Na CHRIS A.
Wa
MASSHELE BLOG
Dhana ya lahaja ni changamano kwa kuwa hutokana na jinsi mtu anayefasili dhana yenyewe anavyotumia ama kigezo cha isimujamii au cha kiisimu katika ufafanuzi wake.
DHANA ya lahaja ni changamano kwa kuwa hutokana na jinsi mtu anayefasili dhana yenyewe anavyotumia ama kigezo cha isimujamii au cha kiisimu katika ufafanuzi wake.
Kigezo cha isimujamii huwashirikisha wanajamii au wazungumzaji wa lahaja fulani na ukapata msimamo wao kuhusu lahaja hiyo. Kigezo cha kiisimu hutofautisha lugha na lahaja nyingine kwa kuzingatia msamiati wa msingi, fonolojia pamoja na mofolojia.
Lahaja pia inaweza kufasiliwa kwa kuzingatia utengano wa kijiografia au kijamii. Hii ina maana kwamba, unaweza kusikia kuwa, lahaja fulani inazungumzwa mahali fulani au huzungumzwa na kundi fulani la watu. Mfano, lahaja ya Kitumbatu huzungumzwa katika sehemu za kisiwa cha Tumbatu na vivyo hivyo lahaja ya Kipemba huzungumzwa na watu wa Pemba.
Mwandishi Msanjila katika kitabu chake cha Lugha na Utambulishaji wa jamii, anasema lahaja ni lugha mojawapo kati ya lugha ambazo kimsingi huhesabiwa kuwa lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au muundo kutokana na eneo lugha hiyo inazungumzwa.
Katika kitabu cha Historia ya Kiswahili Sanifu kilichoandikwa na Massamba, anadhihirika kuwa, lahaja ni lugha mbalimbali za Pwani zilizokuwa na uhusiano wa karibu sana.
Lugha hizo ni kama vile Ci-mbalazi, Ki-amu, Ki-mvita, Ki-jomvu, Ki-mtang’ata, Ki-makunduchi, Ki-tumbatu, Ki-mgao na Ki-unguja ambazo wataalamu wengine wanaziita lahaja mfano,Ukizitazama fasili hizi kwa makini utagundua kuwa, kila mtu ana mtazano wake kuhusu lahaja, wengine wanasema ni vilugha, ni lugha inayojitegemea, wengine wanasema ni tofauti ndogondogo hasa za kimatamshi katika lugha moja.
Lakini pia wengine wanaona lahaja ni tofauti za lugha kwa kigezo cha kijiografia na wengine wanaona ni tofauti za kijamii na kijiografia. Kwa hiyo mitazamo hii ndio huleta utata na uchangamano katika kufasili dhana ya lahaja.
Kimsingi fasili iliyotolewa na Msanjila inaweza kutusaidia kujua dhana ya lahaja kwani fasili hii ni ya kiutendaji.
Mjadala kuhusu idadi ya lahaja za Kiswahili na namna zilivyoinukia ulianza kitambo na hadi sasa hivi hakuna utafiti wa hivi karibuni unaoweza kutusaidia kuthibitisha idadi kamili za lahaji za Kiswahili.
Lahaja 20
Katika kitabu cha 'Historia ya Kiswahili’ chake Chiraghdin na Mnyampala kumetajwa idadi ya lahaja ishirini zikiwemo Kiunguja, Kimrima, Kimgao, Kimvita, Kihadimu, Kipemba, Kirumba, Kiamu, Kipate, Kisiu, Kitikuu, Kingazija, Kingozi, Kitumbatu, Kimtang’ata, Chichifundi, Chibalanzi, Kingwana, Kinyare na Kijomvu.
Nurse na Spear katika ’Reconsructing the History’ of Language wametaja idadi ya lahaja kumi na sita na wamezigawa katika makundi mawili ambayo ni kundi la Kaskazini na la Kusini.
Kundi la Kaskazini lina lahaja saba wakati la Kusini lina tisa. Baadhi ya lahaja hizo ni Kipate, Chimiini, Kibajuni, Kisiu, Kijomvu, Chifunzi, Kipate, Kiunguja, Kimtang’ata na Kimakunduchi. Utata kuhusu idadi za lahaja za kiswahili unatokana na sababu zifuatazo:
VIGEZO
Unaweza kufanya utafiti wa lahaja za Kiswahili kwa kutumia kigezo cha kijiografia, kijamii, pamoja na kiisimu. Vigezo hivyo vyote vinaweza kukupatia idadi tofauti za lahaja mfano, Massamba katika utafiti wake kwa kutumia kigezo cha kiisimu, alifanya utafiti katika jamii za Chi-ruri, Chi-jita, na Ki-kwaya akathibitisha kuwa hizi ni lahaja za lugha moja na si tofauti.
Pia kwa kutumia kigezo cha utengano wa kijiografia na kijamii mfano katika lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa uanishaji umefanywa kwa utengano wa kijiografia kama vile, Kipate kinazungumzwa sehemu za Pate na lahaja ya Kipemba huzungumzwa Pemba.
Hivyo kutokana na sababu kama hizi husababisha watafiti wengi kutofautiana katika kupata idadi kamili za lahaja.
UKURUBA
Kutokana na kusigana kwa namna fulani kwa lahaja za Kiswahili, kukurubiana huko kwa lugha na mipaka ndiko kunakofanya wazungumzaji wake wajihisi wanazungumza lugha moja. Pia kusigana kwa lahaja hizi husababisha hawa watu wajihisi wanazungumza lugha tofauti.
MAJINA
Kutokana na kutofautiana kwa majina ya lahaja, kuna baadhi ya majina ya lahaja moja hutajwa tofautitofauti na wataalamu mbalimbali, mfano Chiraghdin na Mnyampala (1977) anataja jina la lahaja ya Kihadimu, anasema lahaja ya Kihadimu aliita Kimakunduchi.
Vivyo hivyo Nurse na Spear (1985) wanasema lahaja hiyo ni Kimakunduchi. Hivyo inaleta utata katika kujua kwamba hii ni lahaja moja au ni lahaja mbili tofauti.
MAENDELEO
Kutokana na maendeleo ya Kiswahili sanifu, mfano mpaka sasa kuna baadhi ya lahaja zimebakia kimaandishi lakini kiuhalisia hazipo na hazitumiki katika Kiswahili.
Mfano, lahaja ya Kimgao iliyokuwa inapatikana sehemu za Kilwa imo kwenye maandishi ya wataalamu kama vile Chiraghdin na Mnyampala (1977), Nurse na Spear (1985).
Lakini watumiaji wake hivi sasa wanatumia Kiswahili sanifu, kwa hiyo inaleta utata katika kupata idadi kamili ya lahaja za Kiswahili
Pia kuna baadhi ya lahaja zipo na zinatumika lakini bad
o hazijahifadhiwa katika maandishi, mfano Kiunguja.
+255766605392