Sunday

Chadema walia kuchezewa rafu na CCM Moshi

0 comments


Zoezi la upigaji wa kura katika kata nne za majimbo ya Hai na Moshi mjini leo Jumapili limefanyika kwa amani huku Chadema ikilalamika kuchezewa rafu na CCM kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Moshi mjini, Priscus Tarimo, amesema hawaelewi msingi wa malalamiko ya Chadema, wakati Jeshi la Polisi wajibu wake ni kudhibiti uhalifu.

“Polisi wanachokifanya ni kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani. Polisi hawawezi kukaa kimya wakati vijana wa Chadema wanatishia amani. Lazima wakamatwe,” amesema.

“Salama yao ni kupiga kura na kurudi nyumbani waache vyombo vifanye kazi yao. Uchaguzi unasimamia na sheria na kanuni na polisi wanasimamia ili zisimamiwe,” amesisitiza Tarimo.

Katibu huyo amesema uchaguzi huo ulikwenda vizuri kwa vile vituo vilifunguliwa kwa wakati na wananchi walipiga kura kwa amani tofauti na Chadema walivyokuwa wakilalamika.

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema amesema awali walifikiri wanaingia kwenye uchaguzi huru na wa haki lakini wamegundua wameingia kwenye vita ya udiwani.

“Hapa ninapozungumza na wewe Mwenyekiti wa Kijiji cha Shiri Mgungani (hakumtaja) amekamatwa sasa hivi na polisi. Pale Mferejini vijana wetu wa boda boda walikamatwa asubuhi,” amesema Lema.

“Pale Weruweru kitongoji cha Upareni ni kama mkutano wa hadhara. CCM wanawafundishwa wapiga kura na hakuna hatua zinachukuliwa. Sielewi nchi inaelekea wapi,” alisisitiza Lema.

Lema amesema ni kutokana na hali hiyo ya kamatakamata ya Polisi, imesababisha watu waliojitokeza kupiga kura kuwa wachache kuliko ilivyotarajiwa kutokana na kuhofia kukamatwa.