
Imam mkuu nchini Misri ameidhinisha marufuku dhidi ya biashara ya sarafu ya kidijitali ya Bitcoin akisema ni "haramu" kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.
Mufti mkuu Sheikh Shawki Allam amesema sarafu hiyo ina hatari nyingi za "kutokea kwa utapeli, ulaghai na kutokuwepo na ujuzi".
Bitcoin ilianza kuuzwa mwaka jana ikiuzwa chini ya $1,000 (£737) lakini kufikia mwisho wa mwaka ilikuwa ikiuzwa $20,000.
Baadaye, ilipoteza thamani kwa 25% katika kipindi cha wiki moja, na kuzua hofu miongoni mwa wawekezaji.
Mufti Mkuu huyo amesema hatari zinatokea kutokana na hali kwamba hakuna anayeisimamia sarafu hiyo wakati btc 1= $17,000
"Bitcoin ni haram kwa mujibu wa Sharia na inawadhuru watu binafsi, makundi na taasisi," amesema kwa mujibu wa gazeti la Ahram.
Soko la kwanza la Bitcoin lilifunguliwa Agosti 2017 nchini Misri.
Mwezi jana, serikali iliharamisha sarafu hiyo.
Mshauri wa Mufti Mkuu, Magdy Ashour, aliambia gazeti la Egypt Today kuwa Bitcoin inatumiwa "kuwafadhili magaidi moja kwa moja".
Wakosoaji wa fedha hizo wamesema kupanda thamani kwake kwa sasa ni "puto hatari" kama ilivyofanyika kwa dotcom, lakini wengine wanasema kupanda bei kwake kunatokana na kuanza kukubalika kwa fedha hizo.
"Bitcoin kwa sasa ni kama treni inayoongeza kasi zaidi na zaidi ilhali haina breki," amesema Shane Chanel wa shirika la kifedha la ASR Wealth Advisers la Sydney.
Ingawa watu wengi wamewekeza mabilioni ya dola katika Bitcoin, thamani ya jumla ya $268bn ya fedha hizo kwa jumla bado ni ndogo ukilinganisha na aina nyingine za mali au fedha.