Wednesday

LUGHA INAVYOHUSIANA NA MAZINGIRA YA JAMII

0 comments


 
Kwa Mukhtasari
Kama zao la amana ya jamii, lugha ni kitendo cha jamii kwani ni sehemu ya utamaduni wa jamii husika. Lugha ni njia inayotumiwa na wanajamii ili kueleza na kusambaza utamaduni wake.



LUGHA ni mfumo wa sauti nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku ili kueleza mawazo, hisia na mahitaji yao.
Kusema kuwa lugha ni mfumo ina maana kwamba lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali ambavyo kwavyo ni sauti, silabi, neno na sentensi.
Vipashio hivi hushirikiana kwa pamoja ili kuunda tungo zenye maana zinazokubalika. Ikiwa tungo hizi hazina maana - na hivyo haziwasilishi ujumbe wowote wenye mantiki - basi haziwi lugha kwa sababu lugha ni mfumo wa mawasiliano. Jamii ni kundi la watu wanaoishi katika eneo fulani, wanaojitambulisha na upekee wa kundi moja, wenye utamaduni mmoja na lugha moja.
Isimujamii ni tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano uliopo baina ya mawili hayo. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika miktadha tofauti; aina mbalimbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.
King’ei (2010), anaeleza kuwa lugha ni zao la jamii, na ni kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika.
Pili, lugha hutumiwa na jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalum cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo, isimujamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu baina ya lugha na jamii ambayo ndiyo mzazi wa lugha ya binadamu.
Kama zao la amana ya jamii, lugha ni kitendo cha jamii kwani ni sehemu ya utamaduni wa jamii husika. Lugha ni njia inayotumiwa na wanajamii ili kueleza na kusambaza utamaduni wake.
Wanaisimu, Sapir na Whorf (1972), wanaeleza kuwa lugha huathiri sana na kudhibiti jinsi wazungumzaji na watumiaji wake katika jamii fulani wanavyoufasili ukawaida wa ulimwengu wao. Kulingana na wanaisimu hawa muundo wa maana katika lugha ndiyo msingi wa mawazo au utaratibu wa fikira.
Mwanadamu hawezi kufikiri kamwe bila ya kutumia lugha. Jambo hili linamaanisha kuwa kwa vile mawazo na fikira za mwanadamu vinaukiliwa na lugha basi inawezekana kudhibiti fikra za wanajamii kwa kuidhibiti matumizi ya lugha yao.
Katika miktadha ya nchi nyingi za Kiafrika, hili limethibitika kwani miongoni mwa wanajamii, wengi wanahusisha maarifa na lugha fulani (mathalani Kiingereza). Hii inatokana na imani iliyochapuliwa na wakoloni kwamba Kiingereza ni lugha ya ustaarabu na ya kitaaluma. Hivyo uwezo wao wa kudhibiti matumizi ya lugha kwa kututoa katika matumizi ya lugha za kwanza (za mama) yamefanikisha kuelekeza fikra za wanajamii hawa kwenye mawazo kwamba taaluma na usomi ni kujua Kiingereza na lugha nyingine za kigeni.
Kwa mujibu wa King’ei (2010) lugha yoyote iwayo hurejelea mazingira ya jamii husika, na ndiyo maana watu wenye lugha sawa na wanaishi katika mazingira tofauti wanaweza kuwa na mitazamo tofauti ya kimaisha na ufasili wao wa ulimwengu. Kwa kutumia nadharia ya Ukiliaji wa Kiisimu (Linguistic Determinism), lugha ndiyo inayoongoza mawazo ya watu na huathiri hata maana ambazo watu huzitoa kuelezea dhana na mitazamo fulani katika maisha ya kila siku.
Kwa njia ya lugha, watu wa jamii fulani wanapata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya jamii. Isitoshe, Austin (1962) anasema kuwa, ni muhimu kuhusisha matumizi ya lugha na muktadha wake wa kijamii kwani lugha huwa na matumizi tofauti kama vile kutoa mapendekezo, kuahidi, kukaribisha, kuomba, kuonya, kufahamisha, kuagiza, kukashifu, kusifu na kuapiza. Lugha ndicho chombo kinachotumika kuwaleta pamoja na kuwaunganisha wanajamii huku ikisaidia kuimarisha uhusiano miongoni mwa wanajamii hao kadri wanavyopania kudumisha ushirikiano.
Katika muktadha wa Kiafrika, kwa mfano, heshima ya mtu inatambulishwa na jamii ya watu ndiyo maana Waswahili wana msemo unaosema “mtu ni watu”.
Kauli hii kwa ujumla inatuonyesha kuwa katika harakati za maisha ya wanajamii, heshima na kukubalika kwa mtu pamoja na kueleweka kwake kunatokana na namna mtu anavyohusiana na wanajamii wengine pamoja na kutumia lugha kwa ufasaha.
Haya yote yanawasilishwa kutoka katika jamii moja hadi katika nyingine kwa kutumia lugha ambayo ndiyo nyenzo muhimu ya kudumisha mawasiliano. Sidhani yapo manufaa yoyote mengine ya lugha nje ya kutimiza kiini kikuu cha mawasiliano. Ingawa hivyo, mawasiliano hayo baadaye ndiyo yawezayo kuzalisha mafanikio mengine katika maisha ya kila siku.
Mtu binafsi
Licha ya jamii kutambulika kwa kutumia lugha, lugha ni kitambulisho kamili cha mtu binafsi. Lugha huwa na uwezo wa kuonyesha sifa fulani kuhusu mzungumzaji, anayerejelewa na uhusiano uliopo kati ya wanajamii.
Utamaduni hutambulishwa katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu kwa kutumia lugha pia. Kwa mfano, katika fasihi, tunatambua mambo mbalimbali yanayohusu jamii tofauti hasa katika kipera cha maigizo yahusuyo majigambo kutokana na namna wanajamii wanavyotumia lugha yao kujipambanua kwa jamii nyingine.
Lugha pia hutumika katika kurithisha mila, itikadi na desturi za jamii ikiwa pamoja na jukumu la kutolea elimu kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Binadamu huweza kufunzwa na kupewa maadili mbalimbali kwa kutumia lugha ili waweze kujitambua kuwa wao ni akina nani na wapo ulimwenguni kwa sababu zipi.
Kwa mfano, watoto huweza kufunzwa masuala yanayohusu uana wao ambao hutokana na jinsia yao; vijana wanaoshiriki sherehe za jando na unyago wanafunzwa masuala ya utu-uzima kwa kutumia lugha. Katika kuwapa mawaidha, wasichana kwa wavulana hufunzwa kuhusu unyumba na kuelekezwa ipasavyo kimaadili.
Pamoja na kuwa wanajamii wanaona matendo yanayotendwa ndani na nje ya jamii, wanahitaji namna ambavyo daima wataona wema ukishinda uovu na athari za kuteua ama kufuata au kutofuata matendo hayo.


No comments:

Post a Comment