Hii inatokana na Facebook kuitaarifu polisi nchini Dernmark kuhusu vijana wapatao 1,004
Si kitu cha ajabu kwa mtandao wa Facebook kutoa taarifa wakati kunapokuwepo na ushahidi wa vitendo vya uhalifu, lakini tukio la hivi karibuni ni tofauti na linaweza kuwa na athari kuliko kawaida.
Hii inatokana na Facebook kuitaarifu polisi nchini Dernmark kuhusu vijana wapatao 1,004 (baadhi wakiwa na umri chini ya miaka 18) baada ya kugundua kuwa watumiaji wake wa Messenger walikuwa wakitumiana video zinazoonyesha watoto wawili walio na umri chini ya miaka 15 wakifanya mapenzi, kwa mujibu wa Engadget.
Kitendo hicho ni kukiuka sheria inayozuia usambazaji wa picha zisizo za maadili za watoto. Wengi walioshiriki kutuma (kushare) video hiyo walifanya hivyo mara chache, polisi ilisema, lakini wengine walituma mara nyingi.
Polisi walisema waliotuma mara nyingi walijua wanafanya nini japokuwa hawakujua kuwa ni kinyume cha sheria.
Yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliwa na adhabu ya kifungo cha siku 20 jela, lakini pia wataandikishwa kwenye daftari la wahalifu na kutofutwa kwa miaka kumi ijayo.
Video za mwisho zilitumwa mwishoni mwa majira ya kipupwe mwaka 2017, lakini mashtaka yameibuka sasa kwa kuwa shauri hilo ni kubwa na gumu, kwa mujibu wa polisi.
Uchunguzi ulihusisha ofisi nne za polisi nchini Dernmark na umeibuka baada ya mamlaka nchini Marekani kutoa onyo kwa Facebook ambalo lilipelekwa pia kwa polisi wa barani Ulaya (Europol).