Tuesday

TATIZO LA MWANAMKE KUKOSA SIKU ZAKE.

0 comments

Sikujua ni binti wa miaka 22. Tangu amezaliwa hajawahi kupata siku zake, hajavunja ungo. Sasa hivi sikujua ana mchumba. Hata hivyo ana wasiwasi juu ya hatma ya uhusiano wao kutokana na hali yake. Anajiuliza je, lini atavunja ungo? Je, anaweza kupata watoto? Je, anaweza kufanya tendo la ndoa bila matatizo? Je, hali yake inatibika?
Sikujua ni binti wa kufikirika lakini wapo wasichana wengi wenye matatizo na maswali kama ya Sikujua.
Hali ya msichana kutokupata siku zake mpaka anazidi miaka 16 inaitwa primary amenorrhea. Hali hii huweza kutokea kwa msichana ambaye ukuaji wake wa mwili na kupevuka kwake ni kwa kawaida au kwa wasichana ambao wana matatizo ya ukuaji na kupevuka.
Sababu zinazosababisha tatizo hili ni

1. makosa wakati urutubisho wa yai kabla ya kuzaliwa. Wasichana wa namna hii huzaliwa bila kuwa na seli za uzazi zilizokamilika, jambo linalosababisha washindwa kutoa mayai kama inavyopaswa. Wasichana hawa wanaweza kufanya tendo la ndoa bila matatizo iwapo hawana tatizo lingine la kimaumbile. Hata hivyo ni muhimu sana wasichana hawa kfanyiwa upasuaji na kuchukua kipande cha ovari kwa ajili ya vipimo vya maabara ili kuhakikusha kutokuwepo kwa vinasaba vinavyoweza kusababisha kupata kansa (ovarian dysgeminoma) baadae.
Wakati mwingine matatizo haya husababisha kutokukua kabisa kwa kifuko cha uzazi na sehemu ya uke. Ugonjwa huu unaitwa Rokitansky syndrome. Wasichana hawa wanaweza kufanyiwa upasuaji ili waweze kufanya tendo la ndoa lakini hawawezi kupata hedhi wala kupata mtoto kwa vile hawana kifuko cha uzazi.

2. Njia ya uzazi kuziba. Hili ni kundi la wasichana ambao damu ya hedhi haitoki kwa vile njia ya uzazi imeziba. Wasichana hawa mara nyingi husikia maumivu ya tumbo yanayojirudia kila mwezi. Maumivu haya husababishwa na mkusanyiko wa damu inayokosa njia ya kutoka. Wasichana hawa wanaweza kufanya tendo la ndoa iwapo kuziba huko hakujahusisha uke.
Tatizo hili hutatuliwa kwa upasuaji wa kufungua sehemu iliyoziba na msichana hupata ujauzito na kujifungua bila matatizo. Iwapo njia iliziba kiasi kikubwa na upasuaji umeacha kovu, inaweza kushauriwa kujifungua kwa upasuaji ili kuepuka kupasuka na kupoteza damu nyingi.

3. Wembamba kupitiliza. Kumekuwa na mtindo na tabia ya wasichana kujinyima chakula ili wawe wembamba. Tabia hiyo ikipitiliza husababisha msichana kutokupata siku zake. Magonjwa ya tabia za kuogopa kula ni anorexia nervosa na bulimia. Msichana huyo alipata tiba itakayomuwezesha kubadili tabia na kula chakula bora cha kutosha hupona na kuweza kuishi kama kawaida. Picha inaonyesha mfano wa msichana mwenye ugonjwa wa anorexia nervosa.

4. Mazoezi makali na stress. Hili linawahusu hasa wasichana wanaoshiriki michezo na mashindano mbalimbali. Tiba yake ni kupunguza stress na kufanya mazoezi kwa kipimo.

5. Uvimbe kwenye ubongo. Kunapokewa na hali hii mara nyingi msichana pia huwa na maumivu ya kichwa na matatizo ya kuona. Hii ni kwa sababu sehemu ya ubongo inayohusika na hedhi iko karibu na mishipa ya fahamu ya macho. Hali inahitaji kupimwa na daktari na hutibiwa kwa dawa au upasuaji kutokana na ukubwa na aina ya uvimbe. Wasichana waliopata matibabu sahihi hupona na kuendelea na maisha ya kawaida katika mahusiano pamoja na kujifungua bila matatizo.

6. Matatizo ya mfumo wa hormone. Hili hutokeo kwa wanawake wengi sana. Iwapo tatizo hilo litatokea kabla msichana hajavunja ungo, husababisha msichana kutokuvunja ungo na kushindwa kupata mtoto. Matatizo haya hutibika kwa kutumia dawa zenye hormone anayokosa mgonjwa au kwa kutumia dawa inayopunguza hormone iliyozidi. Wasichana hupona na kuishi maisha ya kawaida ya mahusiano na kupata watoto.

7. Ujauzito usio wa kweli ( pseudocyesis). Hii ni hali inayomtokea msichana/mwanamke ambaye kisaikolojia anajihisi kama mjamzito na anaweza kuwa na dalili zote za ujauzito lakini kiuhalisia sio mjamzito. Hali hii hutokea mara chache sana, sio ugonjwa wa kawaida, lakini ni mojawapo ya sababu ya msichana kukosa siku zake.
Nini cha kufanya kwa msichana mwenye matatizo haya?
Matatizo ya kuchelewa kuvunja ungo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na daktari. Hii ni kwa sababu hali hiyo inaweza kuashiria uwepo wa ugonjwa mwingine, vilevile ni vizuri kujua kuwa hali hiyo mara nyingi hutibika.

Daktari atakuuliza maswali kuhusu afya yako na kukupima. Utafanyiwa ultrasound, vipimo vya damu na vipimo vingine kutokana na matokeo ya vipimo vya awali.
Baada ya chanzo cha ugonjwa kufahamika utapewa ushauri nasaha na kupewa fursa ya kuuliza maswali. Halafu utaambiwa aina za matibabu yanayokufaa. Baada ya hapo utaanza matibabu.
Sehemu muhimu ya matibabu ya hormone ni ushirikiano wa mgonjwa kutumia dawa kama jinsi alivyoshauriwa na daktari

No comments:

Post a Comment