inavyosema “united we stand, divided we fall” na matokeo yake wana daruso tumekuwa kitu kimoja kama familia licha ya tofauti mbali mbali tulizokuwa nazo.
Baada ya kusema hayo hakika nitoe shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Daruso ndg Jeremiah Jilili na serikali yake hakika kiongozi huyu atakuwa Rais wa kukumbukwa na jumuiya hii ya wasomi kwa namna alivyoshughulika kikamilifu kutatua kero za wana Daruso waliomwamini na kumpa dhamana ya kuwaongoza. Ndg Jilili ametuonyesha kuwa sifa ya kiongozi bora ni kuleta mabadiliko chanya kwa jamii anayoiongoza, waingereza wana msemo usemao “ Leaders are there to bring positive changes to their people” na hiki ndicho ndg Jilili alichokifanya na hakika katika hili anastahili pongezi kwa kila mwana daruso ambae ni mdau wa maendeleo. Viva Jeremiah Jilili utakuwa Rais wa kukumbukwa na wana Daruso nyakati zote kwa alama za matokeo chanya ulizozitia kwenye mioyo yao.
Licha ya juhudi hizo na mafanikio hayo kuna mambo kadha wa kadha yalikuwa changamoto kwa serikali hii na kiongozi huyu maana waswahili wana msemo usemao “penye mafanikio hapakosi changamoto” hivyo eiza Ndg Jilili au serikali yake ilikwaana na kikwazo katika kuwaletea maendeleo wana Daruso kama vile urasimu au ukiritimba kwenye uongozi wa chuo haswa pale viongozi hawa walipokuwa wakiwasilisaha kero mbali mbali zinazowakumba wana Daruso zimekuwa zikichukua muda mrefu kufanyiwa ufumbuzi na uongozi wa chuo mfano Barabara ya kuelekea hosteli za magufuli ambayo imekuwa kero kubwa haswa kipindi cha mvua, mh Rais ndg Jilili na serikali yake wamekuwa wakilipigia kelele suala hili kwa uongozi wa chuo lakini limechukua muda bila kushudgulikiwa.
Wako mwana Daruso,Mchambuzi,mfuatiliaji na mkereketwa Wa siasa za DARUSO
“UNITED WE STAND, DIVIDED WE FALL”