Thursday

DHAMBI YA WINGEREZA KWA WAPALESTINA.

0 comments









Na: Jumaa H Heshima

Dr Kadeghe M. Katika kitabu chake cha Kingereza "Grammar and Functional English" anapinga kutafsiri majina yaani "John" kwenye "Bible" ya Kingereza akatafsiriwa kama Yohana kwenye Biblia ya Kiswahili wakati "Job" nae akaitwa "Ayubu". Kioja kikubwa kipo hapa "England" kuitwa "Wingereza".

Kwani ni nani hasa aliyeanzisha jambo hili la England kuiita Wingereza? Aliwaza nini?  Hivi ni sahihi kweli jina la Kinyakyusa "Mwafilombe" likatafsiriwa kama "Mahindi" na bado likawa ni jina la mtu husika?  Au "Tuntufye" aitwe "Tumsifu" na  "Gwamaka" aitwe "Mwenye Nguvu"? Bila shaka huu ni unajisi wa majina na lugha kwa ujumla.

Kwa minajili hiyo katika makala hii tofauti na kichwa kilivyo tutatumia jina "England" kama lilivyo kwa uasili wake na sio lile "Wingereza" la kutafsiriwa kama sio kubadilishwa.

England ni nchi inayopatikana bara la ulaya. Upande wa Kaskazini imepakana na Scotland, upande wa Kusini Magharibi imepakana na `Celtic sea', upande wa Mashariki imepaka na `North sea' na upande wa magharibi imepakana na Wales. Wakazi wa taifa hili ni Wazungu/Waengland.

Palestina ni nchi inayopatikana bara Asia, iko kwenye ukingo wa Bahari ya Maditerania. Nchi hii kwa upande wa Kusini imepakana na sehemu ya Misri na Sinai, upande wa Kaskazini imepakana na Lebanon na Syria, upande wa Mashariki imepakana na Jordan na upande wa Magharibi imepakana na Bahari ya Mediterania. Wakazi wa taifa hili ni Waarabu.

Neno dhambi linaashiria matendo mabaya yasiyokubalika katika jamii pia mbele za mungu. Neno hili dhambi limejikita sana katika maswala ya kiimani.

Katika taaluma ya Semantiki inayohusu maana katika lugha hali hii ya kufanya mambo yasiyokubalika kwenye jamii huakisiwa na maneno tofautitofauti katika mazingira anuai mfano katika kumbi za ibada hutumia neno "Sin" (dhambi) wakati Mahakamani hutumia "Crime" (kosa/hatia). Kamwe huwezi kusikia hakimu akisema mtuhumiwa ametenda "Sin" yaani dhambi bali utasikia mtuhumiwa ametenda "Crime" (kosa/hatia).

Vyovyote iwavyo andiko hili lina lengo la kuangazia mambo mabaya  yaliyofanywa na taifa la England dhidi ya Wapalestina ambayo yamepelekea mauaji ya mamilioni ya watu wasio na hatia "Innocents" pia wengine kukimbia nchi yao na kudhalilishwa kwa jina la `Wakimbizi' katika mataifa mengine.

Kitabu cha bwana Mohamed A. Cha mwaka 1982 chenye jina "Suala la Palestina" kimekua rejea kubwa katika uandishi wa makala hii.

Mashariki ya kati imekua kisiwa cha vita, mauaji na `unyama wa kinyama' kwa miaka 70 sasa (1948-2018) huku bendera ya vurugu ikipeperushwa katika ardhi ya Palestina (Palestina na Izraeli).

Mwishoni mwa aya iliyotangulia limetumika neno Palestina pekee na ufafanuzi wa kwenye mabano ndipo tukaona Palestina na Izraeli ili kueleweka, hii ni kwa sababu mpaka kufikia mwezi Mei, 1948 hakukuwa na nchi iliyoitwa Izraeli ulimwenguni na hata kwenye ramani ya dunia haikuwepo japo kuwa walikuwepo Waizraeli.

Waizraeli waliishi katika nchi mbalimbali bila kuwa na nchi yao inayowaunganisha.

Jambo hili lilipelekea kuanzishwa kwa harakati za kuwaunganisha Waizraeli ili kuwa na nchi yao.

Harakati hizo zilijulikana kama `Zionism' na kwa mara ya kwanza zilianzishwa na Myahudi wa Australia aliyeitwa Theodor Herzl, lengo kuu likiwa kutafuta nchi ya Wayahudi.

Mkutano wa kwanza wa chama cha Uzayoni ulifanyika Basle Uswisi 1897 ambao ulitokana na juhudi za bwana Herzl.

