NI takriban miaka 46, bado Wazanzibari na Watanzania kwa jumla, wanamkumbuka kiongozi mahiri na shujaa, Hayati Abeid Amani Karume.
Huyu ni kiongozi aliyetumia muda wa uhai wake kufanya kazi na kuwatumikia Watanzania. Karume aliuawa kikatili Aprili 7, 1972. Wapinga maendeleo waliokuwa na ndoto ya kurudi tena kwa utawala wa kisultani uliopinduliwa kupitia Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964 hawakutaka aendelee kuishi, wakakatisha maisha ya shupavu huyo.
Hadi anakufa, Karume alikuwa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watanzania wanamkumbuka Karume kwa mambo mengi. Kwanza anakumbukwa kama kiongozi aliyeongoza harakati za Mapinduzi yaliyowafanya wananchi wa Zanzibar kuwa huru katika nchi yao.
Akiwa na viongozi wanasiasa wenzake jasiri, Karume aliongoza Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa kisultani na kuweka madaraka mikononi mwa wazalendo walioshika hatamu katika dola. Maamuzi magumu yaliyoyafanya kiongozi huyo, yaliwashangaza wengi. Yalikuwa ni maamuzi yaliyolenga kuleta maslahi ya wananchi na taifa la Zanzibar.
Hii ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama kilicholeta uhuru, chama cha Afro Shirazi Party (ASP). Moja ya mambo makubwa na muhimu aliyoyafanya Karume, ni kutangaza ardhi yote kuwa mali ya Taifa na kuanzisha zoezi la kugawa ardhi ekari tatu tatu kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba.
Mashamba ya ‘wavamizi’ wa Kiarabu waliyokuwa wakiyamiliki, yaligaiwa kwa wananchi ambao kwa wakati huo hawakuwa na fursa, wala uwezo wa kumiliki ardhi. Machi 11, 1964 kazi ya kugawa ardhi ya mashamba kwa ajili ya kilimo ambayo awali yalikuwa yakishikiliwa na Waarabu ilianza rasmi huko Dole Wilaya ya Kati.
Mwaka 1971, jumla ya ekari 72,000 zimegawiwa kwa wazalendo. Ilipofika tarehe 11 Machi 11, 1964 kazi ya kugawa ardhi ya mashamba kwa ajili ya kilimo ambayo awali yalikuwa yakishikiliwa na Waarabu ilianza rasmi huko Dole wilaya ya kati na ilipofika mwaka 1971 jumla ya ekari 72,000 ziligaiwa kwa wananchi wazalendo.
Karume aliwatangazia wananchi kwamba shamba lolote ambalo asili yake ni la Serikali na baadaye kuchukuliwa na Serikali ya kifisadi na kuwapa jamaa zao, basi shamba hilo litarudishwa katika mikono ya Serikali ya wananchi na kupewa wazalendo.
“Tangazo hilo liliwafurahisha wananchi wote wazalendo kwa sababu kabla ya Mapinduzi, usingeweza kujenga nyumba wala kumiliki ardhi kwa shughuli za kilimo kwa sababu ardhi yote ilikuwa mikononi mwa familia ya kifalme,” anasema Iddi Juma, mkazi wa Chwaka.
Septemba 23, 1964 shujaa huyu akatangaza ‘elimu bure’ kwa watoto wa wakulima na wafanyakazi katika Visiwa vya Unguja na Pemba na hapo, wengi wakapata fursa ya kusoma. Kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, watoto wa Kiafrika walikuwa wakisoma na kuishia darasa la nane. Hakuna aliyeweza kuendelea.
Watoto wa Kiarabu na Kihindi ndio waliokuwa na fursa za kusonga mbele kielimu. Hatua hiyo ilikwenda sambamba na kutaifishwa kwa shule kumi Julai mosi, 1964. Hizo ni shule zilizokuwa zikitoa elimu kwa njia ya kibaguzi kwa makundi ya watu wachache.
Hatua hiyo ilikwenda sambamba na kubadilisha majina ya shule ambazo kabla ya hapo zilikuwa na majina ya watawala wa kifalme zikimaanisha kwamba, hizo shule ni zao na zinapokea watoto wa familia zao tu. Baadhi ya shule zilizobadilishwa majina yaliyokuwa ya kifalme ni Aga Khan iliyopewa jina la Kidutani.
Nyingine ni Bohora School iliyobadilishwa jina na kuitwa Hamamni, pamoja na Shule ya St Monica iliyobadilishwa na kupewa jina la Mkunazini.
Shule iliyokuwa imepewa jina la King George, iibadilishwa jina na kuitwa Lumumba. Aliyekuwa Waziri wa Elimu katika Serikali ya Karume, Ali Sultani alisema alipewa kazi ya kuhakikisha elimu inaimarishwa kwa watoto wa Kiafrika pamoja na kujenga shule nyingi iwezekanavyo.