Baada ya miaka kadhaa kupita mnamo tarehe 2 Novemba, 1917 serikali ya England kupitia waziri wake wa mambo ya nje bwana Arthur J. Balfour ilitoa tamko au tangazo kumwandikia kiongozi wa Uzayoni wa wakati huo bwana Lord Rothchild juu ya swala la Wazayoni.

Tamko hilo lilitolewa kwa njia ya barua. Barua hiyo ilikua kama ifuatavyo;

"Mpendwa Lord Rothchild,

Nina furaha kukueleza, kwa niaba ya serikali ya mtukufu mfalme, tamko lifuatalo la huruma na kuunga mkono matakwa ya Wayahudi na Wazayoni, ambalo limetolewa na kukubaliwa na baraza la mawaziri.

Serikali ya mtukufu mfalme inapendelea wazo la kuanzishwa ndani ya Palestina taifa la Uyahudi, na itatumia juhudi zote iwezekanavyo ilimradi kukamilisha lengo hili, ikieleweka wazi kwamba hakutafanyika chochote kudhuru haki za kiraia na za dini za jamii nyingine zisizokua za Wayahudi katika nchi nyingine yoyote.

Nitafurahi ikiwa utalijulisha tangazo hili kwa shirikisho la Wazayoni.

Wako mkweli,
Arthur James Balfour."

Katika tangazo hili inaonekana wazi mbinu ya usaliti mkubwa wa taifa hili la kibeberu dhidi ya raia wa Palestina.

Bwana Mohamed A. Anaeleza kuwa jambo la ajabu ni kuwa England wakati inatoa ahadi hii, haikuwa na madaraka yoyote kwa Palestina, hata ya kikoloni.

Nia na ahadi hiyo ilisimamiwa vema na England kwa kutumia kila mbinu ili Wayahudi waanzishe nchi ndani ya Palestina.

Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia kuisha mwaka 1918 kulitokea mambo makuu mawili ambayo yalikua na faida kwa Serikali ya England juu ya adhma yao kwa Palestina.

Kwanza ni kuanguka kwa utawala wa Uturuki katika nchi za Kiarabu na pili ni kuanzishwa kwa Jumuia ya Kimataifa `Leage of Nations'.

Mwaka uliofatia (1919) nchi zilizokua zikitawaliwa na mataifa yaliyoshindwa katika vita ziliwekwa chini ya madaraka ya udhamini wa Mataifa yaliyoshinda.

England ilikua nchi muhimu sana kwa ubeberu kipindi hicho hivyo nchi nyingi kuwekwa chini ya udhamini wake. Moja ya nchi iliyowekwa chini ya udhamini wa England ni Palestina.

Hapa Kiswahili tunasema kuwa "Kipele kimepata mkunaji"  na vijana wa kileo nao hawataki kuachwa nyuma wao wanasema "Usiyempenda kaja".

Mtu aliyedhamiria kuisaliti nchi yenu leo hii amepata madaraka juu ya nchi yenu. Hilo ndilo lilitokea kwa Wapalestina.

Serikali ya mtukufu mfalme nchini Palestina ilitumia nguvu zake za kiutawala nchini humo kuwaalika na kuwaruhusu Wayahudi toka nchi mbalimbali ulimwenguni kuhamia na kuweka makazi yao Palestina.

Wapalestina walipinga jambo hilo vikali kwa migomo na maandamano wakiwa wamesha gutuka kuwepo kwa mbinu ya kutaka kuanzishwa nchi ya Wayahudi kwenye ardhi yao.

Mambo yalipoonekana kuwa magumu Serikali ya England iliigiza kuingilia kati na hata kutoa matamko ya kuzuia uhamiaji zaidi wa Wayahudi nchini humo ila ilikua geresha tu.

Serikali hiyo ilipoona mambo yanazidi kwenda mrama iliteua tume iliyoitwa "Tume ya Peel" (1937) kutatua mgogoro huo.

Tume hiyo ilitenda jambo baya zaidi ambalo ndilo linalomwaga damu za raia wasio na hatia mpaka hivi leo huko Palestina.

Tume ilipendekeza kugawanya kwa Palestina katika nchi mbili moja ya Wayahudi nyingine ya Wapalestina na mji wa Jerusalem ubaki kuwa mji huru wa Kimataifa.

Wazayoni walitilia nguvu zaidi swala hilo baada ya vita kuu ya pili ya duni kutokana na ukatili na mauaji toka kwa raisi wa Ujerumani, Hitler. Katika vitabu vya historia ya vita kuu za dunia yasemwa kuwa takribani Wayahudi milioni 6 waliuliwa na Hitler.

Tangu hapo serikali ya Egland ilishindwa kudhibiti vurugu zilizokua zikiendelea nchini humo kwani hata kabla ya tarehe ya kuigawa Palestina rasmi haijafika, Wayahudi walishaanza kuwaua Wapalestina na kuwafukuza katika miji yao kupitia vikundi vyao vya kigaidi vilivyojulikana kama Hoganah na Irgun.

Jumuia ya Kimataifa "League of Nations" ilishidwa kutunza amani ya dunia kwa kushindwa kuzuia vita ya pili ya dunia kutokea, hivyo ilikufa, hapo ndipo ukuzaliwa Umoja wa Mataifa "United Nations" chini ya Marekani.

Marekani ikaanza Kuuvaa rasmi mgogoro wa Palestina na Izraeli.

Baada ya England kuondoa madaraka yao ya udhamini Palestina, ndipo likatangazwa taifa la Izraeli 1948.

Hapo ndipo mambo yalikua mabaya zaidi kwani shabaha ya Wazayuni ilionekana wazi kuwa ilikua kujitanua zaidi na kufukuza Wapalestina katika nchi hiyo.

Lile pendekezo la kuigawa Palestina hawakulitilia maanani tena sasa walitaka zaidi ya kile walichopewa.

Waizareli waliendesha mauaji mengi katika vijiji mbalimbali na kupelekea Wapelestina kukimbilia nchi za jirani za Kiarabu. Waizraieli waliwaalika Wayahudi wenzao popote walipo duniani kuhamia Izraeli.

Kazi ya umoja wa mataifa (kiranja mkuu wa dunia) ni kulinda amani ya dunia lakini kwa kipindi kirefu imeshuhudia uasi wa Wayahudi dhidi ya Wapalestina bila kusema neno lolote japo kulaani tu na Izraeli muda wote imekua ikivunja makubaliano na mapendekezo ya Umoja wa Mataifa tangu wakati huo.

Mgogoro huu ni mpana sana na haitofaa kueleza kila jambo. Kuna mambo mengi yalitokea kuanzia hapo kama mataifa mengine ya Kiarabu kuungana na Palestina dhidi ya Izraeli. Lakini pia kugeuka kwa baadhi ya mataifa ya Kiarabu na kuanza kupambana na Wapalestina badala ya kuwasaidia.

Kuna mfululizo wa matukio mengi sana ya mauaji na mashambulio pia Wapalestina kuungana na kuanzisha chama chao cha ukombozi na mapambano ambacho nacho kimeendesha mashambulio na mauaji mengi kwa Wazayoni. Chama hicho kiliitwa PLO.

Harakati nyingi zilifanyika chini ya chama hicho na kufanikiwa katika mambo kadhaa ingawa bado safari ya kulikomboa taifa hilo ni ndefu.

Bila kuangalia usaliti namba mbili unaoendelezwa na Marekani kwa sasa chini ya Umoja wa Mataifa, hakika England ndio mhusika mkuu na msababishi wa mgogoro huu kutokana na ahadi yake katika tangazo la Balfour na kula njama kuwadhulumu Wapalestina.

Mauaji, mateso, udhalilishaji na uovu wote unaoendelea msababishi mkuu ni England.

Wapalestina hawako tayari kuachia ardhi yao kwa Wayahudi ndio maana huu ni mwaka wa 70 bado wanapambana na wamekua wakipanga mbinu mpya za ukombozi kila kukicha.

Mgogoro huu ulianza kumshinda England aliyeuanzisha, na sasa Marekana ndio hana dalili ya kuleta suluhisho. Majaribio takribani yote ya kuleta amani yameshindikana.

Ugumu wa swala hili ni moja, Wazayoni hawataki kuondoka Palestina kwa hoja kuwa ndio ardhi yao ya asili na Wapalestina nao hawataki kuachia nchi yao dhidi ya uvamizi na ukoloni wa Wazayoni.

Jambo pekee litakalo maliza mgogoro huu ni Wazayoni kuondoka Palestina ama kuondoka na kuwaachia Wapalestina nchi yao kwa amani au kuondolewa kwa mapambano maana imedhihirika wazi kuwa lengo lao halikua kupata makazi tu bali kulipoteza kabisa taifa la Palestina ndio maana hawakuridhika kwa kile walichopewa.

Katika baadhi ya ramani za Kimagharibi hivi leo hazioneshi nchi ya Palestina ila inaoneshwa nchi ya Izraeli.

Kwenye ramani nyingine sehemu hiyo ndogo ambayo Palestina ndio wamebaki nayo imeandikwa "Undetermined" yaani haitambuliki. Ni wazi kuwa lengo halikuwa kuigawa Palestina bali kuifuta kabisa katika uso wa dunia.

Nasimama upande wa Wapalestina kupinga ukoloni wa Wazayoni nchini humo na naamini Wapalestina watashinda hata baada ya miaka 500.

                    *MWISHO*

Mwandishi: Jumaa H Heshima
                     Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
                     0714-638277
                     11-01-2017.