“Mzee Karume aliponiteua kuwa Waziri wa Elimu, nilipewa kazi ya kujenga shule za sekondari kila kijiji ili kupunguza masafa ya watoto kutembea kwa ajili ya kutafuta elimu,” alisema Alisema katika kipindi cha miaka mitatu pekee, zaidi ya shule mpya 10 zilijengwa vijijini pamoja na mjini. Shule hizi zilikuwa zikitoa elimu ya sekondari.
Serikali ya awamu ya saba chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein inaendelea kulinda sera ya elimu bila ya malipo kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bure kuanzia maandalizi, msingi hadi sekondari.
“Sera yetu ya elimu inakwenda sambamba na madhumuni ya kuwapatia wanafunzi wote elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari ili kuwawezesha vijana kupata elimu. Hii ilikuwa ni sehemu ya matunda ya Mapinduzi na kumuenzi Hayati Abeid Amani Karume,” alisema Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein katika kilele cha Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, mwaka huu katika Uwanja wa Amaan.
Baadhi ya mambo makubwa zaidi yanayokumbukwa kwa Karume katika kipindi cha uhai wake hadi sasa, ni pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wazo la kuwepo kwa Muungano linatokana na viongozi wa nchi mbili (Rais Karume Zanzibar, na Mwalimu Julius K. Nyerere kwa Tanzania Bara) na uhusiano wa muda mrefu unaotokana na ujirani, makabila pamoja na vyama vya siasa vilivyokuwa wakipigania uhuru wakati huo kuwa na uhusiano mkubwa.
Aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Makame Mzee alisema, kabla ya Muungano, Karume alifanya ziara katika baadhi ya mikoa ya Unguja na Pemba na kuwauliza wananchi kuhusu Muungano.
“Wapo watu wanaosema kwamba Wazanzibari hawakuulizwa kuhusu Muungano si kweli... Karume alitutembelea kijijini kwetu Mgeni Haji na kutuuliza kama mnataka muungano na wenzenu wa Tanzania Bara,” alisema Mzee.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa, anasema Karume alitembelea Pemba Aprili 30, 1964 baada ya kuungana kwa nchi mbili na kuwatajia faida za Muungano ambazo wananchi wa Pemba watafaidika nazo.
Alisema, Shehe Karume alisema Kisiwa cha Zanzibar ni kidogo ambapo Muungano unayo fursa ya wananchi wa pande mbili hizi kutembelea na kuishi sehemu yoyote. “Ndiyo maana leo wapo jamaa zangu wengi sana kutoka Pemba wanaoishi Tanzania Bara bila ya bughudha wala wasiwasi na hofu.... nenda Tandale... Buguruni hadi Mbagala (Dar es Salaam),” alisema.
Machi 23, 1964 Karume alitangaza matibabu bure kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba huku hospitali kuu iliyopo Mnazi Mmoja na zile za Kisiwa cha Pemba zikiimarishwa ili kutoa matibabu. Mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya afya kutoka hospitali 6 ziliopo Unguja na Pemba na sasa kufikia hospitali 152 huku matibabu yakitolewa bure.
Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo alisisitiza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutekekeleza Ilani ya chama cha ASP kwa kutoa matibabu bure ikiwa njia pekee za kumuenzi Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na kutekeleza sera za Serikali ya Awamu ya Kwanza ya kutoa matibabu bure ambapo tunachokifanya kwa sasa tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma hizo kwa kujenga vituo vingi zaidi vijijini na hakuna mtu anayetembea kilomita tatu kutafuta huduma za afya,” alisema.
Hayati Abeid Amani Karume bado anakumbukwa na Wazanzibari wengi kwa kutekeleza kikweli kweli dhana ya Mapinduzi kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar kupitia ilani ya chama chake cha ASP.
Kwa mfano, baada ya Mapinduzi, Karume alianza ujenzi wa nyumba za kisasa zilizopo Kikwajuni kwa kuweka jiwe la msingi Agosti, 17, 1964 kwa msaada wa iliyokuwa Ujaerumani Mashariki waliokuwa marafiki wakubwa wa Zanzibar.
“Wajerumani walikuwa marafiki zetu wakubwa walitusaidia na kutujengea nyumba za Kikwajuni,” alisema Haji Machano aliyekuwa Katibu Mwandamizi wa Umoja wa Vijana wa CCM. “Ujenzi wa nyumba za Michenzani na zile zilizopo vijijini Unguja na Pemba ni utekelezaji wa manifesto ya chama cha ASP iliyokuwa inataka kuona wananchi wazalendo wanaishi katika makazi bora ya kisasa,” alisema Baraka Shamte.
Huyo ndiye Sheikh Abeid Amani Karume, kiongozi shujaa asiyesahaulika kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliyelifanyia taifa mambo mengi na makubwa, lakini kwa wakati mfupi. Hadi anauawa kikatili, alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa chama cha ASP kilichoongoza Mapinduzi ya mwaka 1964